Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano: Fidia kwa utumwa, 'muhimu' - Nikole Hannah-Jones wa The 1619 Project.

Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)
UN Photo/Mark Garten
Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)

Mahojiano: Fidia kwa utumwa, 'muhimu' - Nikole Hannah-Jones wa The 1619 Project.

Haki za binadamu

Mwandishi wa New York Times Nikole Hannah-Jones, anayejulikana zaidi kwa kitabu chake cha ‘The 1919 Project’ au ‘Mradi wa mwaka 1619’, ambacho kinaweka utumwa kama moja ya vipengele vya msingi vya historia ya Marekani, Jumanne wiki hii amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya biashara ya utumwa. Na baadaye akapata wasaa wa kukaa kitako na UN News kueleza kuhusu alivyofikia kuandika kitabu hicho.  

The 1619 Project ni kitabu ambacho kinaadhimisha miaka 400 ya meli ya kwanza ambayo ilileta waafrika wa mwanzo kabisa katika lililokuwa koloni la Muingereza, ambalo hivi sasa ni jimbo la Virginia nchini Marekani. Huo ndio unatazamwa kama mwanzo halisi wa utumwa wa Amerika katika makoloni 13 ya mwanzo ambayo ndiyo yalibadilika baadaye na kuunda nchi ya Marekani.  

Na kile ambacho kitabu hiki kinajaribu kufanya, kupitia mfululizo wa insha, ni kuuingiza utumwa kama  taasisi ya msingi ya Mrekani na mchango wa Wamarekani weusi katika kitovu cha historia ya Marekani.  

Lakini zaidi ya hayo, pia kuonesha jinsi urithi wa miaka 250 ya utumwa nchini Marekani bado unaunda sehemu kubwa ya jamii yetu leo. Sio tu kuhusu siku za nyuma, lakini ni kuhusu kile ambacho kimetokea hivi sasa. 

Lakini utumwa ni jambo nyeti. Huwezi kuelewa vizuri, huwezi kuelewa ulimwengu wa Atlantiki, huwezi kuelewa nini kilichotokea katika bara la Afrika, na kwa hakika huwezi kuelewa utajiri mkubwa wa wakoloni ikiwa hauelewi utumwa na mambo yake au urithi wake.  

Nikole Hannah-Jones, ripota wa New York Times aliyeshinda Tuzo ya Pulitzer muundaji wa Mradi wa 1619, akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Waathiriwa wa Utumwa katika Atlantiki
UN Photo/Manuel Elías
Nikole Hannah-Jones, ripota wa New York Times aliyeshinda Tuzo ya Pulitzer muundaji wa Mradi wa 1619, akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Waathiriwa wa Utumwa katika Atlantiki

UN News: Unawaambia nini wale wanaosema “sikushiriki utumwa, kwa nini bado unaniambia kuhusu utumwa”? 

Nikole Hannah-Jones: Jambo la kwanza ambalo ningesema ni kwamba haina mantiki kuamini kwamba mfumo uliodumu kwa miaka 400, ambao ulitengeneza upya sura ya dunia, uliotajirisha wakoloni wa Ulaya, ambao uliweka msingi wa ustawi wa kiuchumi wa Marekani, kwamba kwa namna fulani haufanyi kazi tena katika jamii tunamoishi. 

Kwa mfano, nchini Marekani, tumekuwa na utumwa kwa muda mrefu zaidi kuliko tulivyokuwa na uhuru, na watu wa asili ya Kiafrika wanabakia kuwa katikati ya viashiria vyote vya ustawi na jumuiya zote za zamani za watumwa. 

Ikiwa watu watasoma kitabu changu, wataona kwamba kila insha moja haihusu jambo lililotokea muda mrefu uliopita. Ni kuhusu jinsi yale yaliyotokea muda mrefu uliopita bado yanaunda na kufisidi sehemu kubwa ya jamii leo. 

Hakuna hata mmoja wetu aliyekuwa hai wakati Katiba inaandikwa. Na bado tunaelewa kuwa huo ni urithi wetu. Huwezi kudai tu sehemu za historia yako ambazo unafikiri zinakufanya uonekane mzuri au ambazo unafikiri ni za kuinua. 

Habari za UN: Je, ulishangazwa na kurejea nyuma au kudorora katika baadhi ya mambo ya kisiasa? 

Nikole Hannah-Jones: Sishangai. 

Marekani hasa imekuwa katika hali ya kutokubali kuhusu utumwa na urithi wake. Sisi ni taifa lililojengwa juu ya maadili ya uhuru kutoka kwa Mungu. Tunaamini sisi ni taifa huru na la kipekee zaidi duniani. Na utumwa na urithi wake vinasema uongo kwa haki hiyo. 

Utumwa ni unafiki ulio wazi katika taifa linalotaka kuamini kuwa ndilo kilele cha uhuru wa dunia. 

