Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMAS yaendelea na juhudi za kutegua mabomu ya ardhini Sudan Kusini ili maisha yaendelee

UNMAS imekuwa ikitegua mabomu ya ardhini Sudan Kusini yaliyoachwa kutokana na mgogoro.
UNMAS/Irina Punga
UNMAS imekuwa ikitegua mabomu ya ardhini Sudan Kusini yaliyoachwa kutokana na mgogoro.

UNMAS yaendelea na juhudi za kutegua mabomu ya ardhini Sudan Kusini ili maisha yaendelee

Amani na Usalama

Raia wa baadhi ya maeneo nchini Sudan Kusini wameendelea kuishi kwa mashaka kutokana na mabomu ya ardhini yaliyoko katika maeneo yao huku hatari zaidi ikiongezek katika msimu wa mvua ambapo maji husogeza mabomu hayo. Timu ya wataalamu kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuondokana na mabomu ya kutegwa ardhini, UNMAS pamoja na Mamlaka za Kitaifa wanafanya kazi kila siku nchini humo ili kuyadhibiti mabomu ambayo hayajalipuka. 

Wataalam wa kutegua mabomu wakiwa kazini nchini Sudan Kusini. Bomu la kutegwa ardhini limepatikana na kuharibiwa kitaalamu kwa kulipuliwa katika eneo lililo salama mbali na makazi ya watu.  

Ni kazi ambayo wataalamu hawa kutoka UNMISS na serikali ya Sudan Kusini, wanajitahidi kuifanya katika maeneo mengi nchini humo ili kuyaokoa maisha ya watu na mali zao. 

Mfano wa hivi karibuni ni Simon Tanguni ambaye alikuwa analima katika ardhi yake miezi sita iliyopita ambapo aligonga kitu kigumu ardhini kikalipuka na kuurarua mkono wake wa kulia.  Simon anasema, "nilipokuwa nikilima nyuma ya mti, niligonga kitu. Kisha nikakigonga tena, na nilifikiri ni jiwe kwa sababu kulikuwa na mawe mengi karibu na mti. Kwa hiyo, nilijaribu kuondoa jiwe kwa mkono wangu; kisha, ukatokea mlipuko.” 

Simon ana bahati aliweza kubaki hai katika mlipuko huu. Lakini mtu huyu ambaye amezoea kujitafutia riziki kupitia mikono yake, sasa hawezi kufanya kazi ili kutunza familia yake changa. Imebidi asaidiwe na jamaa zake.  alijitafutia riziki kupitia kazi ya mikono, hawezi kufanya kazi ili kutegemeza familia yake changa tena. Imebidi jamaa zake waingilie kati. 

Ili kuangazia athari zinazoendelea za mabomu ya ardhini nchini Sudan Kusini, Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Beysolow Nyati akiambatana na maafisa wa UNMAS ametembelea eneo la Gondokoro lililo nje kidogo yam ji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kujionea hali. Anasema, "tunahitaji familia kurejea katika maeneo ambayo waliishi kabla ya mgogoro. Tunahitaji kilimo kiendelee katika maeneo ambayo tunajua walikuwa na ardhi na watu waweze kuzalisha chakula cha kujilisha na kupunguza ukosefu wa usalama. Kwa ujumla, ni kuhusu usalama. Inahusu kutengeneza mazingira wezeshi kwa watu kuweza kuishi na kustawi.”