Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati umefika kutendea haki nchi zenye maendeleo duni- UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa viongozi wa nchi zenye kipato duni zaidi, LDCs mjini Doha, Qatar tarehe 4 Machi 2023
UN /Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa viongozi wa nchi zenye kipato duni zaidi, LDCs mjini Doha, Qatar tarehe 4 Machi 2023

Wakati umefika kutendea haki nchi zenye maendeleo duni- UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkutano wa 5 wa nchi zenye maendeleo duni zaidi duniani, LDCs ukianza kesho huko Doha  nchini Qatar, hii leo katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa António Guterres amesihi jamii ya kimataifa hasa nchi Tajiri ziongeze juhudi za kusaidia zaidi ya watu bilioni 1.1 walioko kwenye nchi hizo ili waondoke katika mzunguko wa lindi la umaskini.

Guterres ambaye tayari yuko Doha, kushiriki mkutano huo amesema hayo wakati wa mkutano uliofanyika leo ukijumuisha baadhi ya viongozi wakuu wa serikali kutoka LDCs.

“Nchi zenye uhitaji mdogo zitoe msaada zaidi. Na mnahitaji hivi sasa. Mnawakilisha mtu mmoja katika watu wanane duniani. Lakini nchi zenu zimesana kwenye mzunguko wa umaskini ambao unakwamisha maendeleo,” amesema Guterres.

Mkutano huu wa 5 wa LDCs unaanza tarehe 5 hadi 9 mjini Doha, na huwa unafanyika kila baada ya miaka 10 lakini umeahirishwa mara mbili tangu mwaka 2021 kutokana na janga la coronavirus">COVID-19.

Wakiwa Doha, viongozi wa serikali na wadau wengine watatathmini utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Istanbul, uliopitishwa katika kikao tangulizi cha LDC5 kwenye mji huo mkuu wa kibiashara wa Uturuki, Istanbul mwaka 2011.

Halikadhalika watahamaisha usaidizi na hatua za kimataifa kusaidia nchi 46 zenye maendeleo duni zaidi duniani.

Adhabu badala ya tuzo

Katika hotuba ya ukaribisho kwenye mkutano huo wa leo, Katibu Mkuu amesisitiza kuwa gharama ya Maisha inazidi kuwa ngumu kutokana na vita nchini Ukraine, inayochochea ongezeko la bei za nishati na chakula. Hali hii ikichanganyika na athari hasi za vita, mizozo, ukame, njaa na umaskini wa kupindukia inaweka mazingira yanayochochea umaskini na ukosefu wa haki.

Kupanda kutoka LDCs kwenda MICs kunageuka adhabu badala ya tuzo, António Guterres, Katibu Mkuu UN

Katika Mkuu amesema kumaliza ‘kimbunga’ hicho cha matatizo unahitajika uwekezaji mkubwa “na mfumo wa fedha duniani umeundwa kunufaisha nchi Tajiri kwa kiasi kikubwa. Bila msamaha fanisi wa madeni, LDCs zinalazimika kutumia kiasi kikubwa cha mapato kulipa madeni. Na nchi ambazo zimefanikiwa kuingia katika hadhi ya nchi za kipato cha kati, MICs, zitapoteza maslahi mahsusi ya kuwa LDCs kitu ambacho sasa kitageuka kuwa adhabu na si tuzo.”

Wakati wa haki

Halikadhalika Guterres amesema “hatuwezi kuruhusu nchi zirudi nyuma kimaendeleo baada ya kusonga mbele. Katikati ya ukosefu huu wa haki, Umoj awa Mataifa unafanya kazi nanyi ili kuandaa mikakati bora ya kipindi cha mpito, kwa kuzingatia mchakato unaofaa wa kutoka LDC kuelekea nchi ya kipato cha kati, MICs.

Ili kufanikisha Programu ya Utekelezaji ya Doha, (DPoA), mpango wa kipekee uliopitishwa mwezi Machi mwaka 2022 unaolenga Pamoja na mambo mengine kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs katika LDCs, umejumuisha Vyuo Vikuu vya mtandaoni, mfumo wa hifadhi ya chakula na kituo cha kimataifa cha kusaidia uwekezaji.

Pamoja na kile kinachoitwa mfumo wa kuchochea SDGs, uliozinduliwa mwezi Februari, DPoA pia inapendekeza kuongezwa kwa ufadhili kwenye maendeleo endelevu, kupatia majawabu gharama kubwa ya madeni na kuongeza ufadhili wa dharura.

Katibu Mkuu amesema pia kuna umuhimu wa njia mpya na makini za kupima uchumi wan chi kama vile kuandaa vigezo vya ukopeshaji unaongalia zaidi ya panto la ndani la taifa.

Akigusia mkutano unaoanza kesho, Katibu Mkuu amesema “lazima uwe wakati wa haki na usawa,” kwa LDCs na kusisitiza kuwa hebu na tufanye kazi Pamoja ili kupata njia mpya za kusaidia watu wenu. Hebu na tufanye kipengele cha LDC kiwe cha historia.

