Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Wanawake wa Ukraine, wanaokimbia mzozo wakisubiri lifti ili kufikia kituo cha wakimbizi nchini Poland.

WHO yatoa huduma za matibabu na usaidizi wa kisaikolojia kwa wakimbizi wa Ukraine

© Daniele Aguzzoli
Wanawake wa Ukraine, wanaokimbia mzozo wakisubiri lifti ili kufikia kituo cha wakimbizi nchini Poland.

WHO yatoa huduma za matibabu na usaidizi wa kisaikolojia kwa wakimbizi wa Ukraine

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limejizatiti kuhakikisha wakimbizi kutoka Ukraine wanapatiwa msaada wa huduma za matibabu na usaidizi wa kisaikolojia.

"Nipo peke yangu, nipo pekeyangu" ndivyo alivyosema Valentina mwenye umri wa miaka 67 aliyewasili kwenye kituo cha wakimbizi cha Horodlo nchini Poland akitokea Bila Tserkva nchini Ukraine akikimbia vita inayoendelea nchini mwake. Valentina aliugua polio tangu angali mdogo na hivyo ana ulemavu wa kutembea. Safari ya kutoka Ukraine ilikuwa ngumu, alisafiri kwa siku tatu hadi kufika kituoni. Alilazimika kubebwa kutoka gari moja hadi jingine. Sasa ameshaonana na daktari aliyempatia dawa za maumivu huku akimsubiri binti yake amchukue kwenda kuishi naye nchini Israel. Beate Sawicka ni muuguzi kwa zaidi ya miaka 34 nchini Poland, anayefanya kazi katika kituo chakupokea wakimbizi cha Dorohusk na anasema sasa idadi ya wazee ni kubwa na wana magonjwa sugu. Pia kuna watu wenye ulemavu, tofauti na hapo awali walikuwa wakipokea wakina mama na watoto. “Moyo wangu unavunjika kuwaona wakiwa katika hali hii. Wao sio wagonjwa tu, bali pia wamechoka, wamechoka sana, wanatokwa machozi. Tunajaribu kuwasaidia iwezekanavyo. Kuna baadhi yao inabidi tuwabadilishe nepi wakiwa wamekaa kwenye viti mwendo ili tusiwazungushe sana. Nimeifanya kazi hii ya uuguzi kwa miaka 34. Nimekuwa nikihudumia wagonjwa wa aina hii lakini hali zao zinazofaa wawe hospitalini. Hapa kuna baridi, wachafu, kwa sababu wanasafiri kwa saa 48. Moyo wangu unapasuka, hali inatisha kwa tunachokiona hapa.” Nako katika eneo la Krowico Sama Mtaalamu wa afya ya akili na msaada wa kisaikoloji na jamii wa WHO Selma Sevkli, anazungumza na Olga, msichana mwenye umri wa miaka 20 mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu nchini Ukraine aliyekuwa anasomea udaktari lakini sasa anaona ndoto zake zimezimika. “Unachojisikia, unachopitia ni kawaida sana. Huenda nyakati fulani ukahisi: ‘Kwa nini sina nguvu?’, ‘Ni nini kitakachotokea?’, unakuwa na uoga, yote hayo ni ya kawaida sana. Kila mtu anapitia jambo lile lile. Hivi sasa jaribu kuwa na utulivu. Umezungukwa na watu wengi wenye mioyo mizuri ambao wanajaribu kuwasaidia kutoka kote ulimwenguni. Kila mtu anajaribu kusaidia. Olga akizungumza na mtaalamu wa WHO amesema wanahitaji msaada wa kisaikolojia kwa hali na mali kwa kuwa watu wengi wamechanganyikiwa na wamepoteza matumaini akitolea mfano mama yake ambaye amekuwa akilia muda wote na kuangalia habari kwenye simu yake ya mkononi huku mdogo wake akiwa hataki kabisa kucheza au kujihusisha na mtu yeyote na akitaka jambo moja tu, kurudi nyumbani. WHO imeeleza kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanaandaa usaidizi sio tu katika vituo ya kuwapokea wakimbizi wanaoingia nchini Poland bali wanahakikisha wakimbizi hao wanapata usaidizi unaohitaji wa afya ya akili na mahitaji mengine katika maeneo wanayoelekea baada ya kuondoka kituoni hapo.