Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani wafanikisha kutenganishwa kwa watoto mapacha

Watoto mapacha Mohamed na Ahmed wakiwa wamebebwa na wazazi wao kwenye uwanja wa ndege wa Sana'a  nchini Yemen siku waliyowasili tarehe 2 Desemba 2021 baada ya upasuaji uliofanikishwa na wadau kupitia UNICEF huko Jordan.
© UNICEF/UN0565875/Ahmed Abdulhaleem
Watoto mapacha Mohamed na Ahmed wakiwa wamebebwa na wazazi wao kwenye uwanja wa ndege wa Sana'a nchini Yemen siku waliyowasili tarehe 2 Desemba 2021 baada ya upasuaji uliofanikishwa na wadau kupitia UNICEF huko Jordan.

Wahisani wafanikisha kutenganishwa kwa watoto mapacha

Afya

Mapacha wawili waliozaliwa huko Sana’a nchini Yemen wakiwa wameungana kuanzia kifuani hadi tumboni hatimaye wametenganishwa huko Jordan na wamerejea nyumbani.

Ahmed na Mohammed walizaliwa mwezi Desemba mwaka jana wa 2020 wakiwa wameunganika kifua na tumbo, hali ambayo ililazimu madaktari mjini Sana’a kuomba usaidizi kutoka UNICEF ili wasafirishwe kwa ndege hadi Jordan kwa ajili ya upasuaji wa kutenganishwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF lilichangisha fedha za kufanikisha upasuaji huo uliofanyika kwenye mji mkuu wa Jordan, Amman.

Upasuaji ulinfanyika mwezi Julai katika hospitali maalum mjini Amman, na baada ya miezi kadhaa ya kupata matibabu na kupona hatimaye wamerejea nyumbani Yemen.

Watoto mapacha Mohamed na Ahmed walipowasili uwanja wa ndege wa Sana'a Yemen baada ya upasuaji wa kuwatenganisha huko Jordan.
© UNICEF/UN0565887Moohialdin Fuad
Watoto mapacha Mohamed na Ahmed walipowasili uwanja wa ndege wa Sana'a Yemen baada ya upasuaji wa kuwatenganisha huko Jordan.

Upasuaji huo umefanikishwa kutokana na ukarimu wa wahisani mbalimbali binafsi.
Katika uwanja wa ndege wa Sana’a wazazi wa watoto hao hawakuficha tabasamu yao baada ya kuwabeba watoto wao mikononi mwao.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen Philippe Duamelle amesema wahisani binafsi na timu ya madaktari katika hospitali mjini Amman samamba na mamlaka za Jordan vimefanikisha upasuaji huo.
Hata hivyo amesisitiza kuwa ingawa simulizi hiyo imekuwa ya matumaini kwa familia hiyo moja ya mapacha hao, bado mamilioni ya watoto nchini Yemen wanaendelea kutaabika kimya kimya.

Ametaja mahitaji mengine kuwa ni elimu, ulinzi na huduma kama vile maji.