Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madagascar: WFP yatoa msaada wa dharura baada ya kimbunga Batsirai 

Picha iliyopigwa kwa satellite ikionesha kujiunda kwa kimbunga kilichopewa jina Batsirai tarehe 2 Februari 2022.
©UNICEF/NOAA
Picha iliyopigwa kwa satellite ikionesha kujiunda kwa kimbunga kilichopewa jina Batsirai tarehe 2 Februari 2022.

Madagascar: WFP yatoa msaada wa dharura baada ya kimbunga Batsirai 

Msaada wa Kibinadamu

Saa chache baada ya kimbunga Batsirai kusababisha uharibifu mashariki mwa Madagascar, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP lilikuwa katika eneo la tukio likitoa msaada wa dharura. 

Wafanyakazi wa WFP katika eneo la tukio wanaripoti kuwa mji wa pwani wa Mananjary umeharibiwa kabisa. Nyumba zimesombwa na upepo mkali na ufikiaji katika eneo hilo kwa sasa unawezekana tu kwa njia ya anga. Eneo la Manakara, takribani kilomita 100 kuelekea kusini, haifikiki kwa barabara. 

Tathmini ya uharibifu bado inaendelea na hakuna majeruhi au vifo vilivyothibitishwa. Makadirio ya sasa ni kwamba watu 60,000 wanaweza kuathirika na wengine 150,000 waliokimbia makazi yao huenda wakaongezeka zaidi huku viwango vya maji ya mito na mifereji vikiendelea kuongezeka. 

"Mafuriko na hali mbaya ya hewa sio tu kwamba yameharibu nyumba na kuharibu mali, lakini zaidi ya yote yameharibu ustawi na vyanzo vya mapato ya familia zilizoathirika," Pasqualina Di Sirio, Mkurugenzi wa Nchi wa WFP nchini Madagascar amesema akiongeza kuwa, "familia zilizoathiriwa, ambazo kwa sasa ziko katika hali ya ufukara kabisa, zitaona hali zao za maisha zikizorota kutokana na kukosekana kwa usaidizi wa haraka hadi hali yao itakaporejea kuwa ya kawaida." 

Ili kuwasaidia wale waliopoteza kila kitu kutokana na kimbunga hicho, WFP kwa uratibu wa mamlaka za serikali, imeanza kusambaza chakula cha moto kwa watu 4,000 waliohamishwa na waliokimbia makazi yao. Kabla ya kimbunga hicho, WFP ilikuwa imeweka tayari tani 50 za akiba ya chakula, nusu huko Manakara, nusu huko Tamatave, miji miwili mikuu katika pwani ya mashariki/kusini-mashariki, kuweza kusaidia haraka watu 10,000 (kaya 2,000) kwa siku kumi. 

Katika siku zijazo, WFP inapanga kufanya usambazaji wa chakula na pesa kwa wale walioko katika uhitaji.