Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimeshtushwa na kiwango cha mahitaji ya wakimbizi Burkina Faso- Grandi

Wanafamilia nchini Burkina Faso wakila mlo wao pekee wa siku (Aprili 2018)
WFP/Simon Pierre Diouf
Wanafamilia nchini Burkina Faso wakila mlo wao pekee wa siku (Aprili 2018)

Nimeshtushwa na kiwango cha mahitaji ya wakimbizi Burkina Faso- Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Watu wapatao 600,000 wamefurushwa makwao nchini Burkina Faso, baada ya kukimbia mkoa wa kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo kwenda majimbo ya jirani limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. 

Kwa mujibu wa UNHCR, wenyeji wao ambao ni raia wenzao wanakabiliwa na umaskini, upungufu wa huduma za afya, shule duni na mbinu za kujipatia kipato zinadidimia wakati joto linapoongezeka na uzalishaji wa ardhi zao unapungua.

Mapema wiki hii, kundi la watu wasiojulikana waliwaua raia 20 katika shambulio lililotokea katika kijiji cha Lamdamol kwenye jimbo la kaskazini mwa Seno. Shambulio hilo lilikuja wiki moja tu baada ya shambulio lingine kwenye soko katika mkoa wa Soum ambalo lilisababisha vifo vya watu 39. Hamidou Billarga ni chifu wa Kijiji ukanda wa Sahel.

(Sauti ya Hamidou)

"Kwetu sisi ni watu sawa, wale wanaokuja kuiba, wale wanaokuja kuua. Ni waislamu wenye msimamo mkali. "

Karibu asilimia 90 ya wakimbizi wa ndani nchini Burkina Faso wanaishi na familia zinazowahifadhi. UNHCR inawapa msaada wa makazi na vifaa muhimu vya msingi kwani wengi wa waliokimbia wamekimbia mikono mitupu.Katika ziara yake ya wiki hii, ukanda huo, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi ametembelea watu waliofurushwa walioko Kaya.

(Sauti ya Grandi)

"Nimeshtushwa na kiwango cha mahitaji ya kibinadamu. Hii ni dharura ya kibinadamu ya kiasi kikubwa. Watu hawa kimsingi hawana chochote."

Mkoa wa Kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo unahifadhi wengi wa wakimbizi hao. UNHCR na wadau wamekarabati makazi karibu 7,000 hapo lakini wanakadiria kuwa zaidi ya makazi 28,000 yanahitajika hivi sasa. Hamidou Billarga tena amesema

(Sauti ya Hamidou)

“Wengi wa watu kwenye familia yangu wamefika hapa lakini hawana chakula. Tunalala nje, na tunalazimika kuweka mali zetu nje, pia."

Juhudi za kibinadamu zinakwamishwa na ongezeko la vitisho kwa usalama wa wafanyikazi wa kibinadamu kutoka kwa vikosi vilivyo na silaha na kuifanya kuwa vigumu kuhudumia kila mtu aliye na mahitaji, ikiwemo maelfu ya wakimbizi wa Mali ambao Burkina Faso imewahifadhi tangu 2012.