Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi Mkuu Mpya wa ILO kujulikana leo

Wafanyakazi wakisaka madini Camarines Norte, Ufilipino.
© ILO/Minette Rimando
Wafanyakazi wakisaka madini Camarines Norte, Ufilipino.

Mkurugenzi Mkuu Mpya wa ILO kujulikana leo

Masuala ya UM

Hivi sasa wajumbe wa Baraza la uongozi la shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO wanapiga kura ya siri kuchagua mkurugenzi mkuu mpya ambaye atatangazwa punde baada ya uchaguzi kukamilika .

Wanaoshirika kinyang’anyiro hicho ni wagombea watano watatu wanaume na wawili wanawake.

Majina ya wagombea ni Gilbert Houngbo kutoka Togo, Mthunzi Mdwaba Afrika Kusini, Kang Kyung-wha - Korea, Muriel Pénicaud -Ufaransa na Greg Vines kutoka Australia.

Fahamu mchakato wa kumpata Mkurugenzi

Mchakato wa kumpata mkurugenzi mkuu wa ILO ni wa takriban siku nzima ambapo kunakuwa na duru kadhaa za kupiga kura za sir na kisha kufuatiwa na mapumziko ya angalau dakika 45 kati ya kila duru ya upigaji kura hadi hapo mshindi wa mwisho atakapochaguliwa.

Katika kila duru, wajumbe wa baraza la uongozi wanapiga kura na mgombea aliye na idadi ndogo ya kura atatoka hadi mgombea apate zaidi ya nusu ya kura za wapiga kura wote.

Baada ya kila awamu majina ya waliosalia yataonekana kwenye tovuti ya Baraza inaloongoza.

Kumtangaza Mshindi

Kutokana na vikwazo vya kujikinga na Corona au COVID-19 waandishi wa habari na wananchi hawaruhusiwi kushuhudia mchakoto huu katika jengo la ILO.

Hata hivyo mara tu jina la mgombea aliyechaguliwa kujulikana ILO itatoa taarifa kwa vyombo vya habari, kumtangaza mshindi wa kura na wakati huo huo Kikao cha Baraza hilo kilichokuwa kinapiga kura kitakuwa mubashara na Mkurugenzi Mkuu mteule atatoa taarifa ambayo itatangazwa kwenye tovuti ya ILO.

Ukitaka kufahamu wasifu wa wagombea watano wanaowania nafasi hiyo ya ukurugenzi bofya link hii hapa ambapo pia utaweza kuona rekodi za midahalo ya hadhara ya wagombeaji iliyofanyika mwezi  Februari mwaka huu 2022 kwa kubofya hapa .