Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wahifadhi kidijitali nyaraka za zaidi ya miaka 100

Mchakato wa nyaraka za mwanzoni kabisa za Umoja wa Mataifa
UN Photo.
Mchakato wa nyaraka za mwanzoni kabisa za Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa wahifadhi kidijitali nyaraka za zaidi ya miaka 100

Masuala ya UM

•    Nizile za Shirikisho la Kimataifa au League of Nations

•    Zinahifadhiwa kwenye jukwaa maalum na itakuwa bure kuzisoma

•    Zimewekwa pia kwenye kumbukumbu za kihistoria za UNESCO

•    Nyaraka hizo kutumika katika tafiti za uhusiano wa kimataifa

Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Geneva Uswisi iko mbioni kufungua kwa umma wa ulimwengu jukwaa la kidijitali la taarifa za Shirikisho la  Kimataifa au League of Nations, ambapo watu wataweza kusoma nyaraka, kutazama picha na mambo mengine ambayo yalitokea zaidi ya miaka 100 iliyopita. 

Katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na ofisi hiyo Umoja wa Mataifa , Blandine Blukacz-Louisfert, Mkuu wa kitengo cha Kumbukumbu za Taasisi katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva anasema kazi hii iliyoanza takriban miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi. 

“Ilikuwa mwaka wa 2017, tulipoanzisha mpango huu wa kuweka nyaraka kidijitali, ikiwa ni mradi wa Hifadhi ya Kumbukumbu za Umoja wa Mataifa, tulikuwa na kurasa milioni 15 za karatasi. Kurasa hizi zilikuwa na zaidi ya umri wa miaka 100, zilikuwa dhaifu sana na tofauti. Embu fikiria tulikuwa na kurasa hizi milioni 15 mbele yetu, na tunatakiwa kuzigeuza kuwa majalada ya kidijitali. Mwisho wa mradi ni  mwaka huu na tutakuwa na Terabytes 250 za takwimu.”

Unaweza kudhani ilikuwa rahisi na tayari walikuwa wanajua namna bora ya kuhifadhi nyaraka hizo lakini Francesco Pisano Mkurugenzi wa Maktaba na nyaraka anasema hawakuwa na majibu yote. “Tulipoanza, hatukujua ni teknolojia gani inaweza kutumika katika uhifadhi wa nyenzo za kidijiti. Kwa hivyo, hili tulilofanya kidogo tunaweza kusema ni kama kuvumbua kitu maana ulikuwa wakati wa kutumia teknolojia ya diski ambayo inaweza kuruka, na hapo ilibidi kuanza kujiuliza, ninawezaje kufanya hii nyaraka isomeke katika miaka 50 ijayo? Na unajua taknolojia itakuwa ni nyingine kabisa lakini hujui kama ni kuhifadhi nyaraka hizi hewani kwa sababu bado teknolojia hiyo haijavumbuliwa.” 

Maonyesho yaliyoandaliwa kuadhimisha Kumbukumbu ya Miaka Sitini ya kikao cha kwanza cha Baraza la Umoja wa Mataifa, kilichofunguliwa tarehe 15 Novemba 1920, yalitazamwa katika Ukumbi wa Umma wa jengo la Baraza Kuu la Makao Makuu kuanzia katikati ya Novemb
UN Photo/Milton Grant
Maonyesho yaliyoandaliwa kuadhimisha Kumbukumbu ya Miaka Sitini ya kikao cha kwanza cha Baraza la Umoja wa Mataifa, kilichofunguliwa tarehe 15 Novemba 1920, yalitazamwa katika Ukumbi wa Umma wa jengo la Baraza Kuu la Makao Makuu kuanzia katikati ya Novemb

Pamoja na kutokuwa huko na uhakika lakini wameweza kufanikiwa, na sasa mbali na nyaraka zakuandikwa jukwaa pia linajumuisha nyenzo za kuona, kama vile Mkusanyiko wa Picha za shirikisho la Kimataifa. Idadi ya wasomaji nayo imeongezeka maradufu kama anavyobainisha Blandine Blukacz mkuu wa Kitengo hicho cha kumbukumbu.

“Hapo awali, watu walipaswa kuja kibinafsi hapa ofisini kwetu ili kuweza kusoma hizi nyaraka. Kwa ujumla tulikuwa na watu wapatao 150 wanaokuja na kuzipitia hizi kumbukumbu kwa mwaka. Lakini sasa, baada ya kuzindua jukwaa la kidigitali mnamo mwezi Desemba mwaka 2021 hadi mwezi Januari mwaka huu 2022 zaidi ya watu 1,200, na hawa ni watu tofauti walitembelea jukwaa hili. Hivyo, ni kweli tumekuwa na utofauti kubwa. Tulipata maoni kutoka kwa watumiaji, na wanasisitiza sana kuwepo na ufikiwaji wa nyaraka hizi kidemokrasia.”

 

 Ufunguzu wa  mkutano wa Mataifa ulifanyika Geneva tarehe 15 Novemba 1920
UN Photo/Jullien
Ufunguzu wa mkutano wa Mataifa ulifanyika Geneva tarehe 15 Novemba 1920

Mafanikio haya yamepongezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva, Tatiana Valovaya ambaye anauambia umma wa ulimwengu kuwa kufikia mwisho wa mwaka huu wa 2022 umma wa ulimwengu utaruhusiwa kusoma nyaraka hizo bila malipo mtandaoni na pia wanaangalia namna bora ya kuibua tafiti za kwenye historia ya ushirikiano wa mataifa mbalimbali. "Kwetu sisi, huu ni mwanzo tu wa mradi. Na mbali na haya yote ninaweza sema tunatekeleza mambo kwa vitendo. Na kila shaka tunakuletea wewe mdau wetu mawazo ya  Geneva kama kitovu cha historia ya ushirikiano la Kimataifa na kitovu cha maarifa.” 

Kuhifadhi na kukuza ufikiaji wa vyanzo vya msingi ndio msingi wa ujumbe wa Maktaba ya UN na Hifadhi ya Kumbukumbu ya Geneva. 

Nyaraka hizo pia zimesajiliwa kwenye Kumbukumbu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kwenye Daftari la Dunia ambalo huandika shughuli za taasisi iliyotangulia kwa Umoja wa Mataifa, kutoka 1919 hadi 1946.
Uwepo wa jukwaa hili unatoa fursa bora kwa watafiti kote ulimwenguni kukuza mitazamo mipya na mbinu mpya. Itachangia uelewa mzuri wa ushirikiano wa pande nyingi.

Jukwaa hili jipya linaweza kuchangia kuelewa vyema ulimwengu.