Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

“Watumwa” waendelea kuteseka nchini Mali: UN yatoa tamko

Mali ilipiga marufuku utumwa mwaka 1905, lakini baadhi ya watu bado wanaendelea kuonekana kuwa watumwa sababu mababu zao walikuwa watumwa
MINUSMA/Gema Cortes
Mali ilipiga marufuku utumwa mwaka 1905, lakini baadhi ya watu bado wanaendelea kuonekana kuwa watumwa sababu mababu zao walikuwa watumwa

“Watumwa” waendelea kuteseka nchini Mali: UN yatoa tamko

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa hii leo wameitaka serikali ya Mali iwalinde watu wanaoitwa watumwa ndani ya nchi hiyo, kufuatia ongezeko maradufu mwaka huu la vitendo vya ukatili dhidi yao, ikilinganishwa na mwaka 2020.  

Taarifa kutoka ofisi ya Kamishna Mkuu wa haki za binadamu mjini Geneva, Uswisi kwa vyombo vya habari imesema, wataalamu hao wametoa wito huo kufuatia tukio la tarehe 4 mwezi huu wa Julai huko mashariki mwa mkoa wa Kayes ambako wananchi kwenye kijiji cha Makhadougou walitumia silaha kama mapanga kuzuia watu hao wanaoitwa watumwa kushiriki kwenye shughuli za kilimo. Watu 12 wakiwemo wanawake 3 ambao hawakushiriki katika vurugu hizo walijeruhiwa.
“Mashambulio ya kila wakati na yale ya kimfumo kwa watu ambao wanachukuliwa kuwa watumwa hayakubaliki na lazima yasitishwe mara moja” amesema Alioune Tine mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa nchini Mali. 
Naye mwandishi maalum wa Umoja wa Mataifa Tomoya Obokata, amezungumzia utumwa wa kisasa nakusisitiza “Mashambulizi mabaya kama haya, hayaendani na jamii yenye kujumuisha watu wote na nilazima tuyalaani kwa nguvu zote”
Kwa mwaka huu pekee tayari watu 62, kati yao wanaume 57 na wanawake 5 wamejeruhiwa katika vurugu kwenye mkoa wa Kayes, na watu 80 wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Watu hawa ni zaidi ya mara mbili ya mwaka 2020. 


  Utumwa katika Karne ya 21 

Nchi ya Mali ilipiga marufuku utumwa mwaka 1905, lakini mfumo wa “utumwa wa asili” ungali unaendelea ambapo familia ambazo mababu zao walikuwa watumwa wanaendelea kuonekana watumwa mbele ya familia ambazo mababu zao walikuwa mabwana. 
Watu ambao wanatoka kwenye utumwa wanafanya kazi bila kulipwa na wananyimwa mahitaji muhimu ya haki za binadamu na utu. Watu ambao wanakataa kufanyishwa kazi kama watumwa pamoja na asasi za kiraia zinazotetea kupinga utumwa mara kwa mara hushambuliwa na viongozi wa kimila au kidini na washirika wao, na wakati mwingine mamlaka za serikali. 
“Ongezeko kubwa la mashambulizi mwaka huu linaonesha serikali imeshindwa kuwalinda watu wake, hasa wale ambao tayari wanateseka na ubaguzi pamoja na vurugu” amesema mtaalamu Obokata. 


  Sheria ya jinai dhidi ya utumwa

Wataalamu wa UN wamerejea ushauri wao kwa nchi ya Mali kutunga sheria ya jinai dhidi ya utumwa katika nchi hiyo 
“Inatia huzuni sana, kuona mpaka sasa hakuna hata mtu mmoja ambaye ameshitakiwa tangu matukio ya mwaka jana (2020) yatokee. Serikali kushindwa kuwawajibisha wanaoendeleza shughuli za utumwa inatuma picha na ishara mbaya. viongozi wa kimila na kidini wanaoendeleza machafuko hayo lazima wachukuliwe hatua” 
Pia wameeleza lazima jamii za wananchi wa Mali zibadilike kuhusiana na suala hilo la utumwa, ili iweze kusonga mbele na kutambua kuwa kila mwananchi wa nchi hiyo kama mtu mwingine yeyote ulimwenguni anahaki sababu ni binadamu. 
“Ni muhimu kuachana na urithi wa utumwa unaotokana na asili kwa kutambuakwamba raia wote wa nchini Mali wana haki zote na uhuru uliowekwa katika Azimio la ulimwengu wa haki za binadamu na mkataba wa Afrika wa haki za binadamu.” amemalizia Mtaalamu Tomoya Obokata
Hakutakiwi kuwa na ubaguzi wa rangi, jinsia, lugha, dini, kisiasa au mtazamo, kitaifa au kijamii, kutokana na mali au kuzaliwa.