Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usugu zaidi wa dawa dhidi ya E.Coli na magonjwa ya zinaa waripotiwa

Unywaji wa maji machafu ni moja ya sababu ya kupata maambukizi ya bakteria wa E.Coli
© UNICEF/UN066040/Souleiman
Unywaji wa maji machafu ni moja ya sababu ya kupata maambukizi ya bakteria wa E.Coli

Usugu zaidi wa dawa dhidi ya E.Coli na magonjwa ya zinaa waripotiwa

Afya

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kuhusu ufuatiliaji wa maambukizi ya magonjwa katika maabara na matokeo ya usugu wa dawa dhidi ya vijiumbe maradhi, GLASS, inatia matumaini kuwa hivi sasa maabara nyingi zinafanya uchunguzi wa usugu huo na hivyo kutoa fursa ya utafiti na kudhibiti usugu wa dawa.
 

Ripoti hiyo inasema wito wa nchi nyingi sasa zinaweka maeneo ya ufuatiliaji kwa kuwa “miaka mitano iliyopita tulipofanya uchunguzi wa kuandaa ripoti kama ya sasa kulikuweko na maeneo 700 pekee ya ufuatiliaji wa maambukizi yatokanayo na usugu wa dawa na sasa idadi ya maeneo hayo imeongezeka hadi elfu 74,” amesema Dkt. Hanan Balkhy, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO.

Usugu wa madawa dhidi ya viuavijiumbe maradhi, AMR ni nini?
WHO inasema usugu huo unatokea pindi vimelea, virusi au ukuvu na bakteria vinabadilika na kuwa haviwezi tena kutibika kwa dawa na hivyo kuongeza hatari ya kusambaa kwa magonjwa, magonjwa kuwa sugu.

WHO inasema hali hiyo inachochewa na matumizi kupita kiasi ya viua vijiumbe maradhi “na hii ni changamoto kubwa ya kufanikisha malengo ya kiafya ya kimataifa na inaongeza mzigo mkubwa katika uchumi wa taifa na kimataifa.”

Tweet URL

WHO inasema matumizi kupita kiasi pia ya dawa hizo huweza kusababisha kifo, ulemavu, magonjwa yanayosababisha mgonjwa kuwepo hosptali kwa muda mrefu.

Usugu ni kwenye magonjwa yapi zaidi?

Ripoti hiyo ya WHO inaonesha ongezeko kubwa kwenye maambukizi ya damu yanayosababishwa na bakteria aina ya E.coli ambapo bakteria huyo anagomea kutibika na kizazi cha tatu cha dawa aina ya cephalosporins  huku magonjwa ya zinaa nayo yakigomea dawa zao.

Usugu wa tiba dhidi ya magonjwa hayo umeripotiwa zaidi katika nchi za kipato cha chini na kati kuliko nchi tajiri “na hili linatia wasiwasi mkubwa kutokana na uwezo mdogo wa nchi hizo maskini kufikia tiba za kisasa na fanisi dhidi ya maambukizi hayo.”

Usugu pia umeripotiwa kwa tiba dhidi ya ugonjwa wa maambukizi katika njia ya mkojo.
WHO inataka kupanua wigo wa GLASS kwenye matumizi ya viua vijiumbe maradhi na inatiwa moyo zaidi kwa kuwa katka nchi 109, nchi 107 zinafuatilia dawa hizo wanazopatiwa wagonjwa katika kipindi fulani ili kufahamu ufanisi wake.