Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya hatari iliyotangazwa Ethiopia inatumika vibaya: UN

Wananchi wa Ethiopia, wakikimbia mapigano katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo, wanavuka mpaka na kuingia Hamdayet, nchini Sudan
© UNHCR/Hazim Elhag
Wananchi wa Ethiopia, wakikimbia mapigano katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo, wanavuka mpaka na kuingia Hamdayet, nchini Sudan

Hali ya hatari iliyotangazwa Ethiopia inatumika vibaya: UN

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za bindamu, OHCHR, imeelezea wasiwasi wake kufuatia vitendo vya ukamataji wa watu vilivyofanyika wiki iliyopita katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, na pia katika maeneo ya Gondar, Bahir Dar na mengineyo, huku polisi wakitumia vifungu vingi vya hali ya hatari iliyotangazwa tarehe 2 Novemba,2021 ili kukamata, kuwatafuta na kuwaweka kizuizini.

Akizungumza na waandishi wa mjini Geneva, Uswisi msemaji wa OHCHR Liz Throssell amesema matukio haya yanatia wasiwasi zaidi ikizingatiwa kwamba wengi wa wale wanaozuiliwa wanaripotiwa kuwa watu wa asili ya Tigrayan ambao wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara kwa tuhuma za kuhusishwa au kuunga mkono Kikosi cha Ukombozi cha Watu wa Tigray -TPLF.

“Ripoti tulizonazo zinaonesha takriban watu 1,000 wanaaminika kuzuiliwa kwa wiki moja sasa au zaidi, ripoti zingine zinaonesha idadi ya juu zaidi. Hali za kizuizini kwa ujumla zinaripotiwa kuwa mbaya, huku wafungwa wengi wakizuiliwa katika vituo vya polisi vilivyojaa watu, kinyume na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.” Amesema Bi. Throssell.

OHCHR imetoa wito kwa Ethiopia kufuata kwa haki za binadamu kikamilifu ikiwemo haki ya dhamana kwakuwa ripoti walizopokea zinaonesha watu wengi waliokamatwa hawajafunguliwa mashtaka wala kufikishwa mahakamani na kuna wasiwasi wanatendewa vitendo vibaya wakiwa vizuizini. 

Hali ya Hatari inatumika vibaya

Msemaji huyo wa Ofisi ya haki za Binadamu amesema hali ya hatari inayoendelea nchini Ethiopia inaweza kuzidisha hali mbaya ya masuala ya kibinadamu kwakuwa masharti yaliyowekwa ni mapana mno na makatazo mapana yasiyoeleweka ambayo yanaenda mbali zaidi na kugusia mpaka uungaji mkono wa kimaadili usio moja kwa moja kwa kile ambacho serikali imekiita "makundi ya kigaidi".

Throsell amesema “pamoja na uwepo wa hali ya hatari lakini kuna haki fulani za watu haziwezi kudharauliwa hata katika hali ya hatari, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kutoteswa, kutendewa vitendo vya kinyama au kudhalilishwa au kuadhibiwa, haki ya kuishi na haki ya usawa na kutobaguliwa.”

Sheria za kimataifa zinasema kuweka mtu kizuizini kunatakiwa kukomeshwa mara tu mtu huyo atakapoacha kuwa tishio na uwekaji wa mtu kizuizini unapaswa kutumika kwa njia isiyo ya kibaguzi lakini hali iliyopo sasa ya kukamatwa na kuzuiliwa watu nchini Ethiopia chini ya mamlaka ya hali ya hatari hakuheshimu masharti haya. 

Wafanyakazi wa UN

Mpaka sasa wafanyakazi 10 wa Umoja wa Mataifa raia wa nchi hiyo wanashikiliwa pamoja na madereva 34 waliokuwa katika kandarasi ndogo za Umoja wa Mataifa. 

OHCHR imetoa wito kwa walio vizuizini waachiliwe huru mara moja ama wafikishwe mahakamani katika mahakama huru ili washtakiwe.