Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto 1 kati ya 10 duniani watumikishwa katika ajira ya watoto:FAO/ILO

Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) linakadiria kuwa watoto milioni 168 duniani kote - mmoja kati ya kumi - wanashiriki katika ajira za utotoni
UN Photo/Martine Perret
Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) linakadiria kuwa watoto milioni 168 duniani kote - mmoja kati ya kumi - wanashiriki katika ajira za utotoni

Mtoto 1 kati ya 10 duniani watumikishwa katika ajira ya watoto:FAO/ILO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo hii kote duniani mtoto 1 kati ya 10 anatumikishwa katika ajira ya watoto na asilimia kubwa katika sekta ya kilimo ambao ni jumla ya watoto milioni 112 sawa na asilimia 70 ya watoto wote walio katika ajira, limesema leo kongamano la kimataifa lililoandaliwa kwa njia ya mtandao na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO kwa lengo la kusaka suluhu za kutokomeza ajira hiyo.

Video ya shirika la FAO imeonesha baadhi ya watoto wakielezea ndoto zao na matamanio yao wengine wakitaka kuwa waalimu, wanamuziki, marubani  na kadhalika, lakini sasa ndoto hizo zimeota mbawa baada ya kujikuta wamekwama katika ajira ya watoto.

Kwa mujibu wa FAO kongamano hilo la siku mbili lililoanza leo na kubeba kjina “kongamano la kimataifa la suluhu” lengo lake kubwa ni kuchagiza hatua kuchukuliwa ili kubaini na kupanua wigo wa suluhu za kutokomeza kabisa ajira ya watoto katika kilimo.

Kongamano hilo la mtandaoni limeandaliwa chini ya mwamvuli wa "mwaka wa kimataifa wa kutokomeza ajira ya watoto" na limewaleta pamoja wawakilishi kutoka wizara za kilimo, uvuvi, mifugo na mazingira, pia wazalishaji na wakulima,mashirika ya kimataifa, mashirika ya wafanyakazi, benki za maendeleo, makampuni ya biashara, asasi za kiraia, wanazuoni, watoto, wawakilishi wa vijana na watu walioonja shubiri ya ajira ya watoto.

FAO inasema kongamano hilo lina kaulimbiu tatu muhimu:-

Mosi kuhimiza chukua hatua, kwa lengo la kupaza sauti na kupata ahadi kutoka kwa wadau wa kilimo kuhusu kutokomeza ajira ya watoto katika sekta hiyo.
Pili kuhamasisha kwa kuchangia suluhu zitakazoleta mabadiliko na kubaini njia za kusongesha mchakato wa hatua za kuzuia na kutokomeza ajira za watoto katika sekta zote za kilimo.
Na tatu kufanya kazi kwa bidii kuujulisha mkutano wa kimataifa utakaofanyika mtandaoni 2022 kuhusu ajira za watoto na mikakati mingine ya kimataifa kama vile muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha familia kuhusu hatua zilizopigwa katika kutokomeza ajira za watoto.

Kongamano hili la kimataifa la kusaka suluhu dhidi ya ajira za watoto litafunga pazia kesho na FAO inashirikiana na wadau wengine wakubwa kulifanikisha likiwemo  shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO na ushirikiano wa kimataifa wa kupinga ajira ya watoto katika kilimo IPCCLA.