Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DR Congo: Wanajeshi wa kulinda amani watumwa kulinda raia huko Ituri

Helkopta za MONUSCO zikizunguka Ituri DRC (Kutoka Maktaba)
MONUSCO/Nazar Voloshyn
Helkopta za MONUSCO zikizunguka Ituri DRC (Kutoka Maktaba)

DR Congo: Wanajeshi wa kulinda amani watumwa kulinda raia huko Ituri

Amani na Usalama

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakikabiliana na machafuko mapya dhidi ya raia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, wakishika doria na kuwasaidia viongozi wa eneo hilo kuwaachilia huru watu watano waliotekwa nyara na wanamgambo katika jimbo la Ituri.

Hayo ni kwa mujibu wa Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani jana Jumatano.

Dujarric amesema “Walinda amani wanaohudumua katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa  wa kulinda amani nchini DRC ujulikanao kama MONUSCO wamechukua hatua dhidi ya tahadhari na taarifa zilizopokelewa katika siku chache zilizopita na kupeleka askari kufanya doria karibu na eneo la Djugu ili kulinda raia.”

Askari hao wa kulinda amani pia wamewaunga mkono viongozi wa eneo hilo ambapo wamejadiliana kuhusu kuachiliwa kwa watu watano waliotekwa nyara na wanamgambo wa CODECO, ambao ni muungano huru wa makundi ya waasi wa kisiasa na kidini.

Walnda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.
MONUSCO/Force
Walnda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.

Kulishika mkono jeshi la serikali FARDC

Kwa mujibu wa Dujarric "MONUSCO pia imeingilia kati kujibu shambulio dhidi ya kituo cha jeshi la Congo FARDC, huko Tcha".

Ameongeza kuwa "Walinda amani hao pia wanaendelea kuwalinda raia ambao walisaka hifadhi karibu na kituo cha muda cha MONUSCO katika eneo la Drodo huko Ituri."

Mbali ya hayo amesema walinzi hao wa amani walikuwa wametumwa wiki iliyopita kutuliza mapigano kati ya CODECO na wanamgambo wa Zaire na sasa hali sasa inaripotiwa kuwa shwari.

MONUSCO inapaswa kuondoka kabisa DRC ifikapo mwisho wa mwaka 2024 lakini Umoja wa Mataifa umedhamiria kusalia na kutoa msaada kwa raia wa Congo wanaohitaji msaada kwa muda mrefu, baada ya kujiondoa kwa ujumbe huo.