Ndugu watatu wameketi ndani ya nyumba yao katika kambi ya wakimbizi wa ndani nje kidogo ya mji wa magharibi wa Herat, Afghanistan.

Katika hatihati ya zahma ya kibinadamu, watoto wapoteza utoto wao Afghanistan

© UNICEF/Siegfried Modola
Ndugu watatu wameketi ndani ya nyumba yao katika kambi ya wakimbizi wa ndani nje kidogo ya mji wa magharibi wa Herat, Afghanistan.

Katika hatihati ya zahma ya kibinadamu, watoto wapoteza utoto wao Afghanistan

Haki za binadamu

Kwa zaidi ya miaka 70, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) limekuwepo kote nchini Afghanistan hata wakati huu ambapo Taliban imetwaa mamlaka wakati wa majira ya joto. 

 

UN News imezungumza na Samantha Mort, mkuu wa mawasiliano, utetezi na ushirikiano wa kiraia katika shirika la UNICEF nchini Afghanistan, ambaye amehakikisha kuwa ofisi zote za shirika hilo zimesalia wazi ikiwa ni pamoja na ghala za kuhifadhia bidhaa. 

Takriban watu milioni 22.8 kote nchini Afghanistan wanakabiliwa na uhaba wa chakula, ameelezea afisa huyo, akiongeza kuwa hawawezi kupata chakula cha bei nafuu au chenye lishe.

Kati ya watu milioni 38 wanaoishi Afghanistan, watoto milioni 14 hawana uhakika  wa chakula.

Kwa Bi. Mort, "utoto wao umeporwa siku hizi nchini Afghanistan. Kilichosalia ni kubambanya kuweza kuishi, kumaliza siku na kuiona siku ya kesho." 

Janga kubwa 

Afisa huyo ameelezea taswira mbaya ya familia maskini ambazo wazazi wao hawali milo mitatu kwa siku, mlo unapungua na watu huamka bila kujua mlo unaofuata unatoka wapi. 

"Ni kiwango hicho cha uhaba wa chakula kutokana na ukame uliokithiri, mavuno duni na kupanda kwa bei ya vyakula, na hii ni dhoruba kubwa nchini Afghanistan". 

Na ukiwa ni mwanzo wa majira ya baridi kali kwa kawaida, Bi. Mort amesema kuwa theluji itakata mawasiliano ya maeneo ya mashambani kwenye milima.

Hivyo  ameonya kuwa "UNICEF ina wasiwasi sana kwa sababu tunachokiona ni karibu watoto milioni 3.2 ambao wana utapiamlo wa hali ya juu na watoto milioni 1.1 ambao wako katika hatari ya kufa kwa sababu ya utapiamlo mkali na unyafuzi kama hatutaingilia kati kwa matibabu". 

Fatima mwenye umri wa miaka miwili anapimwa hali yake ya lishe katika kituo cha afya cha Bab-e-Bargh ambacho kinasaidiwa na UNICEF katika kliniki kubwa zaidi ya afya ya mji wa Herat.
© UNICEF/Sayed Bidel
Fatima mwenye umri wa miaka miwili anapimwa hali yake ya lishe katika kituo cha afya cha Bab-e-Bargh ambacho kinasaidiwa na UNICEF katika kliniki kubwa zaidi ya afya ya mji wa Herat.

Kumbukumbu za hospitali 

Wiki iliyopita, afisa huyo wa UNICEF alitembelea kliniki za afya katika eneo la Magharibi mwa nchi. 
Katika hatua ya kwanza, daktari alimuonesha kumbukumbu zilizoonesha ongezeko la asilimia 50 ya visa vya utapiamlo mkali huku mwingine akifichua ongezeko la asilimia 30. 

Licha ya ongezeko hilo, Bi. Morte amesema mgogoro huo haukuanza tarehe 15 Agosti bali nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na aina fulani ya ukosefu wa uhakika wa chakula au migogoro kwa miaka 40 iliyopita. 

"Lakini kutokana na ukame, mavuno duni, na kupanda kwa bei ya vyakula, kwa sababu wanawake wengi wametakiwa kukaa nyumbani tangu Agosti 15, familia nyingi zimepoteza chanzo chao kikuu cha mapato", amesema. 

Hadithi za familia 

Bi. Mort amekiri kwamba alimuuliza mama wa mtoto aliye na utapiamlo wa kupindukia iwapo alikuwa akinyonyesha na akaambiwa kuwa licha ya kujaribu, hakuwa na maziwa ya kumnyonyesha mwanaye.  