Lakini nitakuwa nasema uongo ikiwa sitasema jinsi kitabu hicho kimefanywa kuwa silaha na siasa. Miaka mitatu baada ya uchapishaji wake wa mwanzo, imekuwa ya kushangaza sana.   

Na kinachokuambia ni kwamba historia kwa njia nyingi inahusu mamlaka au nguvu. Ni kuhusu nani anapata kuunda uelewa wetu wa pamoja, nani anapata kuunda kumbukumbu yetu ya pamoja. Na nguvu hiyo haitaki tuelewe historia inayoondoa mamlaka hayo. 

Na ndivyo kitabu cha The 1619 Project kinavyofanya. kinawachukua watu ambao wamechukuliwa kama watu wa pembezoni, kinachukua uhalifu wa kimataifa dhidi ya ubinadamu ambao ulikuwa utumwa na kinasema kwamba ulikuwa muhimu kwa Marekani na kwa ulimwengu wa Atlantiki kama maadili haya ya uhuru. Na hilo ni jambo ambalo linatisha sana kwa watu fulani wenye nguvu. 

UN News: Je, unajibu nini kwa wale wanaosema kwamba unafunua kidonda, badala ya kuponya? 

Nikole Hannah-Jones: Kweli, ni wazi, jeraha bado linauma. Ikiwa tunataka kuondoa bandeji na kujua ni kwa nini jeraha linauma, kwa nini tusifanye hivyo? 

Miaka miwili tu iliyopita, tulikuwa na maandamano makubwa zaidi kwa ajili ya maisha ya watu weusi katika historia ya dunia kwa sababu mtu mweusi, George Floyd, aliuawa na afisa wa polisi mweupe, ambaye alibana oksijeni kwa mtu huyu kwa dakika nane. 

Wale wanaosema kwamba ikiwa tunazungumza juu ya hili, tunaifanya kuwa mbaya zaidi, ni wazi sio watu wanaoishi na kuteseka chini ya hali ya historia hii. Binafsi ninaamini kuwa nuru ni dawa bora zaidi ya kuua viini tuliyo nayo, ili kukiri na kusema ukweli kuhusu historia yetu. Na kisha tunaweza kuanza kurekebisha. 

Habari za UN: Je, ungependa Waafrika wachukue nini kutoka katika The 1619 Project? 

Nikole Hannah-Jones: Hilo ni swali zito na gumu kwa sababu tunajua kwamba watu wa Afrika, hasa katika Afrika ya Magharibi na Kati, pia walijihusisha na biashara ya utumwa. Nadhani kukiri kilichotokea ni muhimu pia katika bara la Afrika ili kuelekea kwenye upatanisho. 

Hakuna kinachoweza kufanywa kubadilisha historia. Lakini tunachoweza kufanya ni kukiri kilichotokea na kisha kujaribu kujenga mahusiano pamoja. 

Nadhani Wamarekani weusi wangependa kuwa na uraia katika bara hili (la Afrika) na kuweza kujenga mahusiano haya katika daraja hilo. Nadhani upatanisho huo unaweza kuwa na nguvu sana kwetu sote. 

UN News: Wakati wa hotuba yako kwa Baraza Kuu, uliangazia upinzani na fidia kwa watumwa. Kwa nini nguzo hizi ni muhimu kwa kusonga mbele katika njia ya kujenga kutoka katika urithi wa utumwa? 

Nikole Hannah-Jones: Ninashukuru sana kwamba Umoja wa Mataifa mwaka huu unaangazia upinzani, kwa sababu njia ambayo tunafundishwa kwa kawaida historia hii ni kwamba kwa namna fulani watu weusi, watu wa Afrika walijisalimisha kwa utumwa wao, na hii inatumika kama kuhalalisha utumwa. 

Pia, kwangu, huondoa ubinadamu wetu, kwa sababu sio kawaida kutopigana na utumwa. Hata hadithi ya kufutwa kwa utumwa inawahusisha watu weupe kwa namna ambayo inatunyang'anya umuhimu wetu. 

Si kweli kwamba, siku moja, Uingereza, ambayo ilikuwa taifa kubwa zaidi la biashara ya watumwa ulimwenguni, iliamua tu “hatutaki kufanya hivi tena kwa sababu ni kosa.” Ni maasi na uasi wa watu waliokuwa watumwa ndio uliifanya Dola ya Uingereza isiwezekane kuendelea kuingiza Waafrika katika makoloni yake. 

Na kisha ilipoamua kuwa haiwezi kufanya hivyo tena, pia ni wazi hawakutaka nchi nyingine kuifanya, kwa sababu watakuwa na faida ya ushindani. Hivyo ndivyo tulivyofikia kuzuiwa kwa biashara ya kimataifa ya utumwa. 

Habari za UN: Ulipendekeza katika hotuba yako kwamba upinzani huu uliendelea hadi Karne ya Ishirini. 

