Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la WHO la kuzuia watu kuwa viziwi lawanufaisha wananchi Zambia

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linataka serikali ziwekeze katika huduma za kuepusha watu kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia.
The London School of Hygiene & Tropical Medicine (LSHTM)/A. Smith
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linataka serikali ziwekeze katika huduma za kuepusha watu kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia.

Azimio la WHO la kuzuia watu kuwa viziwi lawanufaisha wananchi Zambia

Afya

Wakati takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha mtu mmoja kati ya watano anaishi na tatizo la kupoteza uwezo wa kusikia nchini Zambia programu maalum ya kuwasaidia wenye matatizo ya masikio kusikia sasa  imeanza kuzaa matunda. 

Nchini Zambia katika wilaya ya Kapiri Mposhi, Alice, mkulima na mama wa familia anaonekana kwenye video ya WHO akielekea kituo cha afya akiwa amembeba mwanae aitwaye Memory Chisenga mwenye umri wa miaka mitatu.

Alice anasema, ameamua kumpeleka mwanae kituo cha Lukomba baada ya kugundua kila anapomsafisha sikio au anapomuogesha, Memory alikuwa akilia na baada ya muda sikio likaanza kutoa usaha.

Mwaka 2017 shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO lilipitisha  azimio la kuzuia watu kuwa viziwi na kupoteza usikivu ambapo serikali ya Zambia nayo ikaanzisha programu maalum ya miaka 5 ya utoaji wa mafunzo kwa wauguzi wa afya ili kukabiliana na uchache wa wataalamu wa kutibu magonjwa ya masikio, pua na koo au ENT.

Takwimu za Zambia zinaonesha wataalamu watano wa ENT wanahudumia watu milioni 17 na hivyo ili kukabiliana na uhaba huo, WHO ikapatia mafunzo watoa huduma hiyo na miongoni mwao ni muuguzi Carol Sinkende ambaye kwa miaka 2 amehudumia zaidi ya wagonjwa 600 akiwemo mtoto Memory.

“Memory Chisenga amekuwa mgonjwa wangu tangu mwezi Desemba mwaka jana wa 2020. Wakati mtoto aliletwa alikuwa na ugonjwa sugu kwenye sikio. Sikio la kushoto lilikuwa limetoboka. Tangu nianze kumhudumia tobo limepungua kwa sababu ya dawa na hii ni dalili kwamba mtoto anapona vizuri."

Alice anafurahia huduma akisema, “Nilitaka kwenda kutafuta dawa. Hapo ndipo nilipoambiwa kwamba kuna muuguzi huko Pula ambaye anafanya kazi ya kutibu masikio. Bila kusita nilienda. Alipomkagua akagundua tatizo na kumpatia dawa.  Zahanati hii ya muuguzi  Carol inafanya kazi vizuri sana, imetusaidia sana. Awali i hatukuweza kusafiri kwa gari kwenda Kapiri Mposhi kupata huduma.”

Muuguzi Carol ambaye kabla ya mafunzo hayo ya kutibu magonjwa ya masikio alifanya kazi kampuni ya mawasiliano, anasema ana mpango wa kujiendeleza kielimu ili aweze kuwa na ushawishi kwenye utungaji será kwa ajili ya watu wenye shida ya usikivu.