Daktari aliyekuwa katika chumba hicho alimuuliza mama huyoendapo alikuwa anakula.  

Mwanamke huyo alijibu kwamba siku nyingi, alikunywa tu glasi ya chai nyeusi na kipande cha mkate peke yake. 

“Si ajabu kwamba hawezi kunyonyesha kwa sababu yeye mwenyewe ana utapiamlo. Na nadhani hiyo ni hadithi ambayo imeenea kote nchini”, afisa huyo wa UNICEF ameongeza. 

Mama huyohuyo kisha akamleta mtoto wake mwenye umri wa miaka 4, akiwa amevaa koti kubwa kupita kiasi. 

"Ungetarajia mtoto wa miaka 4 kuwa akitazama huku na huko na kuwa na hamu ya kujua kuhusu wageni katika chumba hicho. Msichana huyu mdogo aliketi akisaidiwa na koti lake kubwa  katika nafasi ile ile ambayo mama yake alikuwa amemweka chini. Nsa alikuwa akitazama tu sakafuni. Kichwa chake kilikuwa kimeinamishwa. Hakuwa na nguvu alionekana mnyonge sana”, Anakumbuka Bi Mort. 

Ameongeza kuwa baada ya kumvua koti msichana huyo “Mikono yake ilikuwa mwembamba kama ufagio na alikuwa na utapiamlo mbaya ambapo nywele zake zilikuwa zikitoka na ana mashimo makubwa kwenye mashavu yake. Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 4 alikuwa na uzito wa puan 20 tu. Unyafuzi wa kiwango hili unamaanisha kwamba unaweza kufa endapo hautapatiwa matibabu na inamaanisha kwamba endapo hatutawapa matibabu watakufa.” Amesisitiza Bi. Mort 

Juhudi maradufu  

Kwa sababu ya ukame na matokeo duni ya mavuno, UNICEF inatabiri kuwa akiba ya chakula itaisha katikati ya msimu wa baridi.

Shirika hilo linaongeza mara dufu idadi yake ya washauri wa lishe na timu za afya na lishe zinazotembea sehemu moja hadi nyingine ambazo zinaweza kwenda katika jamii za vijijini kusaidia watoto ambao ni vigumu zaidi kuwafikia. 

Bi. Mort amesisitiza kwamba washauri wa lishe mara nyingi huajiriwa mashinani ili jamii ziwaamini. 
"Wana shauku sana, wenye nguvu na wanainua jamii", ameelezea akiashiria mwingiliano mzuri kati yao na akina mama wanaokuja kwa ajili ya kupata msaada. 

"Wanakuja na suluhisho za ubunifu. Wanatumia kile kilicho katika jamii. Wanagawana rasilimali,” alielezea. 
Wataalamu hawa kwa kawaida pia ni wanawake wadogo, waliosoma. Bi Mort anakumbuka kukutana na daktari wa kike katika miaka yake ya mapema ya 30 ambaye alikuwa akiendesha kliniki ya matibabu na wafanyikazi 20, na 18 kati yao wakiwa ni wanawake. 

Daktari alisema "Inatia moyo sana sana kuona wanawake wadogo wenye taaluma wakifanya kazi nchini Afghanistan katikati ya changamoto zote zilizopo", amekumbusha kwamba "hawangeacha kuzungumza kuhusu kazi zao, na kuhusu wagonjwa wao". 

Parwana anaugua Utapiamlo mkali, mahitaji ya lishe ya watoto pia yameongezeka kufuatia matukio ya hivi karibuni huku kudorora kiuchumi ukichangia watu wengi zaidi nchini Afghanistan kuwa katika hali mbaya.
© UNICEF
Parwana anaugua Utapiamlo mkali, mahitaji ya lishe ya watoto pia yameongezeka kufuatia matukio ya hivi karibuni huku kudorora kiuchumi ukichangia watu wengi zaidi nchini Afghanistan kuwa katika hali mbaya.

Parwana anaugua utapiamlo wa kupindukia au unyafuzi ambapo mahitaji ya lishe ya watoto pia yameongezeka kufuatia matukio ya hivi majuzi, huku changamoto ya kiuchumi ikitumbukiza watu wengi zaidi nchini Afghanistan kwenye mgogoro. 

Mustakbali usio na uhakika 

Katika ziara zake zote, Bi. Mort ameshuhudia zaidi hisia za kutokuwa na uhakika na matumaini. 