Nikole Hannah-Jones: Tunafikiria Marekani kama kivutio kwa watu waliokandamizwa katika maeneo mengine wanaokuja Marekani. Jambo ambalo hatuzungumzii ni jinsi watu weusi katika nchi hii walivyonyimwa demokrasia, walinyimwa haki zile zile ambazo Wazungu weupe wangeweza kupata mara moja walipokuja. 

Kulikuwa na uhamiaji mwingine, sio tu wa wahamiaji wanaokuja Marekani, lakini watu weusi Kusini. 

Milioni sita, uhamiaji mkubwa zaidi katika historia ya Marekani, waliondoka Kusini, mara nyingi chini ya kificho cha giza kwa sababu walilazimishwa kufanya kazi huko chini, na watu weupe ambao walikuwa wakinyonya kazi yao hawakutaka waondoke. 

Waliamua kwamba wangekuwa wakimbizi katika nchi yao na kuhamia kaskazini kutafuta maisha bora na fursa bora zaidi. 

Ninahisi kwamba, kama watu wengi zaidi duniani kote wangeelewa hadithi ya Uhamiaji Mkuu, wangejiona wenyewe, hadithi yao ya wahamiaji katika hadithi ya Wamarekani weusi, kinyume na kutaka kusema, "Kwa nini haufanyi vizuri zaidi katika nchi hii?, fadhila kubwa? Kwa nini hutumii fursa yako?” 

Kuhusu fidia, sidhani kama tunaweza kuwa na mazungumzo kuhusu mojawapo ya uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya ubinadamu, na tusoizungumze kuhusu fidia.   

Ninaona kwamba, katika Mkutano Mkuu, msemaji wa nchi za Ulaya Magharibi alionekana kupendelea kuzungumza juu ya utumwa wa kisasa, ambao, bila shaka, ni janga kubwa, na kwamba sisi sote tunapaswa kupigana. 

Ni rahisi kuzungumza juu ya utumwa mahali pengine kuliko kukabiliana na uhalifu halisi. Ni lazima tuwe na fidia, na ninaamini katika fidia za kifedha katika ulimwengu wa Atlantiki. Na kuna mazungumzo tofauti kuhusu fidia kwa ukoloni pia. 

Watu weusi katika Amerika, kwa mfano, wana moja ya kumi ya utajiri wa Wamarekani weupe. Mtu mweusi aliye na mtoto ana theluthi moja ya utajiri wa Wamarekani weupe. 

Na sio kwa sababu Wamarekani weusi kwa namna fulani ni wavivu, hawataki elimu, hawataki nyumba bora, hawataki kufanya kazi. Tunajua kwamba hiyo si kweli. Kwa kweli, sielewi jinsi watu ambao walilazimishwa kufanya kazi kwa ajili ya watu wengine wanaweza kuchukuliwa kuwa wavivu. 

Angalia Haiti, sehemu ambayo ililazimika kulipa fidia kwa mabwana wa kizungu kwa sababu watumwa walijikomboa.  

Na katika Marekani, kikundi pekee cha watu waliopata malipo kwa ajili ya utumwa walikuwa wamiliki weupe wa watumwa katika Washington, D.C. 

Habari za UN: Umoja wa Mataifa unapaswa kufanya nini ili kusaidia mradi huu unaoitwa 1619 Project? 

Nikole Hannah-Jones: Ninaipongeza UN kama chombo kwa kutoa ripoti kuhusu ubaguzi wa rangi nchini Marekani na kuwa tayari kupinga unafiki wa nchi hiyo kwa njia ambazo mara nyingi huzioni. 

Lakini lazima kuwe na kazi ya nguvu zaidi kuhusu suala la fidia. 

Pia kuna suala kuhusu uwakilishi katika Baraza Kuu. Tunaweza kuangalia mataifa mengi katika ulimwengu wa Atlantiki ambayo yalikuwa mataifa yaliyokuwa yakishikilia watumwa, na hatuoni diaspora ya Kiafrika ikioneshwa nani anakuwa katika nafasi kama hizi. 

Ninadhani kuna mengi ya kufanya. Lakini pia ninaamini kwamba Umoja wa Mataifa umeongoza katika maeneo muhimu sana. 

Imekuwa uzoefu wa hali ya juu kuwa hapa na kuweza kuhutubia Mkutano Mkuu. 

Nilisimulia kisa cha bibi yangu ambaye alikuwa na elimu ya darasa la nne, ambaye alizaliwa kwenye shamba la pamba, ambaye alifanya kazi za ndani hadi alipostaafu, na kamwe hakuweza kufikiria kwamba kujitolea kwake yake yote ingeniruhusu mimi kuzungumza kwa niaba ya watu wetu katika mababu zetu kwa njia hii. 

Ninaondoka leo nikijsikia fahari sana, na kuheshimiwa sana, na ninahisi uwepo wa mababu zetu karibu nasi.