Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 34 wafa maji bahari ya Sham- IOM

Wafanyakazi wa IOM huko Obock,Djibouti wakielekea kwenye eneo la Bahari ya Sham kusaidia mamlaka za Djibouti katika kusaka manusura na maiti za watu waliozama baharini.
IOM
Wafanyakazi wa IOM huko Obock,Djibouti wakielekea kwenye eneo la Bahari ya Sham kusaidia mamlaka za Djibouti katika kusaka manusura na maiti za watu waliozama baharini.

Wakimbizi 34 wafa maji bahari ya Sham- IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Watu 34 wamekufa maji baada ya boti walimokuwa wakisafiria kukimbia machafuko nchini Yemen kuzama kwenye bahari ya Sham ikiwa njiani kuelekea Djibouti.

 

Taarifa ya shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, hii leo huko Obok, nchini Djibouti imesema boti hiyo inamilikiwa na wasafirishaji haramu wa binadamu ilikuwa imebeba wahamiaji 60 na imezama asubuhi ya leo kwa saa za Djibouti.
IOM inasema hata hivyo hadi sasa haijafahamika chanjo cha kuzama kwa boti hiyo.
Tukio hili la karibuni ni miongoni mwa matukio yanayotokea kila mwaka kwenye eneio hilo ambapo maelfu ya vijana wa kiafrika wanafanya safari za hatari kutoka nchi kama vile Somalia, Eritrea na Somalia wakipitia Djibouti na Yemen ili kwenda kusaka maisha bora katika nchi za ghuba.

IOM inasema janga la coronavirus">COVID-19 linalazimisha watu kurejea nyumbani kutokanana mipaka kufungwa.
Mwezi uliopita, wasafirishaji haramu wa binadamu waliwatupa kwenye bahari ya Sham watu 80 waliokuwemo kwenye boti kwa madai kuwa boti hiyo ilikuwa inazama baada ya kubeba watu wengi kupindukia. Watu watano kati ya hao walikufa maji.

Licha ya hatari hizo, wahamiaji wanaendelea kumiminika Djibouti kutokea Yemen ambapo mwezi Machi pekee, wahamiaji zaidi ya 2,343 waliwasili Djibouti kutokea Yeen, ikilinganishwa na mwezi uliotangulia wa Februari ambapo idadi illikuwa 1,900. Idadi kubwa walikuwa wanarejea nyumbani Ethiopia na Somalia.

Mwezi uliopita, wasafirishaji haramu wa binadamu waliwatupa kwenye bahari ya Sham watu 80 waliokuwemo kwenye boti kwa madai kuwa boti hiyo ilikuwa inazama baada ya kubeba watu wengi kupindukia- IOM

Mkuu wa IOM nchini Djibouti, Stephanie Daviot anasema kile ambacho IOM inafanya hivi sasa ni kushirikiana na mamlaka za Djibouti na mashirika ya kiutu na wahisani ili kumaliza mwenendo wa machungu wanayokumbana nayo wahamiaji.

Wakati huo huo, IOM imesema makumi ya maelfu ya wahamiaji kutoka pembe ya Afrika wamekwama Yemen na wanaishi katika mazingira magumu, wakiwa hawana maji, chakula, huduma za tib ana usalama.
Kwa wale ambao wanataka kurejea nyumbani, wanalazimika kuwalipa wasafirishaji haramu kiwango kikubwa cha fedha.

IOM inachofanya ni kuwapatia chakula, maji safi, huduma za matibabu na ushauri nasaha hususan wale waliopitia machungu wakati wa safari.

Tayari wahamiaji zaidi ya 6,000 nchini Yemen wamejisajili ili kurejea nyumbani kwa hiari na IOM inatoa wito kwa serikali kwenye ukanda huo kuchukua hatua zadi kufanikisha mpango huo wa kurejea nyumbani kwa hiari, VHR.

Ili kufanikisha, mwezi uliopita, IOM ilizindua ombi la dola milioni 98 ili kusaidia wahamiaji walioko Pembe ya Afrika na Yemen.