Rais wa Malawi Lazarus McCarthy Chakwera ambaye ndiye Mwenyekiti wa kundi la nchi zenye kipato duni zaidi duniani, LDCs akifungua mkutano wa viongozi wa nchi hizo huko Doha, Qatar, 4 Machi 2023
UN /Evan Schneider
Rais wa Malawi Lazarus McCarthy Chakwera ambaye ndiye Mwenyekiti wa kundi la nchi zenye kipato duni zaidi duniani, LDCs akifungua mkutano wa viongozi wa nchi hizo huko Doha, Qatar, 4 Machi 2023

LDC5 lazima iwe vitendo na si maneno matupu

Mkutano huo wa viongozi wa LDC ulifunguliwa na Rais wa Malawi Lazarus McCarthy Chakwera, ambaye ndiye mwenyekiti wa kundi la LDC.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Malawi ni moja ya nchi maskini zaidi duniani ikiwa na pato la ndani la taifa la dola 639 mwaka 2021.

Kama ilivyo kwa nchi nyingi za LDCs, umaskini, utapiamlo umesambaa katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, ambako nusu ya wananchi wakiishi chini ya kiwango cha umaskini.

Malawi pia inakabiliwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, huku mafuriko na ukame vikisababisha uharibifu zaidi wa mazao na mbinu za kujipatia kipato.

Katika hotuba yake, Rais Chikwera akasisitiza “changamoto hiyo ya kipekee duniani na vikwazo vya kimataifa vinavyokumba LDCs haziwezi kutatuliwa na yeyote kati yetu hapa peke yake, na kwamba mataifa mengi yametelekeza ushirikiano wa kimataifa na kuanza kufanya kazi kitaifa zaidi na kutupilia mbali udugu na ubinadamu, lakini lazima tuepuke kishawishi hicho.”

“Hatuko hapa kuzungumza tu,” amesema Rais Chikwera, “tuna kazi maalum ya kufanya na matokeo ya kuonekana. Kwa Pamoja tutakuwa na Chuo Kikuu cha mtandaoni; mfumo wa kusongesha uwekezaji; mfumo wa kuhifadhi chakula; mfumo wa kuhimili na kujengea mnepo majanga;  mfumo wa kusaidia mpito wa kutoka LDCs kuwa MICs.”

Rais Chakwera amesihi wadau wote wa maendeleo “tekelezeni wajibu wenu ili mtuondolee vikwazo vinavyotukabili.”

Hamza Abdiwahab, mshiirki kijana kwenye LDC5 akitokea Somalia akizungumza na Habari za UN

Yatakayojiri wiki nzima

Wakati wa mkutano huo, makumi ya viongozi wa LDCs walibadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kutatua kwa Pamoja changamoto zinazokabili nchi zao na kupata majawabu yenye maana.

Halikadhalika walitoa mwongozo dhahiri wa jinsi ya kuhakikisha  utekelezaji wa malengo, ahadi na matokeo ya DPoA kwa LDCs kwa mungo wa 2022-2031 pamoja na Azimio la kisiasa la Doha.

Katika siku chache zijazo, viongozi kutoka kona mbalimbali za dunia watakutana na sekta binafsi, wabunge na vijana kusongesha mawazo mapya, kuchochea ahadi mpya za usaidizi na kuhimiza utekelezaji wa ahadi zilizokubaliwa chini ya DPoA.

Mkutano unatarajiwa kutangaza mipango na matokeo mahsusi ambayo yanapatia majawabu changamoto zinazokumba LDCs na kusaidia kufanikisha DPoA.

Ushiriki wa ngazi ya juu utakuwa muhimu kwa mkutano huo wa 5 wa LDCs ili kujenga kasi ya kuchochea upya ubia wa wadau mbali mbali ili kufanikisha malengo ya juu zaidi ya DPoA.

Ushiriki wa vijana

Kuna majukwaa matatu mahsusi kwa ajili ya vijana, sekta binafsi na wabunge ambayo yamefanyika leo jumamosi, kando ya mkutano wa viongozi.

Mchana, makumi ya vijana wakiwakilisha vijana milioni 226 kutoka LDCs walishiriki kwenye jukwaa la vijana, la kwanza kabisa kuwahi kufanywa na LDCs.

Jukwaa hilo limetoa fusa pekee ya vijana kubadilishana mawazo, majawabu na hatua za kuleta matokeo.

Hamza Abdiwahab, kijana kutoka Somalia ameiambia Habari za UN  kwamba ukosefu wa utulivu ndio changamoto kuu inayokumba LDCs kwenye ukanda wa taifa lake huko Pembe ya Afrika, hali ambayo amesema inaathiri masuala mengi yanayohusu ubora wa elimu na umaskini.

Na bila shaka, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchi 24 kati ya nchi zote 46 zenye kipato duni zaidi duniani zilikuwa na mapigano mwaka 2019. Nchi 3 kati ya 4 kwenye kundi hilo la LDCs ziko kwenye mapigano au mazingira baada ya mapigano.

“Naamini kuwa sisi vijana tunapaswa kushiriki katika utoaji wa maamuzi ili tuweze angalau kuwa na utulivu wa kisiasa wa kuweza kufanikisha SDGs katika miaka7 ijayo,” amesema Hamza.

