Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, usalama na amani ni muhimu katika kufikia maendeleo Afrika-AU, UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (Kulia) na mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat wakihutubia waandishi wa habari.
Video Screen Shot
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (Kulia) na mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat wakihutubia waandishi wa habari.

Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, usalama na amani ni muhimu katika kufikia maendeleo Afrika-AU, UN

Amani na Usalama

Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya masuala ambayo yataathiri ukuaji wa uchumi wa bara Afrika iwapo uchafuzi wa mazingira hautapunguzwa kwa asilimia 45 kufikia mwaka 2030 na kutokomezwa kabisa ifikapo mwaka 2050 amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia waandishi wa habari Jumatatu alasiri jijini New York, Marekani.

Bwana  Guterres amesema hayo baada ya mkutano wa faragha na  mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat ambapo amesema, “tuna miradi inayoshabiana, ajenda ya mwaka 2063 ya maendeleo ya Afrika  na ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu kote ulimwenguni, lakini ajenda hizo mbili ambazo zinalenga utandawazi sawa na maendeleo endelevu na jumuishi haziwezi kutekelezwa bila uwekezaji na moja ya changamoto ambazo tutakabiliana nazo katika miezi michache ijayo ni kuhakikisha kwamba kuna juhudi kwa ajili ya ufadhili wa sio tu maendeleo bara la Afrika lakini hususan kwa ajili ya maendeleo barani Afrika.”

Aidha Katibu Mkuu amesema sio tu kwa sababu ya kuonesha mshikamano na jamii ya kimataifa lakini pia, “maendeleo Afrika ni muhimu kwa ajili ya usawa na amani duniani, ili kuwezesha suala la uhamiaji kuweza kushughulikiwa vilivyo kwa hio ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kuimrsha ufadhili kwa ajili ya maendeleo katika nchi barani Afrika.”

Kwa upande wake Bwana Mahamat amesema, “tumemaliza mkutano wetu wa tatu kati ya AU na UN na tukiangazia masuala ya amani, usalama, maendeleo na suala muhimu la mabadiliko ya tabianchi.

Leo tena tumepitia azimio la kutumia vyema ubia wetu kwa ajili ya masuala yenye maslahi kwa mashirika yetu mawili. Tunasubiri kwa hamu kubwa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu tabianchi, na mnafahamu kuwa Afrika ni moja ya mabara ambayo yameathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi licha ya kwamba haijachangia kabisa kwenye mabadiliko ya tabianchi. Mathalani ukame na kuenea kwa jangwa.”

Suala la Libya

Uharibifu Tripoli, Libya.
OCHA/Giles Clarke
Uharibifu Tripoli, Libya.

Kuhusu Libya Katibu Mkuu akijibu swali kutoka kwa mwandishi habari juu ya ujumbe wake wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani  na hususan kwa Jenerali Khalifa Haftar, Kamanda wa jeshi la kitaifa la Libya amesema, “sina ujumbe mahsusi kwa mtu binafsi, ujumbe wangu ni kwa walibya wote kwa sasa, kulingana na msimamo wa amani na usalama wa Baraza la Usalama la Muungano wa Afrika, tunatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa sasa, kwa bahati nzuri kuna sitisho kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani  lakini tunachohitaji ni kusitishwa kwa mapigano na ushawishi wa nje kuruhusu walibya kwa mara nyingine kuweza kuja pamoja na kuweza kujadili kwa pamoja suluhu.”

Ameongeza kuwa, “tulikuwa na malengo ya pamoja ambayo yalijumuisha kongamano la kitaifa nchini Libya na kongamano la maridhiano ambalo lingefanyika Addis Ababa, nchini Ethiopia tuna matumaini kwamba juhudi zitarejeshwa kuwezesha hili kufanyika ili kuweza kusonga mbele katika siku za usoni lakini kwa sasa kipaumbele ni kusitishwa kwa mapigano nchini Libya.”

Naye mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika kuhusu Libya amesema, “Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika lilipitisha uamuzi wa kutaka sitisho la mapigano. Pia kuna hatua tumechukua, tulikuwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mimi mwenyewe tulikuwepo Libya mwezi mmoja uliopita. Bahati mbaya mkutano wa maridhiano wa kimataifa haukufanyika. Hata hivyo kipaumbele hivi sasa ni mapigano yakome. Na tunachoamini hii leo ni kwamba hakuna suluhu kupitia mapigano katika mzozo wa aina, ni lazima pande kinzani zikubali kusitisha mapigano na zisake njia za amani za kumaliza mzozo.”