Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua madhubuti zahitajika kukomesha ajira ya watoto duniani: ILO 

Watoto wakifanya kazi katika migodi Ouagadougou, Burkina Faso.
© UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakifanya kazi katika migodi Ouagadougou, Burkina Faso.

Hatua madhubuti zahitajika kukomesha ajira ya watoto duniani: ILO 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kongamano la 5 la kimataifa kuhusu kutokomeza ajira ya watoto duniani  lililoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO, limefunguliwa leo mjini Durban nchini Afrika Kusini kwa wito wa kutaka kuchukuliwa hatua za haraka kukabiliana na ongezeko la idadi ya watoto wanaotumbukia katika ajira ya watoto 

Akizungumza katika ufunguzi wa wiki ya majadiliano ya mkutano huo unaofanyika  ana kwa ana na mtandaoni, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amewataka wajumbe kujitolea kuchukua "hatua mbali mbali kuleta mabadiliko katika maisha ya watoto, akielezea utumikishwaji wa watoto kama ajira ya watoto na ni adui wa makuzi ya watoto wetu na adui wa maendeleo.” 

Ameongeza kuwa "Hakuna ustaarabu, hakuna nchi na hakuna uchumi unaoweza kujiona kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ikiwa mafanikio na utajiri wake umejengwa juu ya migongo ya watoto”. 

Wito wake umeungwa mkono na mkurugenzi mkuu wa ILO Guy Ryder ambaye amesisitiza kwamba “Ajira ya Watoto ni ukiukwaji wa haki za msingi na lemnmgo letu lazima liwe kwamba kila mtoto kila mahali anakuwa huru dhidi ya ukiukwaji huo. Hatuwezi kupumzika hadi pale lengo hilo litakapotimia.” 

Bwana Ryder ameongeza kuwa “Wengine wanaweza kusema kwamba ajira ya Watoto ni athari ya umasikini ambayo haiepukiki na kwamba ni lazima tuikubali. Lakini hilo si sahihi, asilani hatuwezi kukumbatia ajira ya watoto.” 

Mvulana wa miaka 13 akifanya kazi katika duka la kukarabati gari Syria.
UNICEF/Alessio Romenzi
Mvulana wa miaka 13 akifanya kazi katika duka la kukarabati gari Syria.

Ukomo wa SDGs za kutokomeza ajira hiyo unakaribia 

Huku ukomo  wa lengo la maendeleo endelevu la kutokomeza ajira ya watoto ifikapo mwaka 2025 ukikaribia, wazungumzaji wengi kwenye mkutano huo wameeleza haja ya haraka ya kurejesha maendeleo ambayo yalikuwa yamefanywa katika kanda nyingi kabla ya janga la COVID-19

Takwimu za hivi karibuni za ILO zinaonesha kuwa watoto milioni 160 karibu mtoto 1 kati ya 10 ya watoto wote ulimwenguni bado wako katika ajira ya watoto.  

Na idadi inaongezeka, na janga hilo linatishia kurudisha nyuma miaka ya maendeleo yaliyopigwa.  

ILO inasema ajira ya watoto imeongezeka hasa katika kundi la umri wa miaka 5 hadi 11. 

Afrika inaongoza kwa ajira hizo 

Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano wa kimataifa wa kutokomeza ajira ya watoto kufanyika barani Afrika eneo ambalo kwa kuzingatia takwimu idadi ya watoto wanaotumikishwa iko juu zaidi na hatua za kuitokomeza yamekuwa ya polepole zaidi.  

Shirika hilo la ajira duniani linasema ajira nyingi za watoto katika bara la Afrika kwa asilimia 70 ni katika kilimo, mara nyingi katika mazingira ambayo watoto wanafanya kazi pamoja na familia zao. 

Mkutano huo utaendelea yaliyojiri katika mikutano minne ya awali ya kimataifa, iliyofanyika Buenos Aires (2017), Brasilia (2013), The Hague (2010), na Oslo (1997), ambayo iliibua ufahamu wa suala hilo, kutathmini maendeleo, kuhamasisha rasilimali, na kuanzisha mwelekeo wa kimkakati wa harakati za kimataifa dhidi ya ajira ya watoto. 

Mkutano huo unatarajiwa kuhitimisha kwa “wito wa Durban wa kuchukua hatua” ambao utaelezea ahadi madhubuti za kuongeza hatua za kukomesha ajira ya watoto.