Maeneo ya kilimo yakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji- SOFA

26 Novemba 2020

Zaidi ya watu bilioni 3 wanaishi kwenye maeneo ya kilimo ambayo yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na nusu yao wanakabiliwa hawana maji ya kutumia, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo mjini Roma,  Italia na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.
 

Ripoti hiyo kuhusu hali ya chakula na kilimo duniani, SOFA, inasema kuwa sambamba na uhaba huo, kiwango cha mtu mmoja kupata chanzo cha maji kimepungua kwa zaidi ya asilimia 20 katika miongo miwili iliyopita, hali inayotilia umuhimu suala la kilimo kinachotumia maji machache.

Sekta ya kilimo ndio inayoongoza duniani kwa matumizi makubwa ya maji ambapo FAO inasema usimamizi mzuri kwenye matumizi ya maji “ikiwemo kuwepo kwa haki ya kumiliki maji, usimamizi na ukaguzi katika matumizi ya maji ni muhimu ili dunia iwe na uhakika wa chakula na lishe kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.”

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu anasema katika utangulizi wa ripoti hiyo ya mwaka huu wa 2020 kuwa inatuma ujumbe mzito ya kwamba uhaba wa maji katika sekta ya kilimo ni suala linalopaswa kushughulikiwa kwa ujasiri iwapo ahadi ya kimataifa kupitia SDGs inatakiwa kutimizwa.

Wanawake nchini Madagaska wanapanda mboga kwenye ardhi kwa kutumia mfumo mdogo wa umwagiliaji, ambapo WFP inatoa fursa za mapato kwa mashirika ya wakulima wamiliki wadogo.
WFP/Giulio d'Adamo
Wanawake nchini Madagaska wanapanda mboga kwenye ardhi kwa kutumia mfumo mdogo wa umwagiliaji, ambapo WFP inatoa fursa za mapato kwa mashirika ya wakulima wamiliki wadogo.

Hatua za kuchukua

SOFA2020 inataja hatua za kuchukua kuanzia kuwekeza katika uvunaji wa maji, uhifadhi wa maji kwenye maeneo yanayotegemea mvua na kuboresha mifumo ya umwagiliaji kwenye maeneo ambako kilimo kinategemea mfumo wa umwagiliaji.
Halikadhalika kilimo cha kiuchumi kama vile, kulima mazao yanayostahimili ukame, kuwa na mbinu bora za usimamizi wa maji.
Ripoti hiyo inasema kuwa kufanikisha SDGs ikiwemo lengo namba mbili la kutokomeza njaa ni jambo linalowezekana lakini “kwa kuhakikisha kuna mifumo thabiti na fanisi ya matumizi ya maji ikiwemo yale yatokanayo na vyanzo vya asili na yale ya mvua.”

Maji ni rasilimali muhimu

Ripoti inasema kuwa maji yanapaswa kutambuliwa kama kitu chenye thamani na chenye bei ikiongeza “tabia iliyozoeleka imefanya maji kuonekana kuwa bidhaa ya bure a hivyo kuiondolea thamani sokoni. Bei inayoakisi thamani halisi ya maji, inaweza kutuma ujumbe sahihi kwa watumaiji wa maji ili waweze kuyatumia kwa busara zaidi.”

Wakati huo huo ni lazima kuwepo na sera na usimamizi bora wa kuhakikisha kuwa kila mtu anapata huduma hiyo adhimu.

Ripoti inaongeza kuwa usimamizi wa maji lazima uangazie tatizo na uendane na wakati na kwamba wakazi wa vijijini wanaweza kunufaika zaidi kupitia mifumo ya umwagiliaji.

Umwagiliaji kusongesha Afrika lakini tatizo ni mitaji

Kati ya mwaka 2010 na 2050, ripoti inasema kuwa maeneo ya mavuno yatokanayo na umwagiliaji yanatarajiwa kuongezeka katika maeneo mbalimbali duniani lakini ongezeko litakuwa maradufu katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara mamilioni ya wakazi wa vijijini watanufaika.

Ripoti inadokeza kuwa katika baadhi ya maeneo, mifumo ya umwagiliaji kwa wakulima wadogo wadogo itakuwa na ufanisi zaidi kuliko miradi mikubwa ya umwagiliaji.

Hali hiyo inatia matumaini zaidi kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambako vyanzo vya maji vya ardhini bado havijaendelezwa vya kutosha n ani asilimia 3 tu ya eneo la kilimo ndio linatumia mifumo ya umwagiliaji.

Hata hivyo uendelezaji wa mifumo ya umwagiliaji unakumbwa na vikwazo kadhaa ikiwemo ukosefu wa haki za umiliki wa maji sambamba na ukosefu wa mitaji na mikopo.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter