Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kusuasua kwa chanjo ya COVID-19 kwakwamisha ukuaji uchumi Afrika kusini mwa Sahara

Muhudumu wa afya akiandaa chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini Moghadishu Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Muhudumu wa afya akiandaa chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini Moghadishu Somalia

Kusuasua kwa chanjo ya COVID-19 kwakwamisha ukuaji uchumi Afrika kusini mwa Sahara

Ukuaji wa Kiuchumi

Uchumi wa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara unatarajiwa kuimarika mwaka huu 2021 baada ya kuporomoka mwaka uliotangulia wa 2020 kutokana na janga la ugonjwa Corona au COVID-19.
 

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya mtazamo wa uchumi katika ukanda huo, ripoti iliyotolewa leo jijini Washington DC nchini Marekani na shirika la fedha duniani, IMF ikisema kuwa uchumi utakua kwa asilimia 3.7 mwaka huu wa 2021 na asilimia 3.8 mwaka ujao wa 2022.
IMF inasema inakaribisha kwa dhati ukuaji huo unaochochewa na mazingira bora ya uchumi nje ya ukanda huo ikiwemo ongezeko kubwa la biashara na bei za bidhaa.

Mkuu wa Idara ya Afrika katika IMF Abebe Aemro Sellasie akizungumzia makadirio hayo amesema “ukuaji unatokana pia na kuimarika kwa mavuno na ongezeko la uzalishaji katika sekta ya kilimo kwenye nchi kadhaa.”

IMF inasema ukanda huo wa Afrika uko katika mwelekeo tofauti usio wa kuridhisha katika kujikwamua ikilinganishwa na maeneo mengine, na kwamba tofauti hiyo kimataifa ambayo inatarajiwa kuwepo kwa muda, imechangiwa na kasi ndogo ya bara hilo katika kuendesha kampeni za chanjo dhidi ya Corona.

Mfanyabiashara mtaa akiuza chai na kahawa kupitia kwenye baiskeli yake mjini Abijan, Cote d'Ivoire katika kipindi cha janga la COVID-19
ILO/Jennifer A. Patterson
Mfanyabiashara mtaa akiuza chai na kahawa kupitia kwenye baiskeli yake mjini Abijan, Cote d'Ivoire katika kipindi cha janga la COVID-19

“Nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimekumbwa na awamu ya tatu ya janga la Corona, na wakati huu virusi ni vikali zaidi vile vya aina ya Delta, ambapo maambukizi yanaongeza zaidi ya mara tatu au mara nne ikilinganishwa na awali. Tunashukuru kuwa kasi ya maambukizi imepungua katika miezi iliyopita, lakini hatuna uhakika wa kuamini kuwa hakutawekupo na wimbi lingine siku za usoni,” amesema Bwana Selassie.

Kasi ndogo ya chanjo katika nchi nyingi za Afrika imesababishwa na mambo kadhaa ikiwemo ukosefu wa chanjo utokanao na baadhi ya nchi kuhodhi kiwango kikubwa cha chanjo huku nyingine zikiwa hazina kabisa. Halikadhalika baadhi ya nchi kuweka vikwazo kwa kampuni za chanjo kutouza nje ya nchi  chanjo hizo za Corona na wengine wakisaka chanjo ya tatu, hali inayoweza kukwamisha usambazaji wa chanjo kwa nchi ambazo bado hazijafikia wananchi wake wote.

IMF imeonya kuwa ukwamukaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara bado uko tete na unategemea pia mtazamo wa uchumi wa dunia ikiwemo mazingira magumu ya kifedha duniani.

Hivyo Bwana Selassie anasema, “watunga sera katika ukanda huo wanahitaji kupitisha sera ngumu wakati huu ambapo ukuaji wa uchumi  ni mdogo kuliko matarajio. Mathalani matumizi yoyote ya lazima lazima yashughulikie changamoto za kijamii na kibinadamu zilizopo, kudhibiti ukopaji wa fedha kwa kuzingatia kuwa deni ni kubwa katika nchi nyingi na zaidi ya yote kuhamasisha ukusanyaji wa mapato.”

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mambo hayo matatu ndio utaamua mwelekeo na ustawi wa nchi hizo ambazo sasa ziko njiapanda.