Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atuma salamu za pole Afrika Kusini kufuatia athari za mafuriko 

Mji wa Johannesburg Aprili 3, 2020 nchini Afrika Kusini.
IMF Photo/James Oatway
Mji wa Johannesburg Aprili 3, 2020 nchini Afrika Kusini.

Guterres atuma salamu za pole Afrika Kusini kufuatia athari za mafuriko 

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza masikitiko yake kufuatia vifo na uharibifu wa mali kutokana na mafuriko nchini Afrika ya Kusini. 

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric imemnukuu Katibu Mkuu akituma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa pamoja na serikali na wananchi wa Afrika ya Kusini kutokana na mafuriko hayo katika jimbo la Kwazulu-Natal. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300 huku mvua kubwa zaidi ikitabiriwa katika miji ya Durban katika siku chache zijazo. 

Halikadhalika vyombo hivyo vya habari vimesema kuwa idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kwa kuwa hadi leo Alhamisi, watu wengi hawajulikani waliko, na kwingineko ni familia nzima. 

Picha zinazosambazwa zimeonesha uharibifu wa majengo, majumba pamoja na miundombinu ikiwa imesombwa kwa maji. 

Bwana Guterres kupitia taarifa hiyo ameelezea mshikamano wa Umoja wa Mataifa na serikali ya Afrika Kusini huku akisema Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa msaada utakaohitajika.