Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana mkidhamiria mnaweza kukabiliana na chochote:Amina J. Mohammed

Amina Mohammed alipowasili Johannesburg, Afrika Kusini kuongea na vijana, hapa akipokelewa na Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Nardos Bekele-Thomas.
UN News/Rebecca Hearfield
Amina Mohammed alipowasili Johannesburg, Afrika Kusini kuongea na vijana, hapa akipokelewa na Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Nardos Bekele-Thomas.

Vijana mkidhamiria mnaweza kukabiliana na chochote:Amina J. Mohammed

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Vijana barani Afrika wameaswa kudhamiria kukabiliana na changamoto zinazowakabili na pia kuikabili duniani , kwani penye nia pana njia. Wito huo umetolewa leo na naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed katika mkutano wa maendeleo ya vijana barani Afrika unaofanyika mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Katika mkutano huo unaojadili uongozi wa vijana, ushiriki wao katika maendeleo na changamoto zinazowakabili vijana, Bi. Mohammed amesema duniani kote hivi sasa  kuna idadi kubwa kabisa ya vijana ambayo haijawahi kushuhudiwa n vijana bilioni 1.8 ni wa umri wa kati ya miaka 10 na 24 na Afrika ndio eneo changa kabisa ambalko wavulana na wasichana ni zaidi ya asilimia 60 ya watu wote. Lakini vijana hawa amesema wanakabiliwa changamoto kubwa na lukuki “Mara nyingi wako msitari wa mbele wa mwenendo uliopo ikiwemo changamoto za kimataifa katika baadhi ya nchi vijana wanakabiliwa na vita na ugaidi, kwingine athari za kiuchumi na kutengwa, ongezeko la kutokuwepo usawa, kukosa elimu bora, ujuzi na huduma za afya. Vijana pia wanashuhudia njia za ushiriki wao zikifungwa na haki zao kubinywa.Na kibaya zaidi vijana wanashuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu na pia kuona serikali na wengine wakishindwa kuchukua hatua kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kasi inayotakiwa.”

Amesisitiza kuwa tunahitaji kubadili mfumo wa uchimi wetu na kukumbatia mifumo mipya ya uzalishaji na matumizi. Amewatia moyo vijana hao akisema watu wanapokuwa na dhamira wanaweza kukabiliana na chochote akiwakumbusha kwamba ajenda  ya maendeleo endelevu SDGs na ajenda ya Muungano wa Afrika ya 2063 tayari zimewekewa mkakati wa kijamii na kiuchumi wa kuleta mabadiliko ambapo wote wakiungana na kudai mabadiliko kuanzia mashinani, hadi kimataifa na kushirikisha vijana malengo yatatimia kwani

Afrika tunayoitaka haitowezekana bila ushiriki wa kikamilifu wa vijana wa Afrika, hususan ambao wanakabiliwa na changamoto wakiwemo wanawake na wasichana. Kwani leo hii Umoja wa Mataifa umetambua kwamba matumaini yetu bora kwa ajili ya amani ya kimataifa na ustawi wa dunia hii yako mikononi mwa vijana. Tunahitaji uongozi wenu, ushiriki wenu na mchango wenu kote duniani.”

Mwisho amewaambia vijana hao kwamba “Ninawategemea kuwa chachu ya mabadiliko na wabeba mwenge ambao dunia inautaka mwanga wake kwa udi na uvumba , utu tunaoutaka kwa wavulana na wasichana unaanzia kwenu  na kwa kila mmoja wetu, itakuwa ni safari na mwisho wake utategemeana na jinsi gani mtakavyosafiri  katika barabara ya kuelekea 2030, ninaamini kwamba kwa uwezo wa vijana wa Afrika , Afrika tunayoitaka inawezekana.”

Mkutano huo umewaleta pamoja maelfu ya vijana kutoka barani afrika, wawakilishi wa serikali, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia.