Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya waandamanaji Sudan ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu:Bachelet

Waandamanaji wameingia mitaani katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum tarehe 11 Aprili 2019,
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji wameingia mitaani katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum tarehe 11 Aprili 2019,

Mauaji ya waandamanaji Sudan ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu:Bachelet

Haki za binadamu

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet leo amelaani vikali mauaji ya watu 39 nchini Sudan yaliyofanywa na vikosi vya ulinzi tangu kufanyika mapinduzi ya kijeshi nchini humo tarehe 25 Oktoba mwaka huu. 

 Watu 15 kati yao wamearifiwa kupigwa risasi jana Jumatano pekee wakati wa maandamano yaliyofanyika mjini Khartoum, Khartoum-Bahri na Omdurman.

Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswisi Bi. Bachelet amesema "Kufuatia wito wetu wa mara kwa mara kwa jeshi na mamlaka za usalama kuacha kutumia nguvu zisizo za lazima na zisizo na uwiano dhidi ya waandamanaji, ni aibu sana na jambo la kusikitisha kwamba risasi za moto zimetumika tena jana dhidi ya waandamanaji. Ufyatuaji risasi kwenye umati mkubwa wa waandamanaji wasio na silaha, na kuacha watu kadhaa wakiwa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa, ni jambo la kusikitisha, ambalo linalenga kuzima sauti ya upinzani wa umma, na huo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu." 

Kwa mujibu wa duru za huduma za matibabu, zaidi ya watu 100 walijeruhiwa wakati wa maandamano ya jana na 80 kati yao walipata majeraha ya risasi kwenye miili yao sehemu ya juu na vichwani.

Pia kulikuwa na matumizi makubwa ya mabomu ya machozi. Shughuli za kamatakamata ziliripotiwa kuwa tayari zilifanyika kabla, pamoja na wakati na baada ya maandamano.  

Polisi wametoa taarifa wakisema maafisa 89 wa polisi pia wamejeruhiwa katika purukushani hiyo. 

Kukatwa kwa mawasiliano.

Kamishina Mkuu ameongeza kuwa "Kuzimwa kwa mawasiliano kunamaanisha kuwa watu hawawezi kupiga simu kwa huduma za magari ya kubeba wagonjwa ili kuwatibu waandamanaji waliojeruhiwa, familia haziwezi kuangalia usalama wa wapendwa wao, na hospitali haziwezi kufikia madaktari kwani vyumba vya dharura vimejaa, nikitaja machache tu ya hali halisi na madhara makubwa. Kuzimwa kwa mtandao na mawasiliano kwa ujumla ni kukiuka kanuni za msingi za umuhimu wa haja ya mawasiliano na ni kukiuka sheria za kimataifa." 

Tangu kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi , waandishi wa Habari hususan wale wanaoshukuliwa kuikosoa mamlaka wamekuwa wakilengwa imesema ofisi ya haki za binadamu.

Vikosi vya UNAMID vikiwa katika doria Darfur
UNAMID/Hamid Abdulsalam
Vikosi vya UNAMID vikiwa katika doria Darfur

Waandishi wa habari

Waandishi Habari wamekuwa wakikamatwa, kushambuliwa wakati wakiripoti na pia nyumba na ofisi zao kupekuliwa na vikosi vya ulinzi na usalama. 

Pia kumekuwa na taarifa za kuhuzunisha amesema Bachelet za majaribio ya kuwateka waandishi wa Habari na maafisa wa jeshi waliovalia nguo za kiraia. 

Kamishina mkuu amesisitiza kwamba "Pamoja na kuzimwa kwa mtandao, jukumu la waandishi wa habari katika kupata habari kuhusu hali ya sasa ni muhimu sana, lakini ninahofia kwamba mazingira yanayozidi kuongezek ya chuki dhidi yao yanaweza kusababisha waandishi kujidhibiti, vyombo vingi kushindwa kufanyakazi na hivyo kutishia zaidi uhuru wa vyombo vya Habari. Ninaziomba mamlaka kuwaachilia mara moja wale wote ambao wamezuiliwa kwa kutumia haki zao za uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, pamoja na wahusika wote wa kisiasa waliowekwa kizuizini kama walivyoahidi kufanya hivyo hadharani." 

Mwanamke mzee, mkimbizi wa ndani kutoka nyumbani kwake huko Abyei nchini Sudan, anajiandaa kupokea mgawo wake wa msaada wa dharura wa chakula.
UN Photo/Tim McKulka
Mwanamke mzee, mkimbizi wa ndani kutoka nyumbani kwake huko Abyei nchini Sudan, anajiandaa kupokea mgawo wake wa msaada wa dharura wa chakula.

Kuwajibishwa

Bachelet amesisitiza kuwa wajumbe wa vikosi vya usalama pamoja na viongozi wa kisiasa na kijeshi wanaohusika na matumizi ya nguvu kupita kiasi na yasiyo na uwiano dhidi ya waandamanaji lazima wawajibishwe kwa kuzingatia sheria na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Kamishna Mkuu pia amehimiza haja ya kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya hawalengwi kwa kutoa huduma za matibabu kwa waandamanaji waliojeruhiwa, na kuhakikisha kwamba kazi yao muhimu haitatizwi.