Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yatenga dola milioni 2.5 kuisaidia Madagascar. Kuna uwezekano wa kimbunga kingine

Zaidi ya watu 7,9000 wanaishi katika kituo cha msaada wa watu walioathirwa na kimunga nchini  Madagascar
© UNICEF Madagascar
Zaidi ya watu 7,9000 wanaishi katika kituo cha msaada wa watu walioathirwa na kimunga nchini Madagascar

OCHA yatenga dola milioni 2.5 kuisaidia Madagascar. Kuna uwezekano wa kimbunga kingine

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA Martin Griffiths, ametangaza kutenga dola milioni 2.5 kutoka katika mfuko wake wa dharura za kibinadamu, CERF ili kusaidia mwitikio wa kibinadamu wa sekta mbalimbali nchini Madagascar.

Msaada huo ni pamoja na kutoa maji ya kunywa na chakula, huduma za afya kwa simu, huduma ya afya ya uzazi, usaidizi kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia, vifaa vya makazi na bidhaa za msingi za nyumbani, usaidizi kwa shule na usaidizi wa vifaa. 

Wakati huo huo, jamii zilizoathiriwa na Kimbunga cha Tropiki Batsirai wanaanza kujenga upya na kurejea makwao, pale inapowezekana, lakini wengi bado wanahitaji msaada wa haraka.  

Takriban watu 21,000 bado wamekimbia makazi yao, na nyumba 20,500 zimeharibiwa, zimejaa mafuriko, au kuharibiwa. Shule nyingi na vituo vya afya vinaendelea kufungwa au kufanya kazi kwa kiasi. 

“Ni muhimu kwamba urejeaji wowote salama, wenye kuzingatia utu, hiari na watu wawe wamearifiwa vya kutosha, hasa kwa kuzingatia uwezekano wa hali mbaya ya hewa katika siku zijazo.” Imeeleza OCHA

Takriban watu 270,900 wameathiriwa na kimbunga Batsirai na wanahitaji makazi, maji na usafi wa mazingira, elimu na huduma za afya na msaada wa haraka wa chakula, kwa mujibu wa matokeo ya tathmini ya mahitaji ya haraka ya kisekta iliyofanywa kwa pamoja na Serikali na washirika wa kibinadamu. Taarifa ya OCHA inaeleza kuwa, “takriban dola za Marekani milioni 26.8 zitahitajika katika muda wa miezi mitatu ijayo ili kuokoa maisha na kurejesha huduma muhimu zaidi.” 

Wakati jamii zikiwa ndio kwanza zinapata nafuu kutokana na kimbunga Ana na Kimbunga Batsirai, kuna uwezekano wa kutokea kimbunga kingine kifahamikacho kama  Emnat ambacho mfumo wake unajiunda katika Bahari ya Hindi na kinaweza kuipiga Pwani ya mashariki ya Madagascar hivi karibuni tarehe 22 mwezi huu wa Februari.