Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijinasaba vya mwili havitofautishi uwezo wa msichana na mvulana kwenye sayansi 

Bernice Armelle Bancole ni mwanasayansi katika Sayansi ya Kilimo. Anatoka Benin. Anataka kusaidia kutokomeza matumizi makubwa ya viua wadudu katika nchi za Afrika.
UNESCO/OWSD
Bernice Armelle Bancole ni mwanasayansi katika Sayansi ya Kilimo. Anatoka Benin. Anataka kusaidia kutokomeza matumizi makubwa ya viua wadudu katika nchi za Afrika.

Vijinasaba vya mwili havitofautishi uwezo wa msichana na mvulana kwenye sayansi 

Wanawake

Kuelekea siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi, Tume ya Taifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni, UNESCO nchini Tanzania, imesihi wadau mbalimbali wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati nchini humo, STEM wazingatie matamko mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kuhakikisha elimu inachangia katika maendeleo endelevu.

Kaimu Naibu Mtendaji upande wa Programu wa Tume hiyo Fatma Mrope ametoa kauli hiyo alipozungumza kwa njia ya mtandao na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania akisema, “kupitia hayo matamko ya kimataifa ndiko ambako unakuta ripoti mbalimbali. Kwa mfano sasa hivi kuna ripoti ya mstakabali wa elimu. Kwa hivyo vitu kama hivyo ndivyo vitatufanya na sisi tusibakie nyuma. Sasa hivi dunia imefikia hatua ya kufikiria tukae tujadili elimu hii inaonekana haileti maana ile tuliyoitegemea. Kwa hivyo sasa hivi tunazungumzia elimu ya maendeleo endelevu. Kwa hiyo hata tunapoadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi ni wajibu wetu pia kutafakari hayo mengine yanayohusiana na muktadha mzima wa sayansi na elimu.”  

Bi. Mrope amesema kwa upande wake Tume hiyo hata kabla ya kuanza kwa maadhimisho haya miaka 7 iliyopita imekuwa ikichukua kuhamasisha wanawake na wasichana kwa kuwa na dawati la wanasayansi wanawake.  

“Wale wanawake walikuwa wanapita kuhamasisha wasichana kwenye shule. Na sehemu ambayo walienda sana ni umasaini. Ule uhitaji kwamba ile jamii ni ambayo haikuwahi mapema katika michakato ya kuelimisha watoto wa kike. Lakini pia waliangalia katika maeneo mengine. Ukiacha dawatai la wanasayansi wanawake, lakini pia tumekuwa na utaratibu wa kuhamasisha kupitia taarifa za jamii ya kimataifa. Kuna programu ambayo imeanzishwa katika muktadha wa kijinsia zaidi. Katik kuitekeleza kwetu tulienda Karatu.” Ameeleza Bi Mrope. 

Na kisha akatoa ujumbe kwa watoto wa kike akisema,“kwanza watoto wenyewe wanasoma bailojia, wanasoma kwa hiyo wanasoma katika lile somo la jenetiki. Vinasaba vile vinavyotoka kwa wazazi, ukiacha vile vinavyotuletea utofauti basi vingine mgawanyo wake huwa hamna kusema huyu atakuwa hivi huyu atakuwa hivi. Kwa hiyo katika hali kama hiyo manake ni kwamba tunakuwa na uwezo sawa wa kuweza kufafanua mambo mbalimbali katika mchakato wa elimu.  Kwa hiyo niwape moyo watoto wa kike kwamba wanaweza na wanaweza kufika sehemu mbalimbali katika ngazi mbalimbali kupitia sayansi.”