Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saa chache baada ya kuenguliwa kwenye Ukamishna Mkuu wa UNRWA, Pierre Krähenbühl, ajiuzulu

Kamishna Mkuu wa UNRWA aliyejiuzulu leo 6 Novemba 2019, Pierre Krähenbühl. Picha hii ni ya tarehe 11 Desemba 2018
UN
Kamishna Mkuu wa UNRWA aliyejiuzulu leo 6 Novemba 2019, Pierre Krähenbühl. Picha hii ni ya tarehe 11 Desemba 2018

Saa chache baada ya kuenguliwa kwenye Ukamishna Mkuu wa UNRWA, Pierre Krähenbühl, ajiuzulu

Msaada wa Kibinadamu

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, Pierre Krähenbühl, amejiuzulu hii leo, ikiwa ni saa chache baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kumteua Christian Saunders kuwa kaimu Kamishna Mkuu wa shirika hilo ambalo sasa linagubikwa na ukata.

Guterres alimtangaza Saunders kukaimu nafasi hiyo, baada ya kujulisha kuwa ofisi ya uchunguzi wa ndani ya Umoja wa Mataifa, OIOS, imekamilisha sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu masuala ya usimamizi wa UNRWA.

Matokeo ya uchunguzi huo yamebainisha masuala ya usimamizi ambayo yanahusika moja kwa moja na Kamishna Mkuu Pierre Krähenbühl. 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mchana huu jijini New York, Marekani kuwa Guterres amemshukuru Krähenbühl kwa kujitolea kwake kwa UNRWA na wakimbizi wa Palestina.

Aidha amesema ni muhimu sana hivi sasa kwa nchi wanachama kusalia na imani kwa UNRWA na huduma ambazo inatoa na kwamba, “jamii ya  kimataifa iendelee kusaidia kazi muhimu inayofanywa na UNRWA kwenye maeneo ya afya, elimu, misaada ya kibinadamu, kazi ambayo ni muhimu kwa utulivu wa eneo hilo lililo na mzozo.”

Taarifa zinasema kuwa matokeo ya uchunguzi huo wa awali hayajumuishi tuhuma dhidi ya Kamishna Mkuu kwenye matumizi mabaya ya fedha bali ni masuala tu ya kiusimamizi ambayo yanapaswa kushughulikiwa.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu alikuwa amemwagiza Krähenbühl aende likizo wakati uchunguzi huo ukiendelea ili hatimaye uamuzi ufanyike na hatua sahihi ziweze kuchukuliwa.

Katika miezi michache iliyopita, UNRWA ilianzisha tathmini ya ndani ya utawala, usimamizi na uwajibikaji ili kuhakikisha kuwa vitendo vyake vinakidhi viwango vya juu vya ueledi, uwazi na ufanisi.

Tathmini hiyo ilibaini maeneo kadhaa yanayohitaji kuimarishwa na shirika hilo tayari limeanza hatua sahihi na litachukua hatua zaidi ili kujiimarisha.