Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Anga ndio paa letu na ardhi ndio zulia letu, alalama mkimbizi Afghanistan

Familia za wakimbizi zikihaha kusaka maji katika mazingira ya baridi kali kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
© UNHCR / Andrew McConnell
Familia za wakimbizi zikihaha kusaka maji katika mazingira ya baridi kali kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Anga ndio paa letu na ardhi ndio zulia letu, alalama mkimbizi Afghanistan

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Afghanistan, majira ya baridi kali yamebisha hodi huku wakimbizi wa ndani waliosaka hifadhi kwenye mji mkuu Kabul wakihaha kujikinga na familia zao kwenye mahema yasiyo na vifaa vya kuleta joto, watoto, wanawake na wanaume wakiwa hatarini. 
 

Kuta zinaporomoka, maji yanavuja kwenye dari na mazingira tunamoishi ni mabaya mno! Ndivyo asemavyo Qhados, mkimbizi wa ndani huyu hapa wilaya ya Qharaga jijini Kabul nchini Afghanistan akiwa anatembea peku kwenye theluji akionesha nyumba anamoishi na familia yake ya mke na watoto.

Mavazi yao ni taswira halisi ya machungu wanayopitia kwa kuwa si mavazi sahihi kwenye majira ya baridi kali.

Mkewe Zarmina anasema tuna njaa, mara nyingine tunapitisha siku tatu bila mlo wa usiku.
Kwa Qhados ndoto yao ya kuwa Kabul mambo yatakuwa shwari haijatimia akisema, “hatujawa na furaha tangu tumefika hapa. Tunachoma taka za plastiki jikoni kupata joto. Wakati mwingine tunachoma majani kando ya barabara. Najaribu kupata fedha kwa kukusanya taka.”

Qhados na Zarmina wanawakilisha wakimbizi wa ndani milioni 9 nchini Afghanistan, na walioko hapa Kabul kwenye mahema yasiyokabili baridi wanahaha kuchoma kuni kupata joto, ambapo mmoja wao anasema “ ni theluji na mvua kwa hiyo si rahisi kupata kuni kavu.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema ingawa mapigano yameisha katika maeneo mengi nchini Afghanistan,  kuporomoka kwa uchumi kumezidisha machungu kwa watu wengi wakiwemo wakimbizi hawa.

Mkimbizi mmoja anasema, “haya ndio maisha yetu kwenye haya mahema. Hatuna nguo, hatuna pahala pa kuishi. Anga ndio paa letu na ardhi ndio zulia letu. Tunaishi mazingira haya wakati huu wa baridi kali.”

Kwa sasa UNHCR inatoa msaada wa fedha kwa zaidi ya kaya 20,000 zilizoko maeneo ya kati ambayo ni pamoja na Kabul na majimbo ya jirani, idadi ambayo ni mara 10 zaidi ya mwaka jana.

Tayari Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu ya kimataifa yamezindua ombi la fedha la dola bilioni 4.44 kusaidia watu milioni 22 nchini Afghanistan na wakimbizi milioni 5.7 walioko ndani na nchi tano jirani.