Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO kuhakikisha ufugaji samaki Zimbabwe una tija shambani hadi mezani 

Mfugaji wa samaki akilisha samaki aina ya sato katika moja ya mabwawa. Huu ni mradi wa FAO kupitia FISH4ACP na hapa ni nchini  Côte d'Ivoire moja ya nchi ambako mradi huo unatekelezwa kama ilivyo kwa Zimbabwe.
©FAO/Sia Kambou
Mfugaji wa samaki akilisha samaki aina ya sato katika moja ya mabwawa. Huu ni mradi wa FAO kupitia FISH4ACP na hapa ni nchini Côte d'Ivoire moja ya nchi ambako mradi huo unatekelezwa kama ilivyo kwa Zimbabwe.

FAO kuhakikisha ufugaji samaki Zimbabwe una tija shambani hadi mezani 

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linasema ingawa teknolojia ya ufugaji wa Samaki nchini Zimbabwe imekua bado lengo la kufanikisha uhakika wa chakula kwa kuhakikisha Samaki anafika mezani bado linakabiliwa na changamoto kwa kuwa gharama ya ufugaji ni ya juu halikadhalika gharama ya kitoweo hicho.

Kariba nchini Zimbabwe katika mabwawa ya ufugaji Samaki yanayomiliwa na Lake Harvest Farm, teknolojia ni ya kisasa kuanzia shambani hadi kiwandani ikiwemo uchambuzi wa samaki aina ya sato. 

Kutoka Kariba tunaingia Karoi, shamba lingine lingine la ufugaji samaki likimilikiwa na kampuni ya ufugaji samaki ya Edeni, na mmiliki wake Hafra Nanhanga, naye anafuga sato na anasema, “nilipoingia kwenye ufugaji wa sato, nilidhani ni rahisi, hasa tulipoanza kujenga mabwawa tulijua tunaweza kuchimba tu mashimo yetu na kujenga kuta, kumbe tunahitaji mashine za kuchimba.” 

Tariro Chari, Meneja Mkuu wa shamba la Lake Harvest  anasema samaki anafugwa majini kwa kati ya miezi sita hadi tisa kulingana na uzito anaotaka mnunuzi wa kati ya gramu 300 hadi 900 na “suala kubwa kwa mfugaji yoyote wa sato ni lishe ya Samaki, kwa sababu chakula kinagharimu asilimia 60 ya gharama zote za uendeshaji.” 

Kwa kutambua kuwa Zimbabwe ni nchi isiyo na baharí, shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO lilianzisha mradi wa kusaidia wafugaji wa Samaki ili kuongeza kipato na kuimarisha afya kupitia kitoweo cha Samaki, mradi unaoitwa FISH4ACP uliobuniwa na shirika la nchi za Afrika, Karibea na PAsifiki, na kutekelezwa na FAO

Mradi unawekeza kwenye mnyororo wa thamani wa ufugaji wa Samaki kuanzia shambani hadi mezani lakini bado ulaji samaki nchini Zimbabwe ni wastani wa kilo 2.6 kwa mtu mmoja kwa mwaka ilhali katika nchi za ukanda huo wastani wa ulaji ni kilo 6.  

Gilles Van De Walle wa kitengo cha ufugaji Samaki FAO anasema, “tunataka kufanya kazi kuanzia kwenye boti au kwenye nyavu hadi kwa walaji. Tunataka huu mnyororo uwe na manufaa kama inavyotakiwa.” 

FAO imetangaza mwaka 2022 kuwa mwaka wa kimataifa wa uvuvi wa kienyeji na ufugaji wa Samaki.