Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Yemen ni ‘mwiba’ kwa mama na mtoto

Saleh, mtoto mwenye  umri wa miezi minne, akiwa amelazwa katika hospitali kuu ya Hudaidah na mama yake Nora. Takribani watoto  500,000 nchini Yemen na wanawake wazazi milioni 2 wako hatarini kufariki dunia kutokana na unyafuzi.
UN OCHA/GILES CLARKE
Saleh, mtoto mwenye umri wa miezi minne, akiwa amelazwa katika hospitali kuu ya Hudaidah na mama yake Nora. Takribani watoto 500,000 nchini Yemen na wanawake wazazi milioni 2 wako hatarini kufariki dunia kutokana na unyafuzi.

Mzozo wa Yemen ni ‘mwiba’ kwa mama na mtoto

Afya

Mzozo nchini Yemen ukiwa umedumu kwa miaka minne sasa, wananchi wanaelezea vile ambavyo mazingira yamekuwa magumu kiasi kwamba hawawezi kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku ikiwemo chakula.

Miongoni mwa wananchi  hao ni Kefaya, mama mwenye watoto sita ambaye amelieleza shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu, UNFPA kuwa mzozo huo uliosababisha vizuizi katika baadhi ya maeneo umesababisha yeye na watoto wake kula  mlo mmoja kwa siku, mlo ambao ni mkate kwa maji.

Amesema wakati mwingine hana uhakika wa mlo ufuatao na hafahamu ni jambo gani anaweza kufanya ili watoto wake waweze kuishi.

Naye Umm mwenye umri wa miaka 28 na mama wa watoto watatu anasema kuwa “mume wangu aliuawa vitani na ameniachia watoto niwalee. Kila siku hali inazidi kuwa mbaya.”

Umoja wa Mataifa unasema kuwa Yemen hivi sasa ni nchi yenye janga baya zaidi la kibinadamu duniani ambapo zaidi ya watu milioni 22 wanahitaji msaada wa kibinadamu.

“Theluthi mbili ya wakazi wa Yemen hawana uhakika wa mlo wao ujao,” umesema Umoja wa Mataifa.

Hali ni mbaya zaidi kwa wajawazito, ambapo UNFPA inasema takribani wajawazito milioni 2 na wanawake wanaonyonyesha watoto wako hatarini kufariki dunia iwapo baa la njaa litakumba nchi hiyo.

“Wanawake milioni 1.1 wakiwemo wajawazito na wanaonyonyesha tayari wana utapiamlo uliokithiri, wengine wako hatarini mimba zao kutoka au kujifungua watoto njiti,” imesema UNFPA.

Amma mmoja wa wanawake waliojifungua hivi karibuni ni shuhuda wa mazingira magumu ya ujauzito na amesema, “pindi nilipojifungua mtoto wangu wa pili, alikuwa ana kasoro na alifariki dunia tu baada ya kuzaliwa. Sikupata dawa na chakula cha kutosha wakati wa ujauzito.”

Hata hivyo UNFPA imeshapatia mafunzo wakunga 7,500 nchini Yemen na kwa kushirikiana na wadau inasaidia wakunga 2500 wasioajiriwa sambamba na kuweka kliniki kwa ajili ya mama na mtoto.

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.