Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la kibinadamu Ukraine lashamiri; Watu milioni 6 wanahitaji msaada haraka:WFP/FAO 

Mama aliyekimbia Bucha na familia yake akiwa na mwanae katika kambi ya Zakarpattia, Ukraine.
© IOM/Jana Wyzinska
Mama aliyekimbia Bucha na familia yake akiwa na mwanae katika kambi ya Zakarpattia, Ukraine.

Janga la kibinadamu Ukraine lashamiri; Watu milioni 6 wanahitaji msaada haraka:WFP/FAO 

Msaada wa Kibinadamu

Hali ya kibinadamu nchini Ukraine inaendelea kuwa mbaya zaidi huku mamilioni ya watu waliotawanywa na vita hivyo ndani na nje ya nchi sasa wanategemea msaada wa kibinadamu kuweza kuishi,  yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa wakati huu yakihaha kuwasaidia watu hao kwa kila njia. 

Ttaarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi na Mratibu wa Masuala ya dharura wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP  nchini Ukraine Jakob Kern ambaye alikuwa katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na mji wa Bucha wiki iliyopita, inaeleza kuwa alishuhudia madhila ya hali ya juu. 

“Nimeona jamii ambayo inajaribu kujikwamua kwa kila hali. Watu wengine wamepoteza kila kitu, kuanzia riziki hadi wanafamilia wao. Watahitaji kila aina ya msaada ili warejee katika maisha ya kawaida. Lakini pia tumeshuhudia jitihada kubwa za serikali na jamii za mitaa za kujenga upya miji yao, kusafisha vifusi, kuweka huduma za msingi na kujiandaa kurejea kwa familia zilizolazimika kukimbia makazi yao.” 

Wafanyakazi wa misaada wanatayarisha usaidizi unaohitajika sana kutoka kwa msafara wa mashirika ya kibinadamu unaoongozwa na Umoja wa Mataifa uliofika Sumy, Ukraine.
© UNOCHA/Laurent Dufour
Wafanyakazi wa misaada wanatayarisha usaidizi unaohitajika sana kutoka kwa msafara wa mashirika ya kibinadamu unaoongozwa na Umoja wa Mataifa uliofika Sumy, Ukraine.

Jitihada za misaada 

Ameongeza kuwa WFP inaongeza hatua zake za kufikisha msaada wa kibinadamu kwa mamilioni ya watu walioathirika na mzozo huo wa Ukraine kwa msingi wa kutojuta.  

“Tunakadiria kwamba takriban watu milioni 6 wameathirika na janga la kibinadamu linalokua kwa kasi zaidi duniani nchini Ukraine na watahitaji msaada wa chakula na pesa taslimu. Tunasaidia na kuunga mkono juhudi kubwa za serikali ya Ukraine za kutoa msaada kwa familia zilizo hatarini Zaidi hasa wanawake, watoto na wazee. Tunaongeza msaada wa chakula katika maeneo ambayo hapo awali hayakuweza kufikiwa kama vile Bucha, Irpin, Hostomel na Borodianka.” 

Hadi sasa WFP imekusanya zaidi ya tani 60,000 za chakula kwa ajili ya msaada wake kwa Ukraine, chakula ambacho kinatosha kulisha watu milioni 2 kwa miezi miwili. Zaidi ya theluthi moja  au asilimia 38 ya chakula hicho kimenunuliwa  ndani ya Ukraine. 

WFP wiki saba baada ya kuzuka kwa vita hiovyo imefanikiwa kuwafikia watu milioni 1.7 ndani ya Ukraine kwa msaada wa chakula , na pia imetoa msaada wa fedha taslim dola milioni 3.6 kwenye maeneo ambako masoko bado yamegfunguliwa. 

Kutokuwa na uhakika wa chakula Ukraine 

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO linasema hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula nchini Ukraine inaongezeka na kutia wasiwasi mkubwa.  

Kwa mantiki hiyo sasa shirika hilo linahitaji haraka dola milioni 115.4 ili kuzuia hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula kuwa mbaya zaidi na kuzorotesha Zaidi mnyororo wa usambazaji wa chakula nchini humo. 

“Kuna udharura wa kuwasaidia wakulima wa Ukraine katika kupanda mboga na viazi katika msimu huu wa masika, na wakulima wanapaswa kuruhusiwa na kuungwa mkono kwenda mashambani mwao na kuokoa mavuno ya ngano ya majira ya baridi. Kwa Mpango huu, kulingana na ombi la mashirika mbalimbali FAO imeongeza zaidi ya mara mbili ombi lake la awali la dola milioni 50 ili kaya 376, 660 za wakulima wadogo na wa kati au karibu watu milioni moja hadi mwezi Desemba 2022.” 

Athari za vita kwa dunia nzima 

FAO inakadiria kwamba asilimia 20 ya maeneo yaliyopandwa hayatavunwa mwezi Julai, wakati wachambuzi wa soko la nafaka wanakadiria kuwa eneo la upanzi wa masika litakuwa dogo kwa karibu theluthi moja kuliko kawaida. 

Ukraine ilikuwa ikiuza nje karibu nafaka na mbegu zake zote za mafuta kulingana na wizara ya kilimo yan chi hiyo, hadi tani milioni 6 kwa mwezi  kupitia bandari ambazo sasa zimefungwa.  

Takriban tani milioni 15 za nafaka hazitakuwa na nafasi ya kuhifadhiwa katika maghala kote nchini.  

Na FAO inasema ikiwa Ukraine haiwezi kuuza nje akiba yake ya sasa, wakulima wanaweza wasiweze kuvuna kwa gharama ya chini, achilia mbali kupanda mazao ya mwaka ujao.  

Na bila shaka, ukosefu wa nafaka za Ukraine kwenye soko la dunia kunasathiri bei ya vyakula kote duniani. 

WFP pekee inatumia dola za Marekani milioni 70 zaidi kwa mwezi kununua kiasi sawa cha chakula kama ilichonunua mwaka jana ambacho kingewezesha kulisha wanawake, watoto na wanaume milioni 4 kwa mwezi.