"Nadhani watu hawana uhakika, hawajui msimu wa baridi una nini, mamlaka ya iliyoko sasa watafanya nini baadaye. Hawajui kama jumuiya ya kimataifa itatoa fedha hizi zinazohitajika ili mfumo wa afya na mfumo wa elimu upate nafuu. Wanahisi kama kila mtu yuko katika hali ya kushikilia kidogo, "amesema Mort. 

Kwa afisa huyo wa UNICEF, "ni muhimu sana kwamnba jumuiya ya kimataifa inaelewa kuwa Afghanistan iko ukingoni mwa mgogoro mkubwa wa kibinadamu. Huu si wakati wa kuwa na mawazo ya kisiasa. Watu nchini Afghanistan wanakufa, na wanahitaji msaada wetu. Misaada ya kibinadamu ni kielelezo cha mwisho cha mshikamano wa kibinadamu,” alisema. 
 
Ameongeza kuwa "Wakati huna kitu unatatizika jisikie umesahauliwa na sijui mlo wako unaofuata unatoka wapi, misaada ya kibinadamu inafika mlangoni pako na wewe ni sehemu ya familia kubwa zaidi". 

Mgogoro katika sekta ya afya  

Bi. Mort anakumbuka mazungumzo aliyokuwa nayo wiki iliyopita na mkurugenzi wa hospitali ya watoto ya Indira Gandhi huko Kabul ambaye alimwambia kwamba wakati mwingine analaza watoto watatu katika kitanda kimoja, kwa sababu kliniki nyingi za wilaya na mkoa haziwezi tena kufanya kazi. 

Zaidi ya hayo, watu wanaoishi vijijini wanapaswa kuwapeleka watoto wao katika mji mkuu.  

Lakini kwa sababu umaskini unazuia uwezo wao wa kusafiri, wanangoja mda mrefu hadi wapate fedha na hilo linafanya watoto wao kuwa wameugua sana na kwa muda mrefu. 

“Wamechelewa. Na Watoto wanakufa kwa sababu familia hazikuwa na pesa za kuwaleta mapema hospitali. Tunaona jinsi familia zinavyozidi kukata tamaa”.

UNICEF imebainiongezeko la "utaratibu mbya wa kukabiliana na hali hii, ambapo watu wanakata tamaa kiasi kwamba wanaanza kufanya mambo ambayo hawangefikiria kwa kawaida, kama vile kumtoa mtoto shuleni au kumuuza kwa ndoa za mapema wakati mwingine watoto wachanga wenye umri wa miezi sita”. 

 Mkuu wa mawasiliano wa UNICEF Afghanistan, Sam Mort, akiwasiliana na mtoto katika wodi ya matibabu ya utapiamlo katika Hospitali ya Watoto ya Indira Gandhi huko Kabul.
© UNICEF/Omid Fazel
Mkuu wa mawasiliano wa UNICEF Afghanistan, Sam Mort, akiwasiliana na mtoto katika wodi ya matibabu ya utapiamlo katika Hospitali ya Watoto ya Indira Gandhi huko Kabul.

Elimu kwa wasichana 

Kwa sasa, Bi. Mort anasema wasichana vigori bado hawajaalikwa kurejea shuleni. 

"Tuna wasichana wapatao milioni moja wa umri wa kwenda shule ya upili wanaokaa nyumbani, wamenyimwa haki yao ya kupata elimu. Tunataka kuona kila mtoto yuko shuleni. Ikiwa watoto hawako shuleni, wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuandikishwa kwenye makundi yenye silaha, au kuangukia kwenye ndoa za mapema au kunyanyaswa kwa namna fulani”. 

Hata kabla ya utawala wa sasa wa Taliban, asilimia 70 ya uchumi wa Afghanistan uliimarishwa na misaada ya kimataifa. 

"Kwa msaada huo, wafanyikazi wa afya na walimu hawalipwi. Ukifikiria nchi ambayo haina mfumo wa elimu unaofanya kazi na haina mfumo wa afya unaofanya kazi, utaelewa jinsi maisha yote yanavyoporomoka”, ameelezea Mort. 

Wiki iliyopita katika shule mpya, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alizungumza na darasa la wasichana ambao hawakuwahi kupata elimu. 

Alipouliza kama walikuwa na ujumbe wa kushiriki na ulimwengu, mtoto wa miaka saba aliinua mkono wake juu na kuuliza ikiwa ulimwengu unaweza kuweka amani nchini Afghanistan ili aendelee kwenda shule.

“Niliwaza tu, Mungu anmpenda. Alisema tu kutoka moyonikwamba hebu hakikisha amani nchini mwangu ili niendelee kusoma”, anakumbuka Bi. Mort