Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waethiopia waliokwama Yemen wasaidiwa kurudi nyumbani kwa hiari: IOM

Wahamiaji warejea nyumbani kwa hiari. Picha: IOM

Waethiopia waliokwama Yemen wasaidiwa kurudi nyumbani kwa hiari: IOM

Amani na Usalama

Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM limeanza kusaidia wahamiaji 418 kutoka Ethiopia waliokuwa wamekwama nchini Yemen waweze kurejea nyumbani salama kupitia mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari, VHR.

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo mjini Sana’a Yemen na Addis Ababa, Ethiopia imesema safari hizo za kurejea nyumbani zinafanyika kwa ndege, ikiwa ni mara ya kwanza tangu baada ya kuanza kwa mzozo nchini Yemen mwaka 2015.

Naibu Mkuu wa IOM nchini Yemen, John McCue amefafanua sababu ya kuanza tena safari hizo akisema,“kulingana na wajibu wetu wa kutoa huduma za uhamiaji salama kwa wote, sasa tunaanza safari zetu hadi Addis Ababa. Mwanzo ni wahamiaji 102 ndio watatangulia hususan wale walio na shida yaani wagonjwa na watoto ambao hawana wasaidizi  na opersheni hii itaendelea kwa siku nne, na tunatumaini kuwa tutafanya hivyo hapo baadaye kwani ndiyo njia salama kuwafikisha wahamiaji nyumbani.”

Waethiopia hao waliondoka jana kutoka uwanja wa ndege wa  kimataifa wa Sana’a hadi uwanja wa kimataifa wa Bole huko  Addis Ababa Ethiopia  na safari zingine tatu zimepangwa leo na kesho alhamisi na tena wahamiaji wengine 316 watafuata baadaye.

IOM inasema kuwa zaidi ya robo ya abiria 418 ambao ni sawa na wahamaji 121 ni watoto.  IOM imewasaidia wahamiaji wengi kurejea kwao kwa hiari katika kipindi cha miezi sita iliyopita, na tayari mpango wa hiari wa IOM wa VHR umesaidia wahamiaji 668 kurejea Ethiopia mwaka huu wa 2018 kwa kutumia meli kuvuka ghuba ya Aden.

Hata hivyo juhudi hizo zinakwamishwa na hali mbaya ya mapigano kuzunguka mji wa Hudaidah pamoja na hali ya hewa ambayo haitabiriki.

Tags:IOM, VHR,Yemen, Ethiopia, wahamiaji,Aden