Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ng’ombe mmoja aleta hakikisho la maisha kwa kaya maskini Burundi

Maza, ng'ombe ambaye amebadili maisha ya familia maskini nchini Burundi
@UNICEFBurundi/2021/Hamburger
Maza, ng'ombe ambaye amebadili maisha ya familia maskini nchini Burundi

Ng’ombe mmoja aleta hakikisho la maisha kwa kaya maskini Burundi

Ukuaji wa Kiuchumi

Mtamba mmoja wa ng’ombe anaweza kuonekana si chochote kitu kwa wafugaji wabobezi lakini kwa Beatrice Nibogora na familia yake nchini Burundi, mtamba huyo akipatiwa jina Maza amegeuka lulu na ufunguo wa maisha yenye matumaini na kutimiza methali ya wahenga ya kwamba baada ya dhiki ni faraja. Hii ni baada ya mradi wa Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kubisha hodi kunusuru kaya maskini.

Béatrice mwenye umri wa miaka 23 mke wa Sylvestre Habiyaremye na mama wa mtoto Chianique mwenye umri wa miaka mitatu.

Familia hii ina eneo dogo la ardhi kutoka kwa wazazi wa Sylvestre, lakini haina mifugo katika taifa ambalo kumiliki mifugo kama ng’ombe ni heshima kubwa. Mlo wao kwa siku ulikuwa ni mmoja.
Siku moja, mradi wa Merankabandi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Burundi, ukabisha hodi nyumbani kwake kumuokoa yeye na familia  yake.

Katika kipindi cha miaka mitatu, mradi umepatia kaya maskini 56,000 ikiwemo ya Beatrice migao 15 ya fedha taslimu ikiwa ni jumla yad ola 20 pamoja na mafunzo ya malezi ya watoto, afya ya mama na mtoto na usimamizi wa fedha,

Kupitia simu yake ya kiganjani, Beatrice alipokea mara kwa mara fedha kidogo za kujikimu. Kwa kiasi hicho kidogo cha fedha, mavuno yalianza kuongezeka. Akanunua nguruwe huku akiweka akidunduliza fedha zake.

Beatrice akiwa na ndama wa Maza kwenye shamba la familia yao.
UNICEFBurundi/2021/Ruben Hamburger
Beatrice akiwa na ndama wa Maza kwenye shamba la familia yao.

Na ndipo siku moja, alifanikiwa kumnunua Maza ambaye alizaa ndama na kisha kuanza kuwapatia maziwa. “Tunamkamua Maza maziwa kila siku Maza si ng’ombe wa kisasa kwa hiyo anatupatia lita mbili na nusu za maziwa kila siku. Si kiasi kingi lakini si haba,” anasema Beatrice.

Maziwa hayo ya ng’ombe ni lishe bora kwa mwanae Beatrice, Chanique ambaye sasa kila siku hupatiwa kikombe kimoja cha maziwa. Kiasi kingine cha maziwa, Beatrice anatengeneza jibini.
 Samadi kutoka kwa Maza ikawa mbolea shambani ambako amepanda mahindi, mtama na maharagwe, rutuba ikaongezeka sambamba na mavuno.

Njaa imetoweka kwenye familia yao, huku akiajiri kijana Jean-Marie kijijini kwao kumsaidia kukata majani ya ng’ombe.

Maza amegeuza maisha kuwa rahisi na shuku za awali zimetoweka na nuru imeonekana ambapo Sylvestre anasema, “kabla ya mradi wa Merankabandi, nilikuwa nina hofu kubwa. Sikuweza kuona jawabu la maisha yetu na sikufahamu maisha yetu ya baadaye yatakuwa vipi. Lakini sasa naona kesho yetu! Mtoto wangu anaweza kwenda shule na akapata elimu. Atakuwa na uwezo wa kutunza wapendwa wake. Atakuwa na maisha bora. Leo naweza kuona mustakabali wetu. Mustakabali wetu ni wa uhakika.”