Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi ashinda tuzo ya wakimbizi ya Nansen! Kulikoni?

Ameen Hussain Jubran , muasisi wa asasi isiyo ya kiserikali ya Jeel Albena
© UNHCR/Ahmed Haleem
Ameen Hussain Jubran , muasisi wa asasi isiyo ya kiserikali ya Jeel Albena

Mkimbizi ashinda tuzo ya wakimbizi ya Nansen! Kulikoni?

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa mataifa lakuhudumia wakimbizi UNHCR limeitangaza taasisi ya Jeel Albena ya nchini Yemen kuwa mshindi wa mwaka 2021 wa tuzo ya wakimbizi ya Nansen kutokana na kazi nzuri ya kuwasaidia wakimbizi wa ndani nchini humo. 

Ushindi wa taasisi hiyo ya Jeel Albena ya Yemen umetangazwa leo huko Geneva Uswisi, na Kamisha Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani Filippo Grandi akisema imejitolea kwa muda mrefu kuwasaidia maelfu ya wananchi wa Yemen walioathirika na mapigano na hivyo kuwa na mchango mkubwa. 

“Kila mwaka tunatoa tuzo kwa mtu au kikundi kilichoenda mbali zaidi ya majukumu yao kuwasaidia wakimbizi wa ndani na watu wasio na uraia. Taasisi ya Jeel Albena imefanya vizuri sana kusaidia watu wa pande zote za kwenye mzozo nchini Yemen. Wafanyakazi wake na watu wanaojitolea walikuwa kamili, walifanya kazi kwa umakini na kwa ukimya wakati mapigano yakiendelea, katika hali ya hatari ambapo wadau wengi walikimbia.” Amesema Kamishna Grandi. 

Taasisi hiyo imetoa malazi ya dharura kwa wakimbizi wa ndani 18,000 pamoja na wenyeji wao. Halikadhalika imesaidia maelfu ya wakimbizi kupata ujira, kujikimu na kurejesha heshima na utu wao.  
  
“Kauli mbiu yao ni “Na wayemeni kwa Wayemeni” ni mfano wa roho yao iliyojikita katika kutafuta suluhisho kwa pamoja na jamii ambazo wanafanya nazo kazi” amefafanua Kamishna Mkuu Grandi. 
  

Tuzo ya wakimbizi ya UNHCR Nansen kwa mwaka 2021 imeenda kwa Jeel Albena, taasisi inayotoa msaada kwa wakimbizi wa ndani nchini Yemen
© UNHCR/Abdulhakeem Obadi
Tuzo ya wakimbizi ya UNHCR Nansen kwa mwaka 2021 imeenda kwa Jeel Albena, taasisi inayotoa msaada kwa wakimbizi wa ndani nchini Yemen


Tuzo hiyo itakabidhiwa tarehe 4 mwezi ujao kwa muasisi wa taasisi hiyo Ameen Jubran ambaye naye alikuwa mkimbizi wa ndani na alinusurika kuuawa katika machafuko.  
Muasisi huyo amesema kitendo cha yeye kulazimika kuyakimbia makazi yake ya asili kimemzidishia morali wa kutaka kuwasaidia zaidi wakimbizi wa ndani. 

Kitendo cha tuzo na Nansen kupatiwa taasisi hiyo, kutawezesha dunia kuitazama Yemen zaidi na kuona madhila wanayokumbana nayo watu zaidi ya milioni 4 waliolazimika kuhama makazi yao na ambao kwa zaidi ya mwaka mmoja wamekuwa wakimbizi wa ndani na zaidi ya asilimia 80 wamekuwa wakimbizi kwa zaidi ya mwaka mmoja. 

Tuzo hiyo pia itasaidia kuonesha dunia kazi zinazofanywa na asasi nyingine za kiraia nchini humo. 
Kamishna Grandi amehitimisha taarifa yake kwa kusema “Jeel Albena ni mshindi anayestahili tuzo ya Wakimbizi ya Nansen, ambayo haitolewi tu na UNHCR, bali na kamati inayoongozwa na serikali za Norway pamoja na Uswisi. 
“Ni matumaini yangu makubwa tuzo hii itafanya jumuiya za kimataifa kutupia macho nchi ya Yemen na naamini wakiona kazi isiyo ya kawaida ya Jeel Albena watahamasisha hatua zaidi za kusaidia watu ambao wameteseka. Hongera kwa Jeel Albena “