Sifa ya majaribio ya nyuklia sio chochote bali ni uharibifu- Guterres

29 Agosti 2019

Leo Agosti 29 Umoja wa Mataifa umeadhimisha siku ya kupinga majaribio ya nyuklia na kutoa wito kwa kuridhiwa kwa mkataba wa kupiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia, CTBT kwa nchi wanachama ambao hawajafanya hivyo.

Kupitia ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa mataifa kuridhia mkataba huo wa CTBT na kwamba, “sifa ya majaribio ya nyuklia sio chochote bali ni uharibifu.”

Katibu Mkuu amesema mkataba wa CTBT ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha hakuna majeruhi na ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza usitishaji wa vifaa vya nyuklia

Guterres amesisitiza wito wake kwa mataifa ambayo ni muhimu kwao kuridhia mkataba wa CTBT akisema, “katika dunia kunakoshuhudiwa ongezeko la uhasama, usalama wa pamoja ni muhimu.”

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa takriban majaribio elfu mbili yamefanyika tangu kuanza kwake mnamo Julai 16 mwaka 1945

Umoja wa Mataifa umesema kwamba katika hatua za awali madhara mabaya ya majaribio hayo kwa uhai wa binadamu na athari za hatari za majaribio ya nyuklia kwa mazingira hayakuzingatiwa kwa kina.

UN News/Nargiz Shekinskaya
Mtazamo wa kituo cha majaribio ya nyuklia ya Semipalatinsk Kurchatov, Kazakhstan ambako muungano wa Soviet walikuwa wanafanya majaribio ya silaha za nyuklia.

Kwa muda mrefu hatari zitokanazo na athari za silaha za nyuklia zimetanabaishwa, hususan pale kuna mapungufu katika  mazingira yaliyosimamiwa na wakati huu ambapo kuna  silaha hatir zaidi zilizoko zama zas asa.

Siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya silaha za nyuklia ilitangazawa mwaka 2009 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na maadhimisho yamefanyika tangu mwaka 2010 huku kukiwa na shughuli mbali mbali kote ulimwenguni.

Azimio hilo linatoa wito kufanyike uelimishaji na uchagizaji zaidi kuhusu madhara ya silaha za nyuklia na majaribio au aina zingine za milipuko na umuhimu wa kutokomeza shughuli hizo kama sehemu ya kufikia lengo la dunia isiyo na silaha za nyuklia.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud