Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMAS yaendelea kunusuru maisha ya watu Sudan Kusini kwa kutegua mabomu ya kutegwa ardhini 

Mfanyakazi wa UNMAS akichunguza mabomu ya kutegwa ardhini, jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.
© UN Photo/Isaac Billy
Mfanyakazi wa UNMAS akichunguza mabomu ya kutegwa ardhini, jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.

UNMAS yaendelea kunusuru maisha ya watu Sudan Kusini kwa kutegua mabomu ya kutegwa ardhini 

Amani na Usalama

Wakati hatua kubwa imepigwa katika kuondoa na kutegua mabomu yote ya kutegwa ardhini na mabaki mengine ya vifaa vya milipuko ya vita nchini Sudan Kusini, baadhi ya jamii za nchi hiyo bado ziko hatarini kutokana na uwepo wa mabomu hayo. Moja ya jamii hizo ni  Gondokoro karibu na mji mkuu Juba, ambako kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya huduma za kutegua mabomu ya kutegwa ardhini UNMAS kazi kubwa inaendelea kuyaondoa kabisa mabomu hayo.

Katika jamii ya Gondokoro sasa maisha yameanza kurejea kawaida baada ya muda mrefu watu kulikimbia eneo hjilo lililokuwa uwanja wa vita kwa muda mrefu. 

Mabomu ya kutegwa ardhini yamekatili maisha ya watu na kuwaacha wengine na vilema vya maisha mwaka 2016 vita iliposhika kasi na wengi wakafungasha virago na kuliacha tupu hadi pale ofisi ya UNMAS ilipoamua kulivalianjuga suala la kuondoa na kutegua mambomu yaliyokuwa yametegwa ardhini na vilipuzi vingine vya mabaki ya vita hatua iliyotoa fursa kwa jamii hii kurejea makwao na kuendelea na maisha. 

Hata hivyo kutokana na ukubwa wa jamii yenyewe bado kazi inaendelea na Ilene Cohn, kaimu mkurugenzi wa ofisi ya UNMAS ametembelea eneo hilo kutathimini hatua zilizopigwa “Niko hapa ili kuelewa hasa jinsi operesheni ya kulinda amani ya UNMISS na Mamlaka ya kitaifa ya utekelezaji wa uteguzi wa mabomu ya ardhini wanavyoshirikiana ili kuhakikisha kuwa jamii zinazoishi katika eneo hili zinaweza kutumia ardhi hii kwa kilimo na ufugaji wa ng’ombe. Ninatumai kuwa barabara wanayotaka kutumia imejengwa kwa usalama na kwa ushirikiano yataondolewa mambo ya kutegwa ardhini ambayo ilijitokeza kwa njia ya kushangaza na tukayabaini miaka kadhaa iliyopita.” 

Kuondolewa kwa mabomu hayo katika barabara kuu ya Gondokoro kutaruhusu makampuni ya ujenzi kuendelea na shughuli zao, wafugaji kurejea katika makambi yao, wakulima kurejea mashambani na watu wote kurejea katika maisha ya kawaida. Jurkuch Barach ni mwenyekiti wa mamlaka ya kitaifa ya uteguzi wa mabomu ya ardhini Sudan Kusini NMAA anasema, “Kama kuna mabomu ya kutegwa ardhini, hakuna mtu atakayekuja katika eneo hili hadi tuhakikishe kuwa yameondolewa. Hii ndiyo sababu tunafurahi sana tunapopata usaidizi kutoka kwa UNMISS, UNMAS na jumuiya ya kimataifa ili kufanikisha mradi huu na watu waweze kutembea kwa uhuru katika eneo lote hilo.” 

Mabomu ya kutegwa ardhini na vifaa vingine vya mlipuko bado vinayafanya meneo mengi ya Sudan Kusini kuwa hatari kwenda na hilo linaathiri kila kitu kuanzia kilimo, ugawaji wa misaada ya kibinadamu hadi raia kurejea katika nyumba zao baada ya kukimbia machafuko na mafuriko.