Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa kirafiki wakutanisha walinda amani kutoka Tanzania na baadhi ya viongozi mashariki mwa DRC

Kambi ya wakimbizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNOCHA
Kambi ya wakimbizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mkutano wa kirafiki wakutanisha walinda amani kutoka Tanzania na baadhi ya viongozi mashariki mwa DRC

Amani na Usalama

Kuelekea siku ya kimataifa ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na katika kuendeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,  vikosi vya ulinzi wa amani kutoka Tanzania yaani TANZBATT 9 na kikosi cha utayari TANZANIA QRF2 vimefanya kikao cha Urafiki baina yao na uongozi wa raia wa nchi hiyo katika maeneo ya uwajibikaji wa vikosi hivyo.

"Kikao hiki kina manufaa kwa sababu ndipo sehemu pekee ambapo unaweza ukapata kujua utendaji kazi wa kikundi chetu cha ulinzi wa amani. Kwa maana hawa ndio wawakilishi wawananchi ambao wanatuona tunavyopita kule, tunavtokeleza majukumu kule kwao.

Kwa hivyo wao wanawakilisha mawazo ya wananchi." Ni Kamanda wa kikosi cha TANZBATT 9 Luteni Kanali Barakaeli Mley akieleza manufaa ya kikao hiki na akaongeza akisema, "isingekuwa isingekuwa rahisi kuita watu wote hapa, lakini kupitia wao, ndio wanaweza wakatuambia kwamba tunakubalika, tunafanyaje majukumu yetu, wapi tunakosea, wapi tunapatia. Kwa hivyo kupitia kikao hiki tutapata mawazo yao mazuri na ushauri pia watatupa. 

Naye Kamanda kikosi cha utayari kutoka Tanzania (Tanzania Quick Reaction Force) Luteni Kanali Milao ameeleza kwamba, "machifu ndio wale watu ambao wako na zile jamii ambao ni waathirika. Kwa hiyo wao ndio wanatupatia habari mbalimbali ambazo zinatuwezesha sisi mwisho wa siku kwenda kutekeleza hayo majukumu yetu ya ulinzi wa amani.

Kwa sababu sisi inakuwa sio rahisi kuwafikia wale raia mmojammoja moja kwa moja, lakini kupitia hawa machifu wamekuwa msaada mkubwa kwetu, wameturahisishia. Kwa hivyo hata raia anapokuwa na shida binafsi hasa pindi hali ya usalama inapokuwa haiko sawa kwenye maeneo yao, wanaenda kuripoti kwa machifu, basi na sisi tunapata taarifa kupitia kwa hao machifu, mwisho wa siku tunachukua zile hatua sitahiki." 

Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa serikali ya raia katika maeneo ya uwajibikaji wa vikosi vya Tanzania wameeleza umuhimu wa kikao hicho na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto za kiusalama zilizopo. Josie Kapisa ni Chifu wa eneo la Nzuma akiwakilisha baadhi ya viongozi, anasema, "kwa haya mawasiliano, tumeongea vizuri na tumtoleana taarifa na tumeahidiana kwamba tutaendelea kuwasiliana vizuri na wao wako tayari kutusaidia kwa kazi ambayo tunafanya, na sisi tutawasidia ili wafike mwisho wa misheni yao mambo yakiwa sawa."

Wengine walioshiriki katika kikao hicho ni uongozi wa polisi (Police Nationale Congo) na uongozi wa jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) katika maeneo ya uwajibikaji ya vikosi hivyo.