Armel Azihar Slyvania, mshiriki kijana kutoka Comoro akizungumza na Habari za UN mjini Doha, Qatar kunakofanyika mkutano wa LDCs.

Armel Azihar Slyvania, kijana kutoka Comoro amekazi hoja ya Hamza alipozungumza na Habari za UN.

“Iwapo serikali zetu zina utashi wa kusikiliza vijana na kuchukua majawabu yetu tunaweza kuleta suluhu kwenye nchi zetu na hii itasaidia sana kutatua matatizo yanayotukabili,” amesema Armel.

Washiriki hao vijana wa LDC walijadili masuala ya maendeleo ambayo yanaathiri wao na nchi zao, kama vile elimu, uendelezaj iwa stadi, afya, ajira, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama, haki za binadamu na uhamiaji.

Jukwaa la vijana limepitisha Azimio likipatiwa jina Kwa Vizazi Vyote  ambalo linaelezea ahadi ya vijana katika kuchangia mustakabali bora kwa nchi zilizo duni zaidi duniani na kwingineko.

Azimio hilo la vijana ambalo ni matokeo ya msururu wa mashauriano na vijana kutoka nchi 46 maskini zaidi duniani litatumiwa kama nyaraka ya uchechemuzi na ushawishi kwa mashauriano ya DPoA na litawasilishwa kwa viongozi wa dunia kwenye mkutano wa LDC5 unaofunguliwa kesho Jumapili Machi 5.

Vijana walioshiriki jukwaa la vijana kabla ya kuanza kwa mkutano wa 5 wa LDCs Doha, Qatar 5 Machi 2023
UN News/Anold Kayanda
Vijana walioshiriki jukwaa la vijana kabla ya kuanza kwa mkutano wa 5 wa LDCs Doha, Qatar 5 Machi 2023

Mashirika ya kiraia na UN yafanye kazi pamoja

Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , Csaba Kőrösi ambaye naye tayari yuko Doha,  alihutubia Jukwaa la Mashirika ya Kiraia na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mashirika ya kiraia na Umoja wa Mataifa, akisema ushirikiano huo ni muhimu.

“Serikali hazina hakimili ya busara na hivyo tunahitaji busara zenu. Tunahitaji  ufahamu wenu. Tunahitaji uzoefu wenu,” amesema Kőrösi  akiongeza kuwa “hebu na tuahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kusaidia marekebisho ya LDCs na kufanikisha maendeleo endelevu.”

Bwana Kőrösi ametaja changamoto lukuki zinazokabili nchi zenye maendeloe dunia akisema “ziko njia panda kuelekea malengo ya maendeleo endelevu,” kwa sababu kwa bahati mbaya janga la Corona limefuta ukuaji wa uchumi uliofanikiwa miaka ya nyumba ambao ulikuwa muhimu katika kufanikisha na kuboresha huduma za afya  na nyinginezo na kupunguza umaskini, ambapo hivi sasa baadhi ya LDCs zinakabiliwa na kudumaa kwa uchumi kuwahi kufikiwa katika miongo mitatu iliyopita.

“Mbaya zaidi kati yam waka 2011 na 2019, deni la pamoja la LDCs liliongezeka mara tatu kutoka dola bilioni 10 hadi dola bilioni 33 kwa mwaka. Deni hili linakadiriwa kuongezeka kwa dola nyingine bilioni 50 kutokana na athari hasi za janga,” amesema Rais huyo wa Baraza Kuu akiongeza kuwa kufafanua jambo hilo kibinadamu inamaanisha watu wengine milioni 32 watatumbukia kwenye lindi la umaskini katika nchi hizo za LDCs, huku wanawake na watoto wakibeba mzigo mkubwa zaidi wa kukumbwa na machungu.

Kwa kutambua hilo, Bwana Kőrösi amesema “lakini tunaweza kuchagua kuwekeza kwenye maendeleo endelevu. Hilo ni chaguo bora na chaguo la kimaadili. Hii sio ukarimu bali hii ni kufanya kitu sahihi.”

Ni kwa mantiki hiyo amesema kufanikisha hilo “lazima tufanya kazi kwa pamoja. Maeneo yote, sekta zote,” akitaja DPoA kama mpango wa kina uliobuniwa kutatua changamoto zinazokabili LDCs.

Nchi 46 zenye maendeleo duni zaidi duniani

Hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2023 nchi zifuatazo ziko kwenye kundi la LDCs.

AFRIKA (33): Angola, Benin, Burkina Faso, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Guinea, Guinea-Bissau, Lesotho, Liberia, Madagascar, Malawi, Mali, Mauritania, Msumbiji, Niger, Rwanda, São Tomé na Príncipe, Senegal, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Togo, Uganda, na Zambia 

ASIA (9): Afghanistan, Bangladesh, Bhutan, Cambodia, Jahmhuri ya kidemokrasia ya watu wa Lao, Myanmar, Nepal, Timor-Leste na Yemen 

Karibea: (1) Haiti

Pasifiki: (3): Kiribati, Visiwa vya Solomon na Tuvalu 

Kufahamu zaidi kuhusu LDCs bofya hapa