Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana na mageuzi ya kilimo Tanzania- Shambani hadi kiganjani

Nyuso za furaha kutoka kwa wanakikundi cha Ushindi mkoani Kigoma baada ya mavuno bora kufuatia mafunzo ya mbinu bora za kilimo kutoka FAO ambazo walitumia kwenye shamba darasa.
FAO Tanzania
Nyuso za furaha kutoka kwa wanakikundi cha Ushindi mkoani Kigoma baada ya mavuno bora kufuatia mafunzo ya mbinu bora za kilimo kutoka FAO ambazo walitumia kwenye shamba darasa.

Vijana na mageuzi ya kilimo Tanzania- Shambani hadi kiganjani

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuelekea mkutano wa viongozi duniani kuhusu mfumo endelevu wa chakula uliwenguni mwezi Septemba mwaka huu 2021, mkutano tangulizi utafanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 mwezi huu wa Julai huko jijini Roma nchini Italia, hivyo shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO limekuwa likiendesha mijadala na makundi mbalimbali ili kupata sauti zao za nini kifanyike ili kuwa na mifumo endelevu ya chakula na hatimaye kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2030.

 

Soundcloud

Nchini Tanzania FAO imeendeleza mijadala hiyo kwa kukutanisha vijana wakati wa mkutano uliofanyika mkoani Dodoma nchini humo.

Miongoni mwa vijana walioshiriki ni Alicia Venant Mkurugenzi wa jukwaa la mtandaoni la soko la kidijitali Amdestiny.com kutoka mkoa wa Kilimanjaro ambaye amezungumzia wajibu wa vijana katika kuhakikisha anapata ustawi wa maisha yake na taifa kwa ujumla na ushiriki wao katika kuboresha mfumo mzima wa kilimo. Alicia anasema, “tumefurahishwa sana kwa kuwa vijana sisi ndio tunapaswa kuzungumzia masuala yetu. Tunatakiwa kusema fursa tunazoziona, changamoto tunazopata na kuiamsha serikali pindi tunapoona imetusahau kwa namna moja au nyingine. Sisi tuna uwezo na tunaendelea kuamka na kupambana. Hapa tunaangalia suala la masoko, uchakataji wa mazao na uzalishaji shambani.”

Vijana ‘bongo zetu zimelala’ – Alicia

Alicia anarejea tena kutuambia uzingatiaji wa mlo kamili kwa vijana una umuhimu gani na yeye ameshiriki vipi kuleta mwamko kwa vijana wenzake akisema, “tunahitaji vyakula vyenye lishe ili ubongo wetu uchangamke, unajua vijana wengi sasa hivi bongo zetu zimelala sana. Tunakula hivyo viazi na mayai na kuacha vyakula vyetu vya asili ambavyo wazee wetu zamani walikula na walikuwa na afya.”

Bi. Venant anasema wameibuka na jukwaa www.AmDestiny.com ambalo “linakutanisha wakulima, wanunuzi na wasafarishaji. Hii tumeanzisha baada ya kupata changamoto ya kutopata bidhaa kwa wakati. Kwa hiyo jukwaa hilo linamwezesha mtanzania yeyote hata kama yuko nje ya nchi kupata taarifa ya mkulima yuko wapi na ana bidhaa ipi.”

Mkulima akikagua mahindi yaliyozingatia mbinu bora za kilimo
FAO Tanzania
Mkulima akikagua mahindi yaliyozingatia mbinu bora za kilimo

Mitandao ya kijamii na mageuzi katika lishe

Prince Kweka anatueleza namna mitandao ya kijamii inavyoweza kutumika kuleta mageuzi katika suala la lishe kwa vijana na jamii nzima akisema, “katika jukwaa hili tumeangalia ifikapo mwaka 2030 tuwe na maisha tofauti. Tuwe tumemaliza njaa, utapiamlo na tuendeleze lishe bora. Tunatumia hii dunia ya sasa kwa njia nzuri ambapo ndani ya apu ya ShambaDuniaMarket kuna eneo la taarifa ambako unapata taarifa zote kuhusu kilimo. Tumesaidia sana katika watu kupata masoko na hivyo tumetumia jukwaa hili kufanikisha SDGs.”

Prince anawaambia vijana kuwa kupitia kilimo biashara kijana anaweza kupata kipato na kukabili changamoto ya ajira huku akitoa wito kwa vijana wenzake.
“Ndani ya ShambaDunia sisi vijana ni wakulima, mimi mwenyewe ni mfugaji na mkulima. Kwa hiyo tunatumia fursa na taarifa tunazopata na kuwapatia watu wengine wanaotaka. Vijana lazima tubadili fikra zetu, kukaa ofisini si suala kubwa sana, tujifunze kuwekeza. Unawekeza kwenye kilimo unabadili maisha yako na ya wengine.”

Mwaka wa 2021 umetengwa kwa ajili ya mbogamboga na matunda.Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo
© FAO-Magnum Photos/Alex Webb
Mwaka wa 2021 umetengwa kwa ajili ya mbogamboga na matunda.Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo

Na Mbazi Marisa kutoka Global Shapers Community anaweka wazi mikakati waliyonayo baada ya kukamilika kwa mjadala kuwafikiwa vijana hasa vijijini kwa kuzingatia ukuaji wa teknolojia akisema wao wana jumuiya zisizopungua 400 katika nchi 175 na wana wanachama wapatao 1,000 na zaidi ya yote, tunapoelekea ni kwenye intaneti na si kila mtu anayo, hivyo kwa hao hao wachache tulionao tunafikisha ujumbe.”

Akizungumzia mjadala huo, Mtaalamu wa Lishe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la  Kilimo na Chakula , FAO, Stella Kimambo amesema, “kama unavyofahamu vijana ni sehemu kubwa ya taifa letu tunakusanya mawazo yao kuhusu mifumo ya chakula na tunalenga uzalishaji, usindikaji, usafirishaji mpaka chakula kinapofika mezani, kwa hiyo kila mmoja ana nafasi yake ya kufanya. Kwa sababu mifumo ya chakula siyo lishe peke yake. Tunataka kuangalia mifumo mipya ya chakula na hata kubadili ile sahani ya kijana mezani maana unaona vijana wetu sasa hivi wana makundi ya chakula ambayo wanachagua na mengine hawayapati na husababisha wawe na lishe pungufu au viriba tumbo.”

Mwongozo wa ulaji chakula Tanzania mbioni

Baada ya kupokea mawazo ya vijana, FAO Tanzania inaandaa mpango wa utekelezaji na zaidi ya yote, “kuhusu suala la chakula, hivi sasa tunaandaa mwongozo wa chakula kwa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Kila mtu ataupata ili atambue sahani ya chakula iwe na nini na kwa kiasi gani, mfano matunda kiasi gani, ugali kiasi gani, mboga kiasi gani, huo mwongozo utakamilika karibuni kwa ajili ya wateja wetu.”