Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Kuunganishwa tena kwa wapiganaji wa zamani wa FARC katika mashirika ya kiraia kunawezekana katika mji mdogo wa Llano Grande huko Dabeiba, Colombia

Miaka mitano baada ya makubaliano ya amani, Llano Grande Colombia waunda familia kutoka sehemu tofauti.

UNMVC/Esteban Vanegas
Kuunganishwa tena kwa wapiganaji wa zamani wa FARC katika mashirika ya kiraia kunawezekana katika mji mdogo wa Llano Grande huko Dabeiba, Colombia

Miaka mitano baada ya makubaliano ya amani, Llano Grande Colombia waunda familia kutoka sehemu tofauti.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaelekea Colombia wiki hii kuadhimisha miaka mitano tangu kutiwa saini kwa mapatano ya amani yaliyomaliza miaka 50 ya mzozo nchini humo, na shughuli zake zitajumuisha kusafiri hadi katika kijiji cha Llano Grande, ambako wakazi wa mji huo. na wapiganaji wa zamani wanafanya kazi pamoja ili kupata maisha bora ya baadaye. 

Kijiji hiki kidogo ni mfano wa jinsi gani kupitia njia ya amani, maridhiano na ari familia mpya inaweza kuundwa kutoka miongoni mwa maadui wa zamani. 

UN News imesafiri hadi katika eneo hilo kabla ya kuwasili kwa Katibu Mkuu, ambaye ziara yake ya siku mbili itaanza Jumanne tarehe 23 Novemba. 

Familia ya Llano Grande inasoma maandishi kwenye michoro ya lango la mji huu wa Colombia ambapo wapiganaji wa zamani, wenyeji, wanajeshi na polisi wanaishi pamoja.

Hili lingekuwa jambo lisilowezekana miaka mitano tu iliyopita, kabla ya kufikiwa kwa makubaliano ya amani ambayo yalisaidia kukomesha mzozo kati ya Serikali ya Colombia na jeshi la mapinduzi la Colombia, linalojulikana kama FARC EP. 

Familia ya aina yake 

Pande zote zinajiona kuwa waathirika wa mzozo uliodumu kwa muda mrefu sana. “Sasa wao ni familia ya aina yake na familia moja ambayo imekuwa na heka heka zake, yenye majeraha ambayo yanahitaji uponyaji, lakini ambayo katika kesi hii, Umoja wa Mataifa unasaidia kupitia tiba ya upatanisho". 

Amani "imeleta manufaa mengi kwa wakulima, kwa jamii, na kwa nguvu ya umma. Hasa kwa familia ya Llano Grande. Tunatunzana, tunakutana, tunaona jinsi ya kusaidiana,” anasema mjumbe wa kikosi kidogo cha jeshi, kilichopo kando ya mlima ulioko katika mji wa Llano Grande, na ambaye hakupendelea kutaja jina lake. 
Mkazi  mwingine Luzmila Segura mwenye umri wa miaka 67,  amesema "Ndio, sasa sisi ni familia” ambaye anakumbuka kwamba wakati wa sherehe hiyo, aliamka asubuhi mapema asubuhi nyingi akiwa amejawa na hofu. 

“Unaona watu wenye silaha wakifika. Lo, inatisha sana! Mungu wangu! Tulidhani wamekuja kutuua,”

anakumbuka, akiongeza kwamba wapiganaji wa msituni wenye silaha walikuwa wakishambulia kijiji cha mlimani mara nyingi na hata kupora shamba lake ndogo na kuchoma kila kitu kilichoonekana.  
Alilazimika kuacha shamba lake na kukimbia kwenda kuishi katika kijiji cha jirani. 

Lakini tangu mkataba wa amani ulipotiwa saini, Bi. Segura anasema, akitabasamu: “Sasa ninajisikia furaha sana kwa sababu walinipa nyumba. Sasa hapa ni shwari sana. Sisi sote tunafanya kazi pamoja kama familia. Amani imekita na hadi sasa, kila kitu kinakwenda sawa. Wote kwa pamoja na tayari imeondoa hofu yangu.” 
Sasa anafanya kazi katika kiwanda kipya cha Arepas, kilichoanzishwa kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO). 

Kambi ya zamani ya waasi ya FARC Llano Grande huko Dabeiba, Colombia.
UNMVC/Esteban Vanegas
Kambi ya zamani ya waasi ya FARC Llano Grande huko Dabeiba, Colombia.

Sisi sote tunafanya kazi kwa ajili ya amani 

Carmen Tulia Cardona Tuberque, ambaye anaendesha kiwanda cha Arepas ambako Bi. Segura anafanya kazi, anapendelea kuzungumzia mambo ya sasa kwa sababu yaliyopita anasema ni uchungu sana. 
Akiepuka hadithi binafsi inayojumuisha mume aliyeuawa katika mzozo huo, ni jambo la kusikitisha lililowagusa wengi waliokaa Llano Grande, pamoja na wale waliokimbia. 
“Naamini hii ni jumuiya ambayo, pamoja na matatizo mengi ambayo imepitia, leo hii kila mmoja kwa pamoja tunafanya kazi kwa lengo moja, ambalo ni amani. Hujawahi kufikiria kuwa hii ingetokea, "amesema. 
Ameongeza kuwa “Jamii inachangia punje ya mchanga kwa wananchi. Sisi, hapa kama jamii, tunasaidiana, kwa sababu maelewano yanategemea sana hilo. Watu wengi waliolazimika kukimbia kutokana na machafuko hayo sasa wanarejea Llano Grande. Hilo ni jambo ambalo linakupa motisha sana." 
Vile vile, Jairo Puerta Peña, mpiganaji wa zamani ambaye alijiunga na FARC alipokuwa na umri wa miaka 14, karibu miaka 45 iliyopita, ambaye sasa anahudhuria kozi ya mafunzo ya ujenzi, anasema pia anahisi yeye ni sehemu ya familia ya Llano Grande. "Sote tuna malengo sawa, kuishi vizuri zaidi, kufanya kazi kwa amani na utulivu wa akili." 
Baada ya darasa lake la mafunzo ya asubuhi kumalizika, Bw. Peña ameeleza kwa kina jinsi maisha yake yavyobadilika katika miaka mitano iliyopita: “Maisha ya vita yalikuwa yakitembea sikuzote, kujua, kuzungumza na watu, kusoma na kutoa mafunzo kwa wanajeshi ili tusiuwawe wakati tunapokabiliwa na adui. Baada ya Makubaliano ya amani, maisha yamekuwa shwari. Kuna amani ya akili pia kuwa na familia, kulala, kula, kufanya kazi kwani milio ya risasi, mabomu na helikopta zinazopakia askari hazisikiki tena." 

Mpiganaji wa zamani akihaha kuwa na maisha ya kawaida. 

Rafiki wa Bw. Peña na mpiganaji mwenzake wa zamani, Efraím Zapata Jaramillo, ambaye alikuwa na umri wa miaka 21 alipoacha kazi yake ya ujenzi huko Medellín na kupanda mlima na FARC katika idara ya Caquetá, anaelezea jinsi alivyotoka kuwa mpiganaji milima akiwa na bunduki hadi anavyohaha kuunganishwa tena katika jamii na kuishi maisha ya kawaida kama Mcolombia mwingine yeyote. 

“Sisi sote hapa, waliokuwa wapiganaji, wasio wapiganaji, polisi na Jeshi, ni familia inayopigania amani isonge mbele na si kuchukua silaha tena. Neno liwe ndio silaha yetu na tunapaswa kuitumia sio tu kutetea haki zetu bali pia zile za watu wa Colombia. Hasa wakulima, ambao wametelekezwa na Serikali,” anasema, akiwa ameketi mbele ya cherehani anayotumia kushona mavazi ya jamii, kutokana na msaada wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). 

Aliyeketi karibu naye katika warsha ya ushonaji ni Monica Astrid Oquendo, mwanamke kijana mkulima ambaye makubaliano ya amani yameleta si tu amani ya akili, lakini fursa nyingi za kujifunza na kutoa mafunzo kwa njia ambazo zimefaidi jamii kwa kiasi kikubwa 

"Sisi ni kama familia kwa sababu tunashiriki mawazo, tunashiriki kazi," anasema. 

Akiwa na mkanda wa kupimia shingoni, Bi. Oquendo amefurahishwa na suti na fluna za polo alizoshona kwa mikono yake, na vifaa vya kuzuia upepo anavyojifunza kuunda kwa ajili ya kuuza katika jamii na kwingineko, ili kuwalinda waendesha pikipiki dhidi ya jua, mvua na baridi. 

Mwalimu wa kijiji anasaidia kujenga familia 

Ilipotangazwa kuwa wapiganaji 117 wa zamani wanahamishwa hadi Llano Grande kwa ajili ya kuunganishwa tena katika jamii, Mariela López, mwalimu katika shule ya mji huo, alihisi hofu, na kuwa na mashaka kuhusu kile alichofikiri ni bora kwa eneo la Llano Grande na Colombia kwa ujumla. 

“Siku ya kwanza nilipowaona tena, niliondoka. Nilienda mjini na kukaa huko, nilikaa chini na kulia. Nikasema, nitawezaje kuzungumzia amani ikiwa sijasamehe? Lakini nisiposamehe, basi anayeniudhi ni mimi. Na nikajiambia sitaki familia yoyote nchini Colombia iishi kama nilivyopitia, na kuanzia leo nitachangia chochote kitakachohitajika ili mchakato wa amani ufanyike na hivyo maridhiano yanaweza kupatikana Llano Grande,” alielezea. 

Baadaye, alipokutana na wapiganaji hao wa zamani, alibadilisha maoni yake juu yao: "Tulifikiri, na sio mimi tu, kwamba wapiganaji wa zamani walikuwa watu wenye fujo kwa sababu ya yale tuliyopitia, lakini walipofika, basi nilifikiri walikuwa watu wenye jeuri lakini kumbe sio wabaya sana na nitaomba msamaha kwa kile nitakachosema nadhani wengi wao pia ni waathirika." 

Mkulima na mwathirika wa migogoro Lucila akiwa amesimama nje ya nyumba yake ambayo ilijengwa upya baada ya mchakato wa amani nchini Colombia.
UNMVC/Esteban Vanegas
Mkulima na mwathirika wa migogoro Lucila akiwa amesimama nje ya nyumba yake ambayo ilijengwa upya baada ya mchakato wa amani nchini Colombia.

Umoja wa Mataifa unawashika mkono 

Kikiwa katika wilaya ya Antioquia, Llano Grande ni kijiji chenye wakazi 150. Pia ni kitovu cha mojawapo ya maeneo ya mafunzo na kujumuishwa tena katika jamii ambayo huwezesha kuunganishwa tena kwa wapiganaji wa zamani katika mashirika ya kiraia, huku kukiwa na manufaa kwa jumuiya zinazozunguka. 

Kiko kwenye mali ambayo ilinunuliwa na kukabidhiwa kwa wapiganaji wa zamani katika manispaa ya Dabeiba. 

Inakadiriwa kuwa huko Antioquia, asilimia 80 ya watu waliathiriwa katika vita vya silaha vya Colombia.  

Kihistoria, eneo hilo lilitumika kama ngome ya vikundi vingi vyenye silaha ambavyo viliimarishwa na uchumi haramu kama uchimbaji madini haramu na kilimo cha mazao haramu. 

Kama ambavyo wale wote ambao wamezungumza na UN News katika makala hii walivyoonyesha kwamba amani na familia vinajumuisha vipengele vingi: uaminifu, upatanisho, kuunganishwa tena, msamaha, na kufanya kazi kwa bidii. 

Tangu kutiwa saini kwa mkataba wa amani, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuthibitisha nchini Colombia, pamoja na mashirika na ofisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa, wamekuwa wakiandamana na familia ya Llano Grande katika safari yake, na hivyo kuwezesha kwa maneno yaliyo katika mapatano hayo kuota mizizi. 
Msaada huu umekuwa wa muhimu sana. 
Kwa Bw. Peña ni kwa sababu "imeizuiwa kwa Serikali ya Colombia kufanya chochote ilichotaka katika makubaliano hayo".

Kwa Bi. Segura, ni kwa sababu “jamii imenipa makao mapya”. 

Kwa Bi Cardona kwa sababu ameanza kazi katika kiwanda chake cha Arepas 

Kwa Bw. Zapata na Bi. Oquendo kwa sababu wanafanya maamuzi ya moja kwa moja kwenye karakana yao ya mavazi. 

Na kwa Bi. Lopez, kwa sababu ametoa programu za muziki, kompyuta, na madawati kwa ajili ya watoto katika shule yake. 

Pamoja na yote, kwa msaada wa Umoja wa Mataifa, baadhi ya miradi 15 imezinduliwa kuanzia utengenezaji wa sabuni hadi ufugaji wa samaki, elimu, ushonaji wa nguo, ufugaji na kilimo. 

Baadhi ya ahadi hazikutimizwa 

Lakini kama njia zenye kupindapinda zinazopita kwenye milima ya Llano Grande wenye misitu minene, yenye miti mingi, barabara ya kuelekea amani ina milima na mabonde mengi pia na inahitaji azma kufikia mahali panapotakiwa. 

Kwa hakika, Bw. Zapata Efraím na Bw. Peña wanaeleza kwamba "baadhi ya malengo ya makubaliano ya amani yametimizwa wakati mengine hayajakamilika".  

Wote wawili wamebainisha baadhi ya hatua muhimu bado hazijachukuliwa na Serikali katika maeneo ya makazi, ardhi na chakula. 

Wakati huo huo, miradi mingi huko Llano Grande imekwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha au ufuatiliaji wa kiufundi, na wakati mwingine, hata kutokana na ukosefu wa kujitolea kutoka kwa wapiganaji wa zamani.  

Zaidi ya hayo, tangu Aprili 2021, kumekuwa na ucheleweshaji unaoendelea na kupunguzwa kwa usambazaji wa chakula, na hivyo kusababisha machafuko na mashaka juu ya uendelevu wa muda mrefu wa juhudi za ujumuishaji na upatanisho katika ngazi ya ndani. 

Llano Grande na jumuiya kama hiyo zimepiga hatua kufuatia makubaliano ya amani, lakini katika maeneo mengine, bado kuna kazi kubwa ya kufanywa. 

Sio mbali sana na Llano Grande kuna manispaa ya Apartadó, ambapo Serikali itafanya sherehe ya kuadhimisha miaka mitano tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani, ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atahudhuria. 

Huko, ofisi ya meya imeanza ujenzi wa "barabara kuu kuu ya kuunganisha maeneo ya vijijini walipo wapiganaji wa zamani na jiji", lakini kwa sasa, hakuna rasilimali za kumaliza mradi huo. 

Nao baadhi ya wajumbe wa manispaa hiyo wametahadharisha kuwa pamoja na kwamba hakuna mgogoro kati ya wapiganaji wa zamani, raia, wanajeshi na askari wengine, lakini hakuna maridhiano pia badala yake, “kila mmoja hufanya mambo yake mwenyewe bila kuhangaika na mwenzake,” UN News iliambiwa. 

TAGS: Colombia, mkataba wa amani, Llano Grande