Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto watatu wauawa nchini Sudan: UNICEF

Waandamanaji wakikusanyika mbele ya Makao Makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum (11 April 2019)
Masarib/Ahmed Bahhar
Waandamanaji wakikusanyika mbele ya Makao Makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum (11 April 2019)

Watoto watatu wauawa nchini Sudan: UNICEF

Amani na Usalama

Watoto watatu, msichana wa miaka 14 na wavulana wawili wenye umri wa miaka 15 na 17 wameripotiwa kuuawa wakati wa vurugu karibu na maandamano katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa shirika hilo Ted Chaiban, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za Watoto na kueleza mpaka sasa bado mazingira halisi ya vifo vyao hayajathibitishwa.

“Matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ya amani hayakubaliki na yana athari kubwa kwa watoto na vijana.” Amesema Chaiban na kuongeza kuwa "Watoto lazima walindwe wakati wote dhidi ya aina zote za unyanyasaji na madhara. Kamwe wasiwe walengwa, wanyonywaji au kutumiwa kama vyombo vya siasa.”

UNICEF imetoa wito kwa pande zote zinazohusika kuwalinda watoto wakati wote wafanye hivyo na kuwaepusha na madhara.

“Watoto wa Sudan wanastahili kutimiza matarajio yao ya mustakabali wa amani, ustawi na demokrasia". Amesema Mkurugenzi huyo wa kanda wa UNICEF.