Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanne wauawa wakati wakienda shule nchini Syria

Mtoto wa kike na mwanamke wakitembea kupita majengo yaliyoharibiwa katika jiji la Maarat al-Numaan huko Idlib, Syria.
©UNICEF/Giovanni Diffidenti
Mtoto wa kike na mwanamke wakitembea kupita majengo yaliyoharibiwa katika jiji la Maarat al-Numaan huko Idlib, Syria.

Watoto wanne wauawa wakati wakienda shule nchini Syria

Amani na Usalama

Watoto wanne, kati yao wavulana watatu na msichana mmoja pamoja na mwalimu wamethibitishwa kuuawa hii leo wakati wakiwa njiani kuelekea shuleni kwenye shambulio lililotokea katika soko la Ariha kaskazini magharibi mwa Syria.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ted Chaiban ambaye ni Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto - UNICEF imesema mashambulizi dhidi ya raia ikiwemo watoto ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Chaiban ameongeza kuwa “mapema asubuhi ya leo, basi lilishambuliwa katika mji mkuu wa Damascus Wakati shambulio hilo lilitokea kwenye barabara iliyojaa watu, UNICEF haiwezi kuthibitisha ikiwa watoto walikuwa miongoni mwa walioathiriwa. Vurugu za leo bado ni ukumbusho mwingine kwamba vita nchini Syria havijamalizika. Raia, kati yao watoto wengi, wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa mzozo mbaya wa miaka kumi.”

UNICEF wamekumbusha kuwa watoto wanapaswa kuwa na uwezo wa kufika shuleni salama na wamerudia kutoa wito kwa wale wanaopigana kuacha kuwalenga watoto na badala yake wanapaswa kulindwa wakati wowote hususan wakati wa mizozo.

UNICEF inafanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo magumu zaidi ulimwenguni, kuwafikia watoto wanaoishi katika maeneo duni zaidi ulimwenguni ili kujenga ulimwengu bora kwa kila mtu.