Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika, zaidi ya 85% ya watu bado hawajachanjwa hata dozi moja dhidi ya Covid-19 - WHO 

Mmoja wa Raia wa Uganda akipokea chanjo yake ya kwanza ya Covid-19 huko Hoima, Uganda.
John Kibego
Mmoja wa Raia wa Uganda akipokea chanjo yake ya kwanza ya Covid-19 huko Hoima, Uganda.

Afrika, zaidi ya 85% ya watu bado hawajachanjwa hata dozi moja dhidi ya Covid-19 - WHO 

Afya

“Hatuwezi kumaliza janga isipokuwa tukifunga pengo hili.” Ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, Dkt Tedros Ghebreyesus katika mkutano na waandishi wa habari hii leo mjini Genva Uswisi alipokuwa akieleza hali ya mapambano dhidi ya Covid-19. 

Pengo alilokuwa akilizungumzia Dkt Tedros ni la chanjo ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa barani afrika, asilimia 85 hawajapata chanjo japo hata moja dhidi ya ugonjwa wa Covi-19 ambao unasababishwa na virusi vya corona. 

Dkt Tedrs amesema pamoja na changamoto hizo, WHO inapiga hatua katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu kwa mwezi Desemba mwaka jana 2021, COVAX ilisafirisha zaidi ya mara mbili ya idadi ya dozi ilizozisafirisha mwezi Novemba, “na katika siku zijazo tunategemea COVAX kusafirisha dozi yake ya bilioni 1.” Amesema Tedros.   

Mkuu huyo wa WHO ameeleza kuwa baadhi ya vikwazo walivyokabiliana navyo mwaka jana vimeanza kupungua, “lakini bado tuna safari ndefu kufikia lengo letu la kuchanja asilimia 70 ya watu wa kila nchi ifikapo katikati ya mwaka huu. Nchi 90 bado hazijafikia lengo la asilimia 40, na 36 kati ya nchi hizo zimechanja chini ya asilimia 10 ya watu wao.” 

WHO pia inazingatia kwa uangalifu athari za Omicron dhidi ya chanjo. 

Mwezi Septemba mwaka jana, WHO ilianzisha Kundi la Ushauri wa Kiufundi kuhusu Uzalishaji wa Chanjo ya COVID-19 linalofahamika kama TAG-CO-VAC. Timu hiyo ya wataalamu inaangalia na kukagua athari za minyumbuliko ya ugonjwa katika uzalishaji wa chanjo. 

Jana, TAG-CO-VAC ilisisitiza hitaji la dharura la ufikiaji mpana wa chanjo zilizopo, na kwamba chanjo zaidi zinahitajika ambazo zina utendaji mkubwa zaidi katika kuzuia maambukizi na uambukizaji. 

"Mpaka chanjo kama hizo zitakapotengenezwa, muundo wa chanjo za sasa za COVID-19 zinaweza kuhitaji kuboreshwa, ili kuhakikisha kuwa zinaendelea kutoa viwango vilivyopendekezwa na WHO vya ulinzi dhidi ya maambukizo na magonjwa." TAG-CO-VAC pia ilisema kuwa mkakati wa chanjo wa kutegemea dozi za kurudiarudia mara kwa mara kwa chanjo ile ile hauwezi kuwa endelevu.  

Team hiyo ya wataalamu ilisisitiza kuwa wakati baadhi ya nchi zinapendekeza chanjo ya nyongeza, kipaumbele cha haraka kwa ulimwengu ni kuongeza kasi ya upatikanaji wa chanjo ya msingi, hasa kwa makundi ya watu walioko  katika hatari kubwa ya kuambukizwa. 

Dkt Tedrs ameeleza kuwa idadi kubwa ya watu wanaolazwa katika hospitali kote ulimwenguni hawajachanjwa na kwamba maambukizi mengi yanamaanisha kulazwa hospitalini zaidi, vifo vingi, watu wengi zaidi kukosa kazi, wakiwemo walimu na wahudumu wa afya, na hatari zaidi ya minyumbuliko mingine kuibuka, “ambayo inaweza kuambukiza na kuua zaidi kuliko Omicron. Idadi kubwa ya maambukizi inamaanisha shinikizo zaidi kwa wafanyakazi wa afya ambao tayari wameelemewa na wamechoka.”