Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia ya wahamiaji wa Kiethiopia warejea nyumbani kwa hiyari kutoka Yemen:IOM

Wakimbizi wa Ethiopia wanajiandaa kusafiri kwa njia ya ndege hadi Ethiopia kwa ufadhili wa IOM kutoka
IOM/Avand Hasan
Wakimbizi wa Ethiopia wanajiandaa kusafiri kwa njia ya ndege hadi Ethiopia kwa ufadhili wa IOM kutoka

Mamia ya wahamiaji wa Kiethiopia warejea nyumbani kwa hiyari kutoka Yemen:IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limeanza tena oparesheni zake za hiyari kuokoa maisha kwa kusafirisha wahamiaji VHR kutoka Yemen hadi Ethiopia mwezi huu na linalenga kuwasaidia wahamiaji wasiopungua 6,750 wanaotoka Ethiopia kuondoka katika nchi hiyo iliyoathiriwa na migogoro.

Zaidi ya wahamiaji 600 wa Ethiopia ikiwa ni pamoja na watoto 60 wahamiaji wasio na walezi wamesafirishwa hadi sasa na wamewasili Addis Ababa kutokea Aden katika safari tatu za kwanza za ndege za VHR zilizofanyika mwaka huu . Safari za ndege za ziada zimepangwa kuondoka kutoka Yemen hadi Ethiopia katika wiki zijazo, lakini msaada mkubwa unahitajika haraka kusaidia wale wote wanaotaka kurejea nyumbani kwa hiyari.

Maelfu ya wahamiaji waliokwama nchini Yemen wameelezea nia yao ya kutaka kurejea Ethiopia kwa hiari.

Shirika la IOM sasa linaomba dola milioni 7.5 ili kuwapa usaidizi wa kurudi salama, wenye heshima na wa hiari, pamoja na msaada wa huduma za afya na ulinzi

IOM inatoa msaada mkubwa

IOM nchini Yemen inapanga safari za ndege, inatoa ushauri nasaha kabla ya wahamiaji kuondoka, inasaidia katika hati za kusafiria na huwasiliana na mamlaka ili kuhakikisha njia salama za kupita na usafiri.

Baada ya kuwasili nchini Ethiopia, wahamiaji hao wanaorejea hupewa chakula, malazi ya muda, msaada wa matibabu, ushauri nasaha na huduma nyinginezo.

"Wahamiaji wanaopitia au kukwama Yemen ni baadhi ya wale walioathirika zaidi na hali mbaya ya kibinadamu nchini humo. Wanastahimili hali zinazohatarisha maisha yao na kufika kila siku katika vituo vya vya kuchukua hatua vya IOM baada ya kukabiliwa na unyanyasaji wa kinyama kama vile kuwekwa kizuizini kiholela, kuhamishwa kwa lazima, unyonyaji na mateso. VHR ndiyo chaguo pekee la kurejea salama kutoka Yemen na ni njia ya kuokoa maelfu ya wahamiaji waliokwama.” amesema Christa Rottensteiner, mkuu wa ujumbe wa IOM nchini Yemeni.

Ibrahim, mmoja wa wahamiaji waliorejea Ethiopia wiki iliyopita, amesema “Nilipigwa risasi mguuni na wasafirishaji haramu. Baada ya yote yaliyonipata, nina furaha kurudi nyumbani kwa familia yangu na ninawashauri wengine waepuke njia hii hatari.”

Wakati huo huo, katika operesheni tofauti, IOM inafanya kazi kwa karibu na washirika wengine kusaidia Serikali ya Ethiopia huku nchi hiyo ikiendelea kupokea maelfu ya Waethiopia waliofukuzwa kutoka ufalme wa Saudi Arabia (KSA).

Zaidi ya wahamiaji 25,000 wa Ethiopia wamerudishwa na serikali ya Saudi Arabia tangu Machi 30 kufuatia makubaliano kati ya serikali ya Ethiopia na Saudi Arabia.

Wahamiaji zaidi watarejeshwa miezi ijayo

Katika miezi ijayo, wahamiaji wengine 75,000 wa Ethiopia watarejeshwa chini ya operesheni ya sasa ya hiyari.

Hatua zilzioratibiwa za sekta mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha wanaorejea wanapata huduma muhimu kama vile matibabu, chakula, malazi na usaidizi wa kisaikolojia na pia huduma maalum za ulinzi ili kupunguza mahitaji yao ya haraka, hatari na udhaifu na kuwawezesha kurudi nyumbani kwa usalama na heshima.

Kwa mujibu wa shirika hilo la wahamiaji ufadhili mkubwa unahitajika ili kutoa msaada muhimu wa kibinadamu kwa wahamiaji wanaorejea.

Washirika wa IOM na mpango wa makubaliano na wahamiaji kwa Pembe ya Afrika na Yemen (MRP) wanaomba dola milioni 11 ili kuweza kutoa msaada baada ya kuwasili kwa watu waliorejea.

Tangu mwaka 2017, KSA imewarejesha karibu Waethiopia nusu milioni. Kuna mamia ya maelfu ya Waethiopia wanaoishi katika Ufalme huo kwa sasa, kulingana na takwimu za mamlaka ya Ethiopia, na wanaweza kuhitaji msaada zaidi watakapowasili Ethiopia iwapo pia watarejeshwa.

Msaada wa kibinadamu na huduma za ulinzi za IOM katika kukabiliana na mahitaji ya wanaorejea zinawiana na mpango wa Kikanda wa kukabiliana na wahamiaji katika Pembe ya Afrika na Yemen, 2022.

Mpango wa MRP unalenga kushughulikia mahitaji ya wahamiaji walio katika mazingira hatarishi na jumuiya zinazowakaribisha katika nchi walizopo.

kando ya njia ya uhamiaji ya Mashariki, iliyoko kati ya Pembe ya Afrika na Yemen, kwa msaada mkubwa wa kifedha wa ofisi ya idara ya idadi ya watu, wakimbizi na uhamiaji ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani, shirika la maendeleo ya kimataifa la Uswis na ulinzi wa raia wa Ulaya na operesheni za misaada ya kibinadamu wahamiaji hao wanasaidiwa.