Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani kutoa milioni 135.8 kusaidia wakimbizi wa kipalestina

Ghada Krayem, mkimbizi wa kipalestina, akipokea mafunzo ya ufundi wa umeme wa jua katika kituo cha GTC
© 2021 UNRWA/M.Hinnawi
Ghada Krayem, mkimbizi wa kipalestina, akipokea mafunzo ya ufundi wa umeme wa jua katika kituo cha GTC

Marekani kutoa milioni 135.8 kusaidia wakimbizi wa kipalestina

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la usaidizi kwa wakimbizi wa kipalestina - UNRWA limetangaza Marekani inachangia milioni 135.8 ilikuwezesha kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakimbizi. 

Taarifa kwa vyombo vya Habari iliyochapishwa kwenye wavuti wa UNRWA, imesema ufadhili huo umekuja baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya mfumo wa ushirikiano baina yao na Marekani wenye lengo la kusaidia katika masuala mbalimbali ya maendeleo na kulinda wakimbizi wa kipalestina.

Kamishna wa UNRWA Pilippe Lazzarini amesema “Kusainiwa huku kwa makubaliano ya mfumo wa ushirikiano, na nyongeza ya ufadhili kunaonesha sisi tuna mshirika wetu Marekani ambaye anaelewa hitaji la kutoa msaada muhimu kwa wakimbizi walio katika mazingira magumu”

Ufadhili huo unaenda kusaidia katika maeneo mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa shule zaidi ya 700 zenye Watoto zaidi ya nusu milioni na vituo vya afya 140. Fedha hizo zitatumika kununua chakula, kutoa msaada wa fedha kwa wakimbizi, msaada wa kisaikolojia kwa wakimbizi, huduma za maji, janga la Corona au COVID-19 na shughuli nyingine nyingi. 
Pia zitasaidia katika changamoto mbalimbali za misaada ya kibinadamu katika nchi za Syria, Lebanon, Jordan na ukanda wa Gaza.

Taarifa hiyo imeeleza makubaliano kati ya UNRWA na Marekani yanathibitisha kujitolea kwa pande zote mbili katika kutekeleza malengo ya Umoja wa Mataifa ikiwemo kanuni ya kutofungamana na pande zozote. 
Mwezi April mwaka huu Marekani ilitangaza kurejea kusaidia Palestina na kutoa msaada wa milioni 150 kwa ili kuokoa maisha ya wakimbizi wa kipalestina waliotapakaa katika ukanda wa mashariki ya kati. 
Mwezi Mei Marekani pia ilitoa msaada wa kibinadamu wenye thamani ya jumla ya milioni 33 kusaidia waathirika wa machafuko katika ukanda wa Gaza.