Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bintou Keita wa Guinea kuongoza MONUSCO

Bintou Keita kutoka Guinea, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN /Rick Bajornas
Bintou Keita kutoka Guinea, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Bintou Keita wa Guinea kuongoza MONUSCO

Amani na Usalama

Bintou Keita wa Guinea ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuwa mwakilishi wake maalum nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO.
 

Bi. Keita anachukua nafasi ya Leila Zerrougui kutoka Algeria, ambaye anatamatisha jukumu lake mwezi ujao wa Februari. Guterres amemshukuru Bi. Zerrougui kwa huduma yake na mchango wake muhimu kwa MONUSCO.

Bi. Keita anachukua jukumu hilo jipya akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika masuala ya amani, usalama, maendeleo, kibinadamu na haki za binadamu, wakati akifanya kazi pia katika masuala ya utatuzi wa migogoro na hata mazingira baada ya mizozo.

Tangu mwezi Januari mwaka 2019 amekuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu Afrika katika idara ya Siasa na Ujenzi wa Amani ya Umoja wa MAtaifa na operesheni za kisiasa. Halikadhalika amewahi kuwa Msaidizi wa

Katibu Mkuu katika masuala ya operesheni za ulinzi wa amani tangu Novemba 2017 hadi Desemba 2018.
Kati ya mwaka 2015 na 2017, Bi. Keita alikuwa Naibu Mwakilishi Maalum wa ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa jimboni Darfur nchini Sudan, UNAMID.

Aliongoza pia juhudi za Umoja wa Mataifa za kukabili Ebola huko Sierra Leone halikadhalika Naibu Mwakilishi mtendaji wa Katibu Mkuu kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi.

Alijiunga na Umoja wa Mataifa mwaka 1989 na ameshika nyadhifa mbalimbali andamizi kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Chad, Jamhuri ya Congo, Madagascar, Cape Verde, Rwanda, Burundi na makao makuu New York, Marekani.