Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Programu ya Mastercard yatimiza ndoto ya mkimbizi kusoma Chuo Kikuu

Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.
© UNICEF/Jimmy Adriko
Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.

Programu ya Mastercard yatimiza ndoto ya mkimbizi kusoma Chuo Kikuu

Utamaduni na Elimu

Binti Raba Hakim, msomi mkimbizi kutoka Sudan aliyekulia katika kambi ya wakimbizi nchini Ethiopia hatimaye ndoto yake ya kujiunga na chuo kikuu imetimia baada ya kuanza masomo ya Saikolojia katika Chuo Kikuu nchini Kenya chini ya ufadhili wa wakfu wa Mastercard.

‘’Nilikotokea wasichana hawapati elimu kama wavulana, kama binti ukienda shuleni akili yako inahama kutoka kwenye masomo kwenda kwenye majukumu ya nyumbani “. Ndivyo anavyosema Binti Raba Hakim msomi wa Chuo Kikuu nchini Kenya akikumbuka maisha ya kambini huko Ethiopia. 
 
“Mimi ndio nilipata fursa ya kuendelea na darasa la 11, mimi pekee, msichana mmoja tu, na wasichana wengine, wameolewa. Baba yangu alituambia, asingependa msichana yeyote aolewe kabla hajafika Chuo Kikuu” 
 
Mawazo ya baba yake Raba yanadhihirishwa na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, zikionesha asilimia 5 pekee duniani kote ya wakimbizi ndio hupata fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu, na kwa wasichana takwimu ni chini zaidi ndio maana UNHCR na wadau wake wanashirikiana kuhakikisha wasichana wengi zaidi wanasoma Chuo Kikuu wakilenga kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2030 kama anavyoeleza Linet Aguko kutoka programu ya ufadhili wa Mastercard. 


“Wito wangu ni kwa watu walio tayari kujitokeza na kuwasaidia vijana hawa kujitokeza na kuwasidia, kwa namna yoyote ili waweze kunufuaika na fursa ya kupata elimu ambayo ipo kwa kila mtu” 
 
Akiwa chuoni Raba anapata elimu ambayo anaamini itaenda kusaidia jamii yake. “Nimechagua kozi hii kwa sababu nafanya kazi na wanawake na wasichana. Nyumbani nchini Ethiopia, nimeshuhudia madhila wanayopitia, na ndio maana nimeamua kusoma kozi ya Saikolojia “ 
 
Raba anasema amewaacha wasichana wengi wakiwa darasa la 12 wakitamani kupata fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu na atafurahi zaidi kama ataona wasichana wengi zaidi wakijiunga na masomo Chuo Kikuu.