Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbunifu aibuka na kifaa kisichotumia intaneti kwa ajili ya kufundisha lugha

Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.
UN Tanzania
Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.

Mbunifu aibuka na kifaa kisichotumia intaneti kwa ajili ya kufundisha lugha

Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya lugha mama maudhui yakiwa matumizi ya teknolojia katika kujifunza lugha mbalimbali, fursa na changamoto tunamulika ubunifu uliofanywa na kijana Ombeni Sanga wa kutumia kifaa kisichohitaji intaneti kujifunza masomo mbalimbali ikiwemo lugha ya Kiswahili. 

Ombeni Sanga mkazi wa Tanzania anasema ameamua kuibuka na kifaa hicho kisichotumia intaneti bali teknolojia ya kuweka sauti na roboti au akili bandia, ili kuwezesha wanafunzi hata wale wasio na uwezo waweze kujifunza na kurudia mara kwa mara masomo hata kama mwalimu hayuko darasani au hata wakiwa nyumbani. 

Akihojiwa na Evarist Mapesa wa Redio washirika SAUTI FM ya Mwanza Tanzania, Ombeni anasema “kiukweli sasa hivi vitu vingi vinakwenda na intaneti na kwenda na uhalisia wa mazingira yetu, maeneo mengi ya nchi hayana inteneti, na ili upate huduma ya intaneti lazima uwe na simu au kompyuta mpakato au tableti, nikaona wanafunzi wengi wana maisha ya hali ya chini na ndio maana nikaja na kifaa ambacho gharama yake ni chini ya dola 5, ndio tukaja na Boxpedia yenye mfumo wa mawimbi ya sauti ya MP3.” 

Mbunifu huyu anasema ametumia jina Boxpedia kwa sababu ni kitu ambacho kinabeba taarifa mbalimbali za mfumo wa sauti akiendelea kufafanua kuwa, “kifaa hiki licha ya kwamba hakitumii intaneti, kitakuwa na ufanisi kwa kuwafundisha watu lugha za kigeni. Lakini sisi tumejikita katika Kiswahili na Kiingereza ili kuandaa wanafunzi kuingia wa shule ya msingi kuingia sekondari.” 

Kifaa kitanufaisha watalii pia kujifunza Kiswahili 

Boxpedia ni kama roboti na inasimama badala ya mwalimu, “kwa hiyo ukishuka tu uwanja wa ndege, mradi una nyaraka yako, unajifunza matamshi na kila kitu bila hata mwalimu. Maudhui yanakuwa tayari yameshaingizwa kwenye kifaa.” 

Akifafanua kinavyofanya kazi Ombeni anasema, “kunafanyika maandalizi ambako kila somo au lugha linakuwa na namba yake na mwanafunzi anaweza kujifunza wakati wowote anataka hata kama mwalimu hayuko.” 

Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.
UN Tanzania
Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.

Changamoto anazokumbana nazo 

Ombeni anasema ameshakutana na watu na mashirika mbalimbali kuwaelezea kuhusu kifaa hicho lakini bado watu wanaamini kuwa ni lazima kuweko na intaneti. “unavyokuja kuwatoa watu kwenye  kile wanachoamini inakuwa ni safari ndefu lakini ambayo inaenda kufanikiwa muda si mrefu. Tumeona kuwa ili kutumia kifaa cha intaneti unahitaij simu, na  huwezi kupata simu chini ya dola 50 ambayo ni sawa na 150,000. Kwa hiyo kule shuleni kuna watoto hawana hata viatu vya kuvaa, atanunua lini kifaa cha 150,000 ili kupata fursa ya kujifunza apate kujifunza lugha mbalimbali na masomo yake. Hivyo tukaona tulete kifaa kisichotumia intaneti ambacho hata mzazi wake anaweza kuuza debe mbili za mahindi akanunua hiki kifaa na akajifunza.” 

Kiswahili ni lugha mama kwa wengi Afrika Mashariki 

Lugha mama ni ile ambayo mtu anaizungumza ya kwanza na inaweza kuwa pale alikozaliwa au ni lugha ya asili ya jamii yake. Kwa wengi wa wakazi wa nchi za Afrika Mashariki, Kiswahili ni lugha mama kwa kuwa inazungumzwa katika nchi zote za eneo hilo na zile za jirani na pia ni lugha ya kufundushia shuleni.  

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni, UNESCO linasema maudhui ya mwaka huu ya siku hii ni matumizi ya teknolojia katika kujifunza lugha mbalimbali, fursa na changamoto. 

UNESCO inasema janga la Corona au COVID-19 limefichua pengo la teknolojia kwa sababu kwa baadhi ya watoto walikosa vifaa vya kujifunzia kwa lugha yao ambapo sasa kupitia kifaa hiki kilichobuniwa na Ombeni Sanga mwanafunzi anaweza kujifunza kwa lugha yoyote kupitia mitaala ambayo imepitishwa na serikali. 

Kwa mujibu wa UNESCO kujifunza kwa kutumia lugha mbalimbali hasa lugha mama ni msingi wa ujumuishaji wa watoto kwenye elimu. 

Kwa sasa Ombeni anasema kifaa hicho kitafanyiwa majaribio kwenye shule moja nchini Tanzania mwezi mmoja ujao na mwanafunzi anaweza kuchagua mwalimu yeyote anayetaka kumsikiliza kwa kuwa kifaa kinaweza kuingia maudhui ya masomo ya mwalimu zaidi ya mmoja. 

Kijana huyu mbuni anasema “ingawa bado watu hawana imani nacho, nawajulisha kuwa mambo yanabadilika, halikadhalika sekta ya elimu kwa hiyo iko siku watu nao watabadili fikra zao na kuamini kifaa hiki kisichohitaji intaneti.”