Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Moto waua watoto wakiwa shuleni nchini Niger

Watoto wakimbizi wakichota maji katika eneo la Maradi Niger.
© UNICEF/Juan Haro
Watoto wakimbizi wakichota maji katika eneo la Maradi Niger.

Moto waua watoto wakiwa shuleni nchini Niger

Amani na Usalama

Watoto kadhaa wamekufa baada ya moto kuteketeza shule ya msingi katika mji wa Maradi nchini Niger limeeleza shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF nchini humo. 

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Iliyotolewa usiku wa tarehe 08 Novemba na mwakilishi wa UNICEF nchini humo Stefano Savi akiwa katika mkoa wa Niamey imesema “UNICEF imepata taarifa za awali zinazoonesha kuwa watoto kadhaa waliuawa au kujeruhiwa katika moto huo.”

Savi ametuma salama za rambirambi na pole kwa familia za watoto hao na kueleza "Mioyo yetu iko pamoja na watoto na familia zilizoathiriwa. Rambirambi zetu za dhati kwa familia za wahasiriwa na jamii zao.”

Ameeleza hakuna mtoto anayepaswa kuwa hatarini wakati anajifunza shuleni na kwamba UNICEF itaendelea kushirikiana na mamlaka ya kitaifa na washirika yote nchini humo ili kuhakikisha watoto wanaweza kuhudhuria shule na kujifunza katika mazingira salama.

UNICEF inafanya kazi katika nchi na maeneo190 yenye hali ngumu na mbaya zaidi duniani, ili kuwafikia watoto wasiojiweza zaidi duniani lengo likiwa ni kuhakikisha wanajenga ulimwengu bora kwa kila mtu.