Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha juhudi za Afrika Mashariki kuhimiza amani 

Walinda amani wa MONUSCO kutoka Tanzania wakiwa na wanawake wenyeji wa DRC.
© MONUSCO
Walinda amani wa MONUSCO kutoka Tanzania wakiwa na wanawake wenyeji wa DRC.

UN yakaribisha juhudi za Afrika Mashariki kuhimiza amani 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha juhudi za Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, na viongozi wengine wa Afrika Mashariki kuhimiza amani, utulivu na maendeleo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.  

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini New York Marekani Antonio Guterres amewapongeza viongozi wa ukanda huo kwa uthubutu wao katika kufanyia kazi malengo hayo. 

Katibu Mkuu amesema anatambua juhudi za pande mbili zilizoamuliwa na kongamano la wakuu wa nchi wa ukanda huo, ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi cha kikanda na kufufua mchakato shirikishi wa kisiasa.  

Amesisitiza haja ya uratibu mzuri kati ya jeshi la kikanda na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO, ambao ni muhimu ili kuhakikisha ulinzi wa raia.  

Pia amehimiza makundi yote ya wenyeji yenye silaha nchini DRC kushiriki bila masharti katika mchakato wa kisiasa, na makundi yote ya kigeni yenye silaha kunyang'anywa silaha na kurejea mara moja na bila masharti katika nchi zao za asili. 

Katibu Mkuu anasisitiza umuhimu wa mkakati wa kina wa kushughulikia vyanzo vya mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiwa ni pamoja na hatua zisizo za kijeshi, na utekelezaji mzuri wa utaratibu wa haki ya mpito na mipango ya upokonyaji silaha na kuwajumuisha wapiganaji katika maisha ya kawaida, DDR/R. 

Guterres anatoa wito wa kuendelea kwa mazungumzo ya kina na ya wazi kati ya wadau wote kwa nia ya kutatua mivutano na kuimarisha imani na kuaminiana. Anasisitiza tena kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono nchi za eneo hilo katika juhudi za muda mrefu za kujenga amani zinazolenga kufikia uwajibikaji na kuunganisha mafanikio ya amani na usalama.