Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa UN DR Congo aeleza Baraza la Usalama hali  inavyozidi kuwa tete

Bintou Keita (kwenye skrini), Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani DRC, akitoa maelezo kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali inayoihusu nchi hiyo.
UN Photo/Loey Felipe
Bintou Keita (kwenye skrini), Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani DRC, akitoa maelezo kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali inayoihusu nchi hiyo.

Mwakilishi wa UN DR Congo aeleza Baraza la Usalama hali  inavyozidi kuwa tete

Amani na Usalama

Mapigano kati ya M23 na wanajeshi wa Congo (FARDC) yameongezeka katika maeneo kadhaa na "M23 imepanua mipaka yake zaidi kusini, na kusababisha kuhama zaidi kwa watu kuelekea Goma na Kivu Kusini.” Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambaye pia ni Mkuu MONUSCO, Bintou Keita, amesema leo. 

Akihutubia Baraza la Usalama leo (20 Feb) kwa njia ya video, Keita pia amesema, "Tarehe 12 Februari, mashambulizi ya M23 yalisababisha vikosi vya jeshi la Congo, FARDC, kujiweka tena mashariki mwa mji wa Sake."

Keita ameongeza, "Hali katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu waliohama makazi yao ndani na karibu na Goma ni ya kupita kiasi. Zaidi ya watu 400,000 waliokimbia makazi yao sasa wametafuta hifadhi katika mji huo, wakiwemo watu 65,000 katika wiki mbili zilizopita, na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la wagonjwa wa kipindupindu kutokana na ukosefu wa maji safi ya kunywa, usafi wa kutosha, na usafi wa mazingira.”

Aidha ameeleza kwamba anasikitishwa sana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu za kimataifa na sheria za kimataifa unaofanywa katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa M23, ambapo vuguvugu hilo linalenga watendaji wa mashirika ya kiraia, hasa watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari. “Idadi ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na M23 inaendelea kuongezeka, huku takriban raia 150 wakiuawa tangu kuanza tena kwa mapigano Novemba 2023, wakiwemo 77 Januari 2024.”

Keita amesisitiza, "MONUSCO inaendelea kukabiliwa na wimbi la taarifa potofu na za uongo kuhusu jukumu lake katika mapigano yanayoendelea. Kampeni za mtandaoni zinazolenga MONUSCO zimekuwa zikifanywa na akaunti ambazo hasa ziko nje ya DRC. Hii imesababisha vitendo vya uhasama dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na vikwazo vya kutembea vinavyowekwa na makundi yenye silaha 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika Umoja wa Mataifa Zénon Mukongo Ngay akihutubia pia Baraza la Usalama amesema, "Masuala ya Congo, bila kujali asili yaKE, yatatatuliwa tu na watu wa Congo na ndani ya mipaka ya nchi bila kuingiliwa na